MUSEVENI ALILAUMU KANISA MAUAJI YA OFISA WA POLISI

0
1007

KAMPALA, UGANDA


RAIS Yoweri Museveni amesema kelele kutoka kanisani huenda ziliwafanya polisi wa Uganda wasisikie milio ya risasi iliyomuua afisa mwandamizi wa polisi, Muhammad Kirumira.

Watu wenye silaha waliokuwa kwenye pikipiki maarufu kama bodaboda, walimpiga risasi Kirumira hadi kufa Jumamosi ya wiki iliyopita wakati akielekea nyumbani kwake katika mji wa Bulenga.

Mkewe ambaye pia alikuwa naye katika gari hilo aliuawa.

Mauaji ya Kirumira ni ya karibuni katika mlolongo wa mashambulizi dhidi ya wanasiasa na maofisa wa polisi yaliyoibua hofu ya kuzidi kukosekana kwa usalama nchini Uganda.

Alikuwa kamanda wa zamani wa polisi wa Wilaya Buyende na video ambayo anaonekana kuwataka watu wawafichue ‘mafia’ kuliokoa taifa imesambazwa sana katika mitandao ya jamii tangu kifo chake.

Akizungumza kwenye televisheni Jumatatu usiku, aliwalaani wauaji kuwa nguruwe waoga.

Kulikuwa na polisi katika eneo hilo, lakini walisema hawakusikia milio ya risasi. Kuna uwezekano hawakusikia kwa sababu karibu na eneo kuna kanisa na katika kanisa daima tumekuwa tukipiga kelele kana kwamba Mungu ni kiziwi,” kiongozi huyo wa Uganda alisema.

Aliapa kwamba polisi watajaza pengo la usalama ambalo limetengenezwa na wauaji na kwamba mfumo wa kielektroniki wa utambuzi wa bodaboda utasaidia kutambua watu hawa.

“Jeshi la Uganda limeanza kuweka kamera za CCTV na hatua nyingine zinawekwa ili kuwakomesha hawa nguruwe kwa kuachana na mbinu za zamani za kipolisi,” alisema.

Ripoti zimekuwa zikieleza kwamba Kirumira mara kwa mara alikuwa akiviambia vyombo vya habari na maofisa wengine wa polisi kuwa amekuwa mlengwa wa njama za kumuua.

Alisimamishwa ukamanda wa wilaya , mwaka huu baada ya kuwatuhumu katika mtandao wa facebook polisi wenzake kwa rushwa na kushirikiana na magenge ya uhalifu.

Na alikuwa akisubiri mashitaka ya jinai, matumizi mabaya ya mamlaka wakati wa kifo chake.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here