23.3 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

MOURINHO AFURAHIA LUKAKU KUCHEZA UBELGIJI

MANCHESTER, ENGLAND


KOCHA wa klabu ya Manchester United, Jose Mourinho, ameshindwa kuzuia hisia zake baada ya kuona mshambuliaji wake, Romelu Lukaku, amepewa namba katika kikosi cha timu ya Taifa dhidi ya Cyprus, Jumanne wiki hii.

Katika mchezo huo wa kuwania kufuzu Kombe la Dunia 2018 nchini Urusi, Lukaku alitumia dakika 66 kabla ya kutolewa nje na kocha wao Roberto Martinez, lakini Mourinho amedai kuwa ana furaha kwa kuwa mchezaji huyo atakuwa tayari amepona tatizo la enka.

Mchezaji huyo anaongoza katika kupachika mabao kwenye Ligi Kuu nchini England akiwa na mabao 7, lakini baada ya kuumia enka kocha huyo alikuwa na wasiwasi kwamba atakuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu na kuukosa mchezo dhidi ya Liverpool kesho kwenye Uwanja wa Anfield.

“Kama kweli Lukaku alipata nafasi ya kucheza kwa dakika zote hizo kwenye timu yake ya Taifa, basi tayari atakuwa amepona majeraha yake.

“Ninaamini ulikuwa mchezo muhimu sana kwao na ndio maana alipewa nafasi, hivyo hata huku nafasi yake bado ipo wazi kuelekea mchezo dhidi ya Liverpool,” alisema Mourinho.

Hata hivyo, kocha huyo ameweka wazi kuwa hawezi kumtumia mchezaji wake Marouane Fellaini, ambaye alikuwa kwenye kikosi cha Ubelgiji, kwakuwa amepata tatizo la goti japokuwa amejiunga na Man United katika mazoezi ya jana.

“Suala la wachezaji kuumia linanipa wakati mgumu, lakini siwezi kulalamika sana kwa kuwa ni sehemu ya soka, lazima wachezaji waumie kutokana na mikiki mikiki wanayokutana nayo kila siku mazoezini hadi kwenye michezo yao,” aliongeza Mourinho.

Kocha huyo aliongeza kwa kusema amekuwa na wakati mgumu akiwa kwenye Uwanja wa Anfield, lakini hana wasiwasi sana kuelekea mchezo huo wa kesho huku akidai kuwa kikosi chake kimekamilika na ana uhakika wa ushindi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles