MZANZIBARI AHUKUMIWA JELA UINGEREZA KWA KUDANGANYA AMEKUFA

0
507

Na WAANDISHI WETU

MAMA mmoja mwenye asili ya Zanzibar mapema wiki hii amehukumiwa kifungo cha miaka miwili na nusu jela kwa kosa la kudanganya kuwa amekufa, ili aweze kujipatia pauni 140,000 za Uingereza kutoka shirika la bima la nchi hiyo.

Kiasi hicho cha fedha ni sawa na Sh 405,749,400 za Tanzania iwapo kitabadilishwa kwa sasa, ambapo pauni moja ni sawa na Sh 2,800 za Tanzania.

Mama huyo, aitwaye Arafa Nassib, mwenye umri wa miaka 48, anatuhumiwa kupanga njama hizo akishirikiana na mtoto wake wa kiume, Adil Kasim, mwenye miaka 18 na mtu mwingine wa tatu aliyetajwa kwa jina la Yusuf Abdullah, mwenye umri wa miaka 24.

Daily Mail limeandika kuwa, mama huyo alikuwa na madeni makubwa yaliyotokana na kukopa samani za gharama kutoka katika makampuni ya BrightHouse na PerfectHome.

Inaelezwa, samani hizo alizoziweka kwenye ghorofa alilopanga huko Walsall, West Midlands, alishindwa kulipa na hivyo kuamua kushirikiana na mtoto wake huyo, Kasim, kudai kuwa aliuawa kwa ajali ya barabarani wakati akiwa amekwenda Zanzibar, ili kijana wake huyo aweze kuidhinishiwa malipo ya bima ya maisha ya pauni 140,000.

Inaelezwa fedha hizo ziliombwa na Kasim katika Mamlaka ya Wajane (Scottish Widows) kati ya Machi na Desemba, mwaka jana.

Nassib, Kasim na Abdullah walikuwa nje kwa dhamana hadi Julai 12, wiki hii, siku iliyotolewa hukumu.

Kwa mujibu wa taarifa zilizoripotiwa na Daily Mail, mama huyo pamoja na mtoto wake mashtaka yao yalifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Birmingham Aprili, mwaka huu, baada ya kufanyika uchunguzi dhidi madai ya kifo chake.

Taarifa zinaeleza kuwa, mama huyo na mtoto wake, Kasim na Abdullah, wote ni wakazi wa kitongoji chenye viwanda cha Walsall, kilichoko katika mji wa West Midlands, nchini Uingereza.

Kitongoji cha Walsall kipo umbali wa maili nane kaskazini magharibi mwa jiji la Birmingham na maili sita mashariki mwa jiji la Wolverhampton.

Katika taarifa ya kuthibitisha mashtaka hayo, Jeshi la Polisi nchini Uingereza lilisema mama huyo alikamatwa Februari, wakati akirejea nchini Uingereza, akitokea nchini Canada alikokuwa amekwenda kwa siri.

Kesi hiyo ilikuwa inapelelezwa na Kitengo cha Bima cha Jeshi la Polisi cha jijini London, ambacho kilifanya uchunguzi mapema Novemba, mwaka jana na kubaini kuwa Arafa hakufariki dunia kama ilivyodanganywa mamlaka ya bima.

MTANZANIA Jumamosi lilimtafuta baba mdogo aliyemlea Arafa aitwaye Haji Nassib, ambaye anaishi visiwani Zanzibar na kukiri kuwa hata yeye amezisikia taarifa hizo.

Haji aliliambia MTANZANIA Jumamosi kuwa, alitumiwa taarifa hizo kupitia mtandao wa WhatsApp, ingawa hajapata taarifa rasmi.

“Sina taarifa zozote rasmi zaidi ya kupata habari kwenye WhatsApp kuwa tayari wamehukumiwa, huku nyumbani hawajui na hawajui alidanganya vipi, huku Zanzibar wanajua yupo hai,” alisema Haji.

Anasema kabla ya hukumu hiyo alisikia Polisi kutoka nchini Uingereza walifika Zanzibar kuchunguza tuhuma hizo.

Ingawa Haji anasema hajui Polisi hao wa Uingereza walifika lini, lakini anasisitiza kuwa hawakufika nyumbani kwake.

Haji alisema wao kama familia bado hawana taarifa rasmi na kwamba wakizipata watajua nini wafanye.

“Hatuna taarifa rasmi na sijui nini cha kufanya, huyo Arafa ana watoto wawili, mmoja ndio huyo aliyekamatwa naye…pia ana dada yake ambaye anaishi huko huko Uingereza na sijapata taarifa kutoka kwa hao wote,” alisema Haji.

Akimwelezea Arafa, baba yake mdogo huyo alisema aliondoka Zanzibar miaka ya 90 na kuhamia Uingereza.

Alisema hafahamu kama Arafa ana uraia wa kudumu nchini humo.

Akitoa hukumu dhidi ya Arafa, Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Birmingham, William Edis, alisema; “Ulikuwa ni mwanzo wa kumaliza uongo mwingi mwingi”.

Alilielezea tukio hilo kama ni mpango uliopangwa kisasa, kwa uangalifu ambao umekaribia kufanya kazi.

“Ikiwa Tanzania haijawa katika orodha ya nchi hatari kwa udanganyifu wa bima, ni busara kuchukua hatua,” alisema hakimu huyo na kuongeza;

“Uaminifu katika mchakato wa madai ya bima ni muhimu, labda mfumo wote wa bima upo hatarini”.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here