23.3 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 8, 2024

Contact us: [email protected]

MBARAWA ASHITUKIA MCHEZO MCHAFU JNIA

 

Na LEONARD MANG’OHA-DAR ES SALAAM

WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, amenusa harufu ya rushwa miongoni mwa watumishi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam, hali inayoikosesha Serikali mapato.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Profesa Mbarawa alisema baadhi ya wafanyabiashara uwanjani hapo wamekuwa wakitoa rushwa kwa baadhi ya watumishi wasio waaminifu ili kusogeza mbele muda wa kulipia kodi ya pango.

“Baadhi yenu mlikuwa mnakwenda kwa mtu fulani mnampa pesa kidogo apeleke deni lako mbele, mwingine anaona kulipa kodi ni ngumu anatoa dola 1,000 ili asogezewe mbele muda wa kulipa.

“Kama ni TAA mnafanya hivyo msiwadanganye hawa kuwa akikupa hiki utamsaidia, niwaeleze wazi hiyo haitakusaidia, atachukua hiyo hela yako na bado utalipa hela yangu, ukifanya hivyo utakuwa umepoteza hiyo hela yako bure, ni bora ukalipe,” alisema Profesa Mbarawa.

Alisema inaonesha wazi kuwa kulikuwa na ukwepaji mkubwa wa kodi, kwani katika kipindi cha kuanzia Machi mwaka huu baada ya kufanya mabadiliko wameweza kukusanya Sh bilioni nane.

Aliongeza kuwa, ikiwa kutakuwa na usimamizi mzuri wa ukusanyaji kodi katika viwanja vya Dar es Salaam, Mwanza, Kilimanjaro na Arusha, Serikali ingeweza kupata zaidi ya Sh bilioni 150 kwa mwaka.

Profesa Mbarawa aliwataka wale wanaodaiwa kuhakikisha wanalipa madeni yao kabla ya mwisho wa mwezi Septemba, mwaka huu na atakayeshindwa kufanya hivyo afungashe vitu vyake aondoke mwenyewe kabla ya kuchukuliwa hatua.

“Madhumuni ya kuwaita hapa ni kusikia maoni yenu kuhusu changamoto zinazowakabili katika kufanya biashara hapa, ila kila mmoja akumbuke mwishoni mwa Septemba awe amelipa.

“Nataka hela yangu, hii ni hela ya Serikali, kulipa kodi ni wajibu wa kila mmoja, tunataka hela kujenga viwanja, kuboresha huduma na kulipa wananchi fidia,” alisema Mbarawa.

Alisema Serikali itapitia mikataba yote ya wapangaji wao ili kuhakikisha wanafanya biashara inayonufaisha pande zote mbili, kwani kumekuwapo na baadhi ya wafanyabiashara ambao wanatumia mikataba iliyosainiwa zaidi ya miaka 25 iliyopita.

“Kila biashara tutaifanya kwa ushindani, tutakupa bei zetu tunazotaka ulipe nawe utatupatia yako na tutakupa nafasi uzunguze ni kwa nini unataka bei hiyo, kama utashindwa tutakupa notisi na kuitangaza kwa watu wengine, wako waliofanya hili ni shamba la bibi, sasa ‘enough is enough’.

“Hatutakupa bei ya kukufukuza, lakini nasi hutatupa bei ukatajirika sisi tusipate kitu, hilo halitawezekana,” alisema.

Kuhusu utaratibu wa wafanyabiashara hao kuhamia katika jengo jipya la uwanja huo (terminal III), Mbarawa alisema mchakato wake utatangazwa na utakuwa wa wazi kwa yeyote akakayehitaji.

Aliongeza kuwa, wafanyabiashara hao watapewa kipaumbele, lakini ulipaji wao wa kodi za sasa utakuwa moja ya vigezo vya mtu kupewa.

“Wasipofanya vizuri hapa wasijaribu kabisa kuomba kule, nitawashangaa watakaopitisha jina la mtu anayefanya vibaya hapa,” aliongeza Profesa Mbarawa.

Baadhi ya wafanyabiashara hao walitaka kutatuliwa kwa changamoto mbalimbali uwanjani hapo, ikiwa ni pamoja na kuboreshwa kwa mfumo wa uhakiki wa Idara ya Uhamiaji, ili kupunguza muda wa abiria wa kigeni kukaa uwanjani hapo baada ya kuwasili nchini.

Mengine ni kupunguzwa kwa utitiri wa kodi ambazo walidai kusababishwa kuongezwa kwa bei ya tiketi, kutolewa kwa huduma zinazoendana na thamani ya fedha wanazolipa.

Mmoja wa wafanyabiashara hao mwenye asili ya Asia, ambaye jina lake halikupatikana mara moja, alimtaka waziri kushughulikia urasimu uliopo uwanjani hapo, ambapo baadhi ya maofisa wa serikali wamekuwa wakikataa kupokea fedha za Tanzania na kutaka malipo yafanyike kwa dola ya Marekani.

“Natamani kuona kila siku ukija hapa, hata leo nilikuwa nikizungumza na mfanyabiashara mwenzangu hapa, nashangaa leo nimekwenda chooni nimekuta kuna maji, nadhani ni kwa sababu wewe upo hapa, kabla ya leo hakukuwa na maji.

“Wanataka uache passpoti uende nje ukabadili fedha upate dola bila kusindikizwa, wanakulindaje na wahalifu kama Al shabaab na wakati wewe hujaruhusiwa kuishi hapa,” alisema mfanyabiashara huyo.

Akijibu hoja hizo, Profesa Mbarawa alieleza kusikitishwa kusikia maji yanakosekana uwanjani hapo.

“Sitaki kuzungumzia hapa suala la utawala tutalizunguza kwenye vikao vyetu, pia nimesikia watoa huduma Uhamiaji wachache, niwahakikishie tutaongeza maofisa ili kupunguza muda wa kusubiri huduma,” alijibu Profesa Mbarawa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles