25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Membe: Nikikatwa jina CCM nitakuwa wa Mwandosya

????????NA WAANDISHI WETU
WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, amesema endapo Kamati Kuu ya CCM haitalipitisha jina lake kuwania urais mwaka huu, kura yake ataipeleka kwa kada wa chama hicho, Profesa Mark Mwandosya.
Amesema atafikia uamuzi huo kwa kile alichodai kuwa yeye na Profesa Mwandosya ndio wanakidhi vigezo 13 vilivyowekwa na CCM kumpata mgombea urais.
Kauli hiyo aliitoa jana mjini Mbeya, alipokuwa akitafuta wadhamini, ambapo alisema Profesa Mwandosya amebahatika kuwa na sifa zote za kiuongozi.
“Sina wasiwasi na mtu huyu, hata kama chama kikiliondoa jina langu, basi kura yangu naipeleka kwake kwani yeye ndiye mwanamume aliyekidhi vigezo vyote vilivyopitishwa na kuhalalishwa na chama,” alisema Membe huku akishangiliwa.
Aliwataka wakazi wa Mkoa wa Mbeya kuhakikisha wanayapitisha majina mawili ya wagombea wa nafasi za urais – jina lake na la Profesa Mwondosya.
Hata hivyo, Membe alionyesha kushangazwa na tabia za baadhi ya watangaza nia kuwa na uchu wa madaraka kwa kutaka nafasi zote mbili za urais na ubunge, hivyo kuwataka wananchi kuwakataa mapema kabla jogoo halijawika.

Dk. Kitine kushughulika na PhD ‘feki’

MKURUGENZI Mkuu wa zamani wa Idara ya Usalama wa Taifa (TIS) na Waziri wa kwanza wa Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Dk. Hassy Kitine, ametangaza nia ya kugombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Katika mkutano wake uliofanyika mjini hapa, Dk. Kitine alisema Serikali yake ya awamu ya tano itakuja na sheria kali ya kuwashughulikia watumishi wa umma, mawaziri na watu wengine wenye shahada ‘feki’ ya Uzamivu (PhD), ambao wanaligharimu taifa kutokana na kufanya udanganyifu katika elimu.
Alisema iwapo atateuliwa na chama chake na kisha Watanzania kumpa ridhaa ya kuongoza nchi, atahakikisha wanaotumia PhD feki, wanafungwa jela miaka mitano.
Dk. Kitine aliyechukua muda mwingi kuelezea uzoefu wake alipokuwa Ikulu kama Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa pamoja na mahusiano yake na marais waliopita, alisema imemchukua muda mwingi kutafakari na kufanya uamuzi huo, hasa kutokana na udhaifu wa makada wenzake waliojitokeza kutangaza nia na kuchukua fomu.
“Nimechukua uamuzi huu kwa sababu nimewapima na kuwaona wagombea wengine waliotangaza nia ya kugombea urais ndani ya CCM hawafai na wanahangaika tu. Najua siwezi kuwa kama Baba wa Taifa (Mwalimu Julius Nyerere), lakini nitajitahidi sana kuongoza kama yeye… Mimi ndiye mgombea pekee ambaye napafahamu Ikulu kuliko wagombea wote; siyo mahali pa kukimbilia, kuna matatizo mengi sana,” alisema.
Dk. Kitine aliyewahi kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), katika Serikali ya awamu ya tatu ya Rais Benjamini Mkapa, amekosoa harakati za makada wenzake wa CCM waliotangaza kugombea urais, akieleza hofu yake kuwa hawaonyeshi kuwa na ajenda ya dhati ya kutaka kuutumikia umma wa Watanzania.
Alisema kutokana na miiko ya uongozi aliyojifunza na kurithi kutoka kwa Mwalimu Nyerere, rais ajaye ni lazima awe na uwezo wa kutazama na kuamua kuhusu usalama na mipaka ya nchi, awe mwadilifu, awe na sauti na uwezo wa kuendeleza kilimo kwa ajili ya maisha ya Watanzania.
“Tatizo la uadilifu ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na hata nchi yetu bado ni tatizo kubwa sana. Ni afadhali zimwi lenye uzoefu kuliko zimwi lisilojua kuongoza. Watanzania siku hizi hawapendani, zaidi ya kupenda pesa; nawaambia Watanzania wenzangu (wana CCM), wagombea wengine wanamwaga hela, wakija chukueni, msiwape kura,” alionya Dk. Kitine

January asema hajamuhujumu Rais Kikwete

KADA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), January Makamba, jana amechukua fomu ya kuomba kuteuliwa na chake kuwania urais huku akisema hajamuhujumu Rais Jakaya Kikwete.
January ambaye ni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, alikabidhiwa fomu hiyo na Katibu wa Idara ya Oganaizesheni ya NEC, Mohammed Seif Khatib, baada ya kuwasili katika Ofisi za CCM Makao Makuu mjini Dodoma.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukabidhiwa fomu, January alisema nafasi yake serikalini ana mipaka ya kufanya kazi na mipaka ya kutoa ushauri katika mambo mbalimbali ya kiutendaji.
“Si sahihi kusema nilimfanyia Rais Kikwete hujuma kutokana na hotuba yangu niliyoitoa Dar es Salaam wiki iliyopita kusheheni mambo mengi mazuri, na kwanini siku zote nilikaa nayo tu mambo hayo na sikumshauri ayafanyie kazi,” alisema na kuongeza:
“Tafsiri ya kusema hivyo ni hujuma si sahihi hata kidogo kwa sababu kwa nafasi yangu serikalini nina mipaka ya kufanya kazi na kutoa ushauri.
“Kwahiyo ndiyo maana dhamira yangu imenisukuma kuomba nafasi ya juu ya uongozi katika nchi ili niweze kufanya mambo makubwa.”
Alisema amejitosa kuwania nafasi hiyo ili kushinda na si kujiandaa kugombea katika awamu nyingine.
January alisindikizwa na mkewe Ramona, baba yake Mzee Yusuf Makamba na mama yake Josephine Makamba, wasanii wa muziki wa kizazi kipya wakiongozwa na Mwana Fa na Fid Q, wanafunzi wa vyuo vikuu vya UDOM, CBE, St. John, Mipango, viongozi wa dini na wanachama wa CCM.
“Nimeingia kwa dhamira moja tu ya kushinda na kuleta mabadiliko, sijaingia kujaribu au kujipanga kwa miaka ijayo kwa sababu uwezo na maarifa ninayo, kwa hiyo nitawashawishi wana CCM wenzangu.

Lowassa aivuruga ngome ya Dk. Kamani

WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, jana ameingia mkoani Simiyu na kupokewa na umati mkubwa wa wana CCM wakiongozwa na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge.
Akiwa katika Jimbo la Busega linaloshikiliwa na Waziri wa Mifugo, Dk. Titus Kamani, Lowassa alifanya mkutano wa ndani na kupata wanachama 390 waliomdhamini.
Dk. Kamani ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu ameshachukua fomu na kutangaza nia ya kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano.
Hata hivyo, ilielezwa kuwa Dk. Kamani bado hajafika katika mkoa huo kutafuta udhamini.
Akiwa katika mji mdogo wa Ramadi wilayani Busega, Lowassa aliwashukuru wanachama waliomdhamini na kuwataka wajiandikishe ili wampigie kura atakapopitishwa na chama kuwa mgombea urais.
“Nawashukuru wale wote walionidhamini. Lakini naomba mjiandikishe katika daftari la wapigakura. Kuna watu fulani walitaka kumpeleka mtu wao kuwa rais mwaka fulani. Lakini walichofanya ni kumsukuma na gari huyo mtu wao. Lakini kumbe gari halimfikishi mtu Ikulu, bali kinachomfikisha ni kura,” alisema.
Lowassa pia aliwasalimia wananchi waliokuwa wamekusanyika katika uwanja wa michezo katika mji huo. Hata hivyo Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara aliwaeleza wananchi hao kuwa kanuni za chama hazimruhusu Lowassa kuhutubia.
Alipowasili wilayani Bariadi, Lowassa alitia saini katika kitabu cha wageni cha ofisi ya CCM Mkoa wa Simiyu na baadae kuelekea kwenye ofisi za wilaya alikofanya mkutano na kupokea wanachama waliomdhamini.
Akitangaza idadi ya wanachama waliomdhamini, Katibu wa CCM Wilaya ya Bariadi, Michael Conya, alisema ni 4,863 ambao wametoka katika wilaya za Bariadi, Meatu, Itilima, Maswa na Busega.
“Wanachama waliomdhamini ni 3,203 kutoka Bariadi, Itilima 478, Meatu 636, Maswa 156 na Busega 390, jumla ni wanachama 4,863,” alisema Chonya.
Akiwashukuru wanachama hao kwa kumdhamini, Lowasssa alisema sababu kubwa iliyomfanya kugombea ni kuchukia umasikini.
“Haturuhusiwi kusema, lakini mtaji wa wanasiasa ni watu. Kwanini nagombea? Nataka kugombea urais kwa sababu nimechoka kusikia umasikini. Mwaka 1972, Mwalimu Nyerere alitangaza maadui watatu; yaani ujinga, umasikini na maradhi, lakini hadi leo wapo,” alisema Lowassa na kuongeza:
“Ikimpendeza Mungu huko juu, nitaendesha mchakamchaka wa maendeleo. Nimechoka kusikia umasikini. Maji tuliyoanza kuvuta kutoka Ziwa Victoria hadi leo hayajafika, kwanini? Hayo ndiyo ninayotaka kuyapigania.”
Akizungumza awali, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Jimbo la Busega, Dk. Rafael Chegeni, alimtambulisha Mbunge wa Bariadi Magharibi, Chenge kuwa ni ‘Nyoka wa makengeza’.
“Tolenayo Nzoka ihenge’,” alisema kwa lugha ya Kisukuma akimaanisha; ‘Tunaye hapa Nyoka wa Makengeza’.
Naye Chenge alipokaribishwa aliwashukuru wana CCM kwa kujitokeza kwa wingi, huku akisema Lowassa ndiye anayefaa kuwa rais.
“Nawashukuru wana CCM kwa kujitokeza kwa wingi kumdhamini Lowassa. Huyu ni mwana CCM mwenzetu aliyeonyesha nia ya kugombea urais. Ikimpendeza Mungu na sisi tunapendekeza hivyo na tunaamini yeye ndiye anafaa kwa kipindi hiki,” alisema Chenge.
Akimzungumzia Lowassa, mwenyekiti mstaafu wa CCM wilayani humo, Charles Nkenyenge, alisema anamfahamu tangu alipofanya kazi naye mwaka 1978.
“Tunataka kumdhamini mtu tunayemfahamu na akichukua nchi itasonga mbele. Wakati nikiwa Mwenyekiti wa CCM Bariadi na mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa, Lowassa alikuwa Katibu Msaidizi wa CCM Mkoa wa Shinyanga,” alisema.
Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Bariadi, Juliana Mahongo, alisema anamkumbuka Lowassa kwa kuwa alifanya kazi na mumewe katika usuluhishi wa migogoro ya wafugaji.

Chikawe: Nitaendeleza vita dhidi ya maadui watatu

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe, jana alichukua fomu ya kuomba kuteuliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kugombea urais katika uchaguzi wa Oktoba mwaka huu.
Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa fomu mjini Dodoma, Chikawe alisema iwapo atafanikiwa kushinda, Serikali yake ya awamu ya tano itaendeleza misingi iliyowekwa na watangulizi wake ikiwa ni pamoja na kupambana na maadui watatu.
“Tangu tumepata uhuru Chama Cha Mapinduzi kimejitahidi kukabiliana na maadui watatu wa taifa letu ambao ni ujinga, maradhi na umasikini. Hivi sasa tunae adui mwingine mbaya zaidi anaitwa rushwa.
“Adui huyu pamoja na mambo mengine anadhoofisha sana jitihada za kupigana na maadui watatu wa kwanza. Hata hivyo, misingi ya mapambano dhidi ya maadui hawa imewekwa na marais wetu katika awamu nne zilizotangulia.
“Misingi hiyo itaendelea kuimarishwa, kuboreshwa na kuwekewa mikakati mipya inayoendana na changamoto za sasa ili kuendeleza kupambana vikali dhidi ya maadui hawa wakubwa,” alisema.
Alipoulizwa kuhusu vitendo vya ugaidi ambavyo ni tishio kwa amani ya taifa, Chikawe alikiri kuwapo kwa vitendo hivyo, lakini akasema vilikoma tangu alipoingia katika wizara hiyo.
“Ni kweli hapa nyuma vitendo hivi vilikuwa gumzo kila siku, watu kumwagiwa tindikali huko Zanzibar, mabomu kule Arusha, lakini tangu nimeingia vitendo hivi vimefutika kimya kimya.
“Taarifa zake zipo na dawa yake ipo, jambo lolote haliwezi kuisha hivi hivi tu, kuna kazi iliyofanyika, sasa kueleza nini kimefanyika itakuwa ni kuweka wazi siri za nchi,” alisema.
Alipoulizwa kuhusu vipaumbele vyake iwapo atapata nafasi hiyo, Chikawe alisema hana kipaumbele chake na kwamba vipaumbele vyake ni ilani ya chama chake.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles