23.4 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

MATUMIZI YA TEHAMA IWE CHACHU YA MABADILIKO


NA ASHA BANI

Kutokana na kukua kwa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), mashirika na taasisi mbalimbali yameweza kupiga hatua na kujipambanua kiuchumi ili kuongeza mchango mkubwa kwa Serikali.

Shirika la Posta nchini limekuwa katika hatua ya kuendelea kukua kutokana na matumizi hayo ya Tehama na hata kujipambanua mijini na vijijini katika kutoa huduma zake.

Hivi karibuni Posta Masta Mkuu wa shirika hilo, Fortunatus Kapinga, alielezea umuhimu wa Tehama katika kuhakikisha shirika linapiga hatua zaidi na kuwa na mchango mkubwa serikalini.

Kapinga alielezea mikakati ya shirika hilo ikiwa ni pamoja  na kuanzisha biashara mtandaoni, kuwa na mchakato wa kumiliki ndege binafsi, kuunganisha ofisi 125 za posta kwenye mfumo wa kutolea huduma kielektroniki unaojulikana kama Postglobal nersmart.

Naamini kutokana na mafanikio ya huduma hizo, Watanzania wanaotaka kuuza bidhaa mbalimbali kupitia biashara mtandao na hata maduka ya Shirika la Posta wataweza kunufaika na huduma hizo.

Pia kwa mujibu wa Kapinga maduka ya posta yatatumika kwa wafanyabiashara mbalimbali ikiwemo pamoja na uuzaji wa vitenge, viatu, vitu vya asili na vinginevyo hiyo itasaidia kuongeza pato katika shirika.

Na Waswahili wanasema kupenda bidhaa za nyumbani kwanza kutasaidia kukuza uchumi wa hapa nyumbani na kufanya nchi kupiga hatua, huku kuendelea kwa taasisi kuboresha biashara zake na kujitegemea wenyewe.

Shirika la Posta limeonyesha kupiga hatua kubwa hasa katika kuongeza matumizi ya teknolojia na kutokana na hali hiyo kwa sasa pia  wanatarajia kutumia ndege zisizo na rubani katika eneo la Ziwa Victoria kwa ajili ya kusafirisha vifurushi mbalimbali na kutumia mtandao kuangalia vifurushi vimekwamia wapi na kufikia wapi wakati vikiwa vinasafirishwa kwa mteja.

Hata hivyo, huduma za shirika hilo pia zimeendelea kujipambanua na kuzifanya kuenea mpaka vijijini hivyo kuwapa nguvu zaidi ya kufungua na matawi katika kata.

Hakuna ubishi ufunguaji wa matawi katika kata utasaidia wananchi kupata huduma zao mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupokea vifurushi, vyeti vya vizazi na vifo, vitambulisho vya taifa pasipo kwenda makao makuu ya huduma hizo ambazo hapo awali ilionekana kuwapa shida zaidi.

Mafanikio hayo pia yameonekana pale ambapo shirika limefanikiwa kujitanua kwa kuboresha huduma za kisasa, wakiwa kwenye maandalizi ya kutoa huduma hizo kwa njia za kisasa katika ukanda wa Afrika kwenye kufikisha huduma zao kwa wateja.

Wateja wote katika maeneo ambayo yalielezwa kuwa korofi wataendelea kutumia ndege zisizo za dereva ziitwazo ‘drones’.

Shirika pia limezalisha faida na kuweza kutoa gawiwo la shilingi 250,000,000 kwa Serikali ikiwa ni hatua nzuri na kwa mara ya kwanza.

Kwa watumiaji wa mashirika mbalimbali kumekuwa na malalamiko ya hapa na pale ya wateja kuibiwa mali zao au kupotea Shirika la Posta linaendelea kuimarisha usalama wa mali na fedha za wateja kwa kufunga kamera za kiusalama yaani kuingia katika mfumo wa CCTV.

Hiyo ni hatua sahihi na ambayo itaungwa mkono na kila mmoja wetu kwa kuwa hakuna mtu atakayependa kutumia shirika katika kusafirisha kifurushi au mzigo wake ukaishia hewani kwa kuibiwa au kupotea.

Hili ni jambo jema kwa kulipongeza shirika hata katika kufunga scanner ambayo inahakikisha usalama wakati wa kutoa huduma zao.

Hivi karibuni Shirika la Posta nchini pia lilihudhuria mkutano wa dharura wa umoja wa posta duniani uliofanyika nchini Ethiopia.

Masuala yaliyojadiliwa wakati wa mkutano huo ni pamoja na mpango wa huduma jumuishi wa ulipanaji ambayo inafanywa ili kuweka mazingira ya barua, vifurushi na EMS kuweza kulipana kikamilifu kwa mfumo unaoweza kukidhi gharama za utoaji huduma hizo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles