24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

MENO YA TRA YALIZA VITUO VYA MAFUTA

Na WAANDISHI WETU

MZOZO wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na wafanyabiashara wa mafuta juu ya matumizi ya mashine za risiti za kielektroniki (EFDs), umesababisha usumbufu kwa wamiliki wa magari na wasafiri, baada ya vituo vya kuuzia mafuta kufungwa.

Hatua hiyo ya TRA kufunga vituo vya mafuta, imeanza juzi baada ya hivi karibuni, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, kufungia kituo kimoja cha mafuta jijini Dar es Salaam, kwa kukosa mashine hiyo, huku akisema wafanyabiashara wasiotumia mashine hizo wamekuwa wakiibia serikali.

Kwa taarifa ambazo gazeti hili limeweza kuzikusanya mpaka jana, Mwanza vituo vilivyofungwa ni 72, Arusha 40, Moshi vinane, Tanga 13 kati ya 15, Manyara vitano na Dodoma 15, Dar es Salaam 20 na Pwani 17.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Udhibiti, Maji na Nishati (Ewura), vituo vya mafuta nchini ni zaidi ya 1,400, huku Dar es Salaam peke yake kuwa na vituo 200.

Katika jiji la Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo, alisema zaidi ya vituo 25 vimefungwa.

Hata hivyo, hakuweza kutoa taarifa kwa undani kwa kile alichosema kuwa bado zoezi hilo linaendelea.

Kwa Mkoa wa Pwani, Mtanzania ilishuhudia zaidi ya vituo 17 vikiwa vimefungwa.

Katika hatua nyingine, Kayombo, alisema kwa sasa hawezi kusema ni vituo vingapi kwa nchi nzima vimefungwa na kwamba zoezi la ufungaji wake ni endelevu.

Kayombo alisema hatua ya kufungia vituo vya mafuta imetokana na  zoezi la  ukaguzi wa mashine  za EFDs, ambalo linafanyika nchi nzima.

“Hilo ni zoezi endelevu la kukagua risiti na mashine za EFDs, linafanyika nchi nzima,” alisema Kayombo.

Alipoulizwa ni vituo vingapi vimefungiwa mpaka sasa pamoja  na kutakiwa kutaja idadi ya vituo ambavyo tayari vimefungwa mashine hizo, aliendelea kusisitiza kuwa zoezi hilo ni endelevu.

“Ni kazi endelevu, bado tunaendelea,  tutapata takwimu hizo baada ya zoezi ambalo linafanyika nchi nzima,” alisema Kayombo.

Kayombo alisisitiza kwakuwa mafuta yanasambazwa vituoni yakiwa yameshalipiwa, utaratibu wa mashine hizo una lengo la kukusanya kodi ya mapato inayotokana  na faida  baada ya kujumlisha mauzo yote na kutoa gharama za uendeshaji.

Kufuatia kufungwa kwa vituo hivyo, kwenye vituo vya mafuta ambavyo havikufungiwa, vilikuwa na misafara mirefu ya magari, pikipiki, bajaji na watu wenye vidumu wakitaka kununua nishati hiyo.

Tanga

Katika Jiji la Tanga, ambapo vituo 13 kati ya 15 vilivyomo jijini humo vilifungwa, Meneja wa TRA Mkoa wa Tanga, Swalehe Byarugaba, alisema wamiliki wa vituo vilivyofungwa wamepewa muda wa wiki mbili kuweka mashine hizo na kwamba baada ya muda huo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

“Hatua hii imetokana na serikali kuchoshwa na wafanyabiashara hawa

ambao licha ya kupewa muda wa kutosha, lakini hawakuonyesha nia ya kutekeleza agizo hilo,” alisema Byarugaba.

Akizungumzia hatua zinazoweza kushukuliwa kwa wafanyabiashara watakaokaidi hata baada ya kufungiwa, alisema ni pamoja na kupigwa faini kwa usheleweshaji wa ufungaji wa mashine hiyo.

Mwanza 72

Katika Mkoa wa Mwanza, ambapo vituo 72 vimefungwa, Meneja wa TRA Mkoa, Ernest Dundee, alisema: “Tumefanya kazi hiyo jana (juzi) ambapo kwa mkoa tumefunga  vituo 72, kwa sasa kuna vituo nane ambavyo vinaendelea kutoa huduma ya mafuta kutokana na kuwa vimekidhi matakwa ya kuwa na mashine hizo.

15 Dodoma

Mkoani Dodoma, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Christina Mndeme, akishirikina na Viongozi wa Mamlaka ya Mapato (TRA) Mkoa wa Dodoma, wamevifungia  vituo 15.

Akizungumza na Waandishi wa Habari jana mjini hapa, Meneja wa TRA Mkoa wa Dodoma, Thomas Masese, alisema wamevifungia vituo hivyo kutokana na  kutokuwa na mashine za kutolea risiti  zilizofungwa moja kwa moja kwenye pampu za kutolea mafuta.

Wamiliki Kanda ya Kati

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Waendesha Vituo vya Mafuta Tanzania (TAPSOA) Kanda ya Kati, Faustine Mwakalinga, alisema zoezi hilo linaweza kuleta madhara makubwa kwa ukuaji wa uchumi wa nchi.

Mwakalinga alisema vituo vingi vya mafuta, hasa vilivyoko wilayani havijafungwa mashine hizo.

Mwakalinga alisema haitakuwa jambo la kushangaza kuona mafuta yanaadimika na mengine kuuzwa kwa magendo kwa sababu wengi wa wamiliki wa vituo vya

mafuta hawana uwezo wa kufunga mashine hizo, kwa kuwa zinauzwa bei ghali.

“Nawaambia magari mengi, hasa yanayotoka wilayani yatakosa mafuta na hivyo kusababisha usafiri kwa wananchi kuwa mgumu na pengine kukosekana

kabisa kwa kuwa vituo vingi havijafungwa mashine hizo.’’

40 Arusha

Akizungumza na MTANZANIA kuhusu zoezi la ukusanyaji wa kodi na kufungwa kwa biashara zisizotumia mashine, Meneja wa TRA Mkoa wa Arusha, Apili Mbaruku, alisema mkoani wa Arusha vituo vilivyofungiwa ni 40.

Alisema katika Halmashauri ya Jiji la Arusha vituo 25 vimefungiwa, Wilaya ya Monduli 12, Karatu 11 na Wilaya ya Arumeru vituo vinne.

“Maagizo haya yalitolewa tangu mwaka jana kwa vituo vyote vya mafuta. Lakini wafanyabiashara hawa wamekaidi kufunga pampu kwenye mashine za kutolea mafuta. Kwetu sisi zoezi hili litaendelea kesho (leo) Wilaya ya Longido na Ngorongoro,” alisema Mbarouk.

MANYARA vitano

Akizungumzia zoezi hilo, Meneja wa TRA mkoani Manyara, Joseph Mtandika, aliliambia MTANZANIA jana kwamba tayari maofisa wake wamekwisha kuvifungia vituo vitano vya kuuzia mafuta katika Wilaya ya Babati.

Alisema TRA kuanzia leo wataanza ukaguzi katika vituo vyote vilivyopo wilayani ili kujiridhisha kwa wafanyabiashara waliokuwa wamenunua na hawakuzifunga mashine hizo.

“Tunatuma wakaguzi wilayani, wakikuta mfanyabiashara alinunua mashine siku nyingi lakini hakuwa ameifunga huyo atafungiwa kabisa kituo chake. Lakini kwa wale walionunua hivi karibuni na walikuwa bado hawajafunga, hao watasamehewa na kutakiwa kufunga haraka,” alisema Mtandika.

Kilimanjaro 34

Meneja wa TRA Mkoa wa Kilimanjaro, Philip Kimune, alisema kwa taarifa alizonazo katika mkoa wake vituo vilivyofungwa ni 34.

Alisema Moshi mjini vipo, 16, Hai 14 na Siha vitatu.

“Kwa sasa maofisa wangu bado wako kazini katika wilaya zote, naendelea kupokea taarifa kutoka kila upande ili niwe na idadi kamili ya vituo vyote kwa mkoa mzima wa Kilimnjaro,” alisema Kimune.

Ofisi ya Rwanda Air yafungwa

Katika hatua nyingine, TRA Mkoa wa Arusha imefunga ofisi za Shirika la Ndege la Rwanda kutokana na malimbikizo ya kodi ya tangu mwaka 2014.

Meneja Msaidizi wa TRA anayeshughulikia madeni, Irene Hance, alisema waliandika barua rasmi ya kuwataka walipe haraka malimbikizo ya kodi hizo kabla hatua nyingine za kisheria hazijachukuliwa dhidi yao.

“Tumewaandikia barua na kufanya vikao vya pamoja kuwakumbusha kulipa kodi hizo, lakini bila mafanikio yoyote. Tumetumia nguvu ya sheria kuwafungia ili kuwabana waje kulipia,” alisema Hance.

Kwa upande wake, Meneja Msaidizi Ukaguzi kutoka TRA mkoani hapa, Alex  Katundu, alisema idadi ya taasisi, viwanda na wafanyabiashara wakubwa wanaodaiwa malimbikizo ya kodi wanafikia zaidi ya 80, hivyo aliwataka wafanyabiashara kulipa kodi zao kwa wakati, ili kuepuka  usumbufu kwao na kwa wateja wao.

Mbali na Shirika la Ndege la Rwanda, TRA iliwafungia pia watoa huduma mbalimbali, vikiwamo vituo vya mafuta, hoteli, viwanda, karakana na watengeneza matofali wanaodaiwa kiasi cha Sh bilioni 10 wanazodaiwa kulimbikiza tangu mwaka 2014.

Habari hii imeandaliwa na Aziza Masoud, Dar es Salaam, Sussan Uhinga, Tanga, Fredrick Katulanda-Mwanza, Abraham Gwandu na Eliya Mbonea-Arusha na Ramadhan Hassan – Dodoma

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles