MUSA AFUNGUA KITUO CHA MAFUTA NIGERIA

0
2

KANO, NIGERIA


MSHAMBULIAJI wa klabu ya Leicester City na timu ya Taifa ya Nigeria, Ahmed Musa, amefanikiwa kufungua kituo cha pili cha mafuta mjini Kano nchini humo.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24, amewafurahisha idadi kubwa ya mashabiki wa soka nchini humo kwa kuongeza kituo cha pili cha mafuta ambacho kinaweza kutoa huduma kwa gari sita kwa wakati mmoja.

Kituo hicho kipo umbali wa kilomita 500 kutoka kwenye mji aliozaliwa, lakini ameamua kukiweka umbali huo ili kuweza kuwahudumia mashabiki wake wengine ambao wapo mbali na eneo lake.

Maisha ya wachezaji wa soka si ya miaka mingi sana, hivyo mchezaji huyo ameamua kutumia fedha zake vizuri kwa kuwekeza katika biashara mbalimbali ikiwa pamoja na kituo kikubwa cha mazoezi.

Mchezaji huyo alikuwa nchini humo hivi karibuni wakati wa michezo ya kimataifa ya kalenda ya Fifa, lakini aliweza kutumia nafasi hiyo kufungua kituo hicho na kuna wakati alikuwa anatoa huduma ya mafuta yeye mwenyewe.

Kitendo hicho cha kutoa huduma yeye mwenyewe kiliwafanya mashabiki mbalimbali kujitokeza na magari yao ili awahudumie na kisha kupiga naye picha.

Kupitia ukurasa waka wa Instagram, mchezaji huyo aliweza kuposti baadhi ya picha huku akiwa anatoa huduma na nyingine akiwa na mashabiki wake.

Mchezaji huyo alijiunga na klabu ya Leicester City mwaka jana baada ya kufanya vizuri kwenye klabu yake ya CSKA Moscow ya nchini Urusi huku akifunga mabao 42 kutokana na michezo 125 na tangu amejiunga na Leicester City amefanikiwa kucheza michezo 18 ya ligi na kupachika mabao 2, wakati huo katika timu ya Taifa akicheza jumla ya michezo 63 na kupachika mabao 13.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here