23.6 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

Marekani, Iran zavimbiana Sakata la Saudi Arabia

TEHRAN, IRAN

IRAN imesema ipo tayari kuangamiza nchi yeyote ambayo itaanzisha mashambulizi dhidi yake, Ofisa wa juu wa Jeshi amesema.

Kamanda wa Jeshi la kimapinduzi la Iran, Meja Jenerali Hossein Salami ameionya Marekani na washirika wake kuwa makini na kutofanya kosa lolote.

Kauli yake hiyo imekuja muda mfupi baada ya Marekani kutangaza kupeleka vikosi vya jeshi nchini Saudi Arabia ambayo hivi karibuni vituo vyake vya mafuta vilishambuliwa na ndege zisizo na rubani.

Marekani imeishutumu moja kwa moja Iran na zaidi ikidai kuwa na ushahidi  kwa kuhusika na shambulio hilo ambalo tayari limetikisa bei ya mafuta duniani.

Waziri wa Ulinzi wa Marekani,  Mark Esper akizungumza na waandishi wa habari nchini humo alisema wanajeshi hao wataelekea katika taifa hilo ili kuimarisha ulinzi .

Hata hivyo waziri huyo hakutaja  idadi yao na bado haijajulikana.

Waasi wa Houthi nchini Yemen wanaoungwa mkono na Iran wamesema kwamba walihusika na mashambulizi ya visima viwili vya mafuta wiki iliopita.

Lakini Saudi Arabia na Marekani zimelaumu Iran kwa mashambulizi hayo.

Ijumaa Rais wa Marekani Donald Trump alitangaza vikwazo vipya dhidi ya Iran huku akisema kwamba alipendelea kuzuia mgogoro wa kijeshi.

Vikwazo hivyo vipya ambavyo Rais Trump alivitaja kuwa vya kiwango cha juu vitalenga benki ya Iran na mali yake iliopo ugenini.

”Nadhani kujizuia ni muhimu” , aliiambia ofisi ya White House.

Jana Meja Jenerali Hossein Salami akijibu hatua hiyo ya Marekani kupitia runinga ya taifa alisema; ”Tahadharini ”, aliongeza ; ”Tuko tayari kumuadhibu mtu na tutaendelea hadi kuwaangamiza wachokozi,”.

Kwa mujibu wa Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Esper, Saudi Arabia ndiyo iliyoiomba Marekani msaada huo.

Alisema  vikosi vya Marekani vitajielekeza kupiga jeki wanajeshi wake wa angani mbali na kujilinda dhidi ya silaha za angani na kwamba itapeleka silaha kwa nchi zote mbili.

Mwenyekiti wa wanajeshi wa nchini Marekani, Jenerali Joseph Dunford aliunga mkono upelekeji wa wanajeshi hao akidai kwamba hatasema idadi yao.

Dunford hakutoa maelezo zaidi kuhusu aina ya vikosi hivyo vitakavyotumwa.

KILICHOTOKEA SAUDIA

Mashambulio yalilenga visima vya mafuta vya Abqaiq na kile cha Khurais nchini Saudi Arabia wiki moja iliyopita na kuathiri usambazaji wa mafuta duniani.

Jumatano, Wizara ya Ulinzi ya Saudi Arabia ilionyesha mabaki ya ndege zisizo na rubani na silaha ikithibitisha kwamba Iran ndiyo iliyohusika.

”Taifa hilo lilikuwa linafanya uchunguzi kujua ni wapi mashambulio hayo yalitekelezwa,” alisema msemaji wake.

Kabla ya kauli hiyo ya Saudi Arabia maofisa waandamizi wa Marekani waliviambia vyombo vya habari kwamba wana ushahidi kwamba mshambulizi hayo yalitekelezwa kusini mwa Iran.

Iran imekana kuhusika katika mashambulio hayo , huku rais Hassan Rouhani akiyataja kuwa kisasi cha raia wa Yemen.

Marekani haiamini kama waathiriwa wa vita vya Yemen vya miaka minne na nusu wanaweza kutekeleza mashambulio kama hayo.

Jumatano waziri wa masuala ya kigeni nchini Marekani aliyataja mashambulio hayo kama kitendo cha vita.

Wakati huohuo kampuni ya mafuta ya Saudia , Aramco imesema k inatarajia kiwango cha mafuta kurudi kufikia kiwango cha kabla ya shambulio la mwezi huu.

Kwa sasa Marekani anaonekana kuwa mshirika wa Saudi Arabia wa kimkakati  na imejitolea kuziba mwanya wowote.

Meli ya kijeshi ya Marekani ‘The Destroyer’ imeegeshwa kaskazini mwa Ghuba ili kuzuia makombora yanayotoka upande huo.

Vifaa zaidi ya kujilinda vinatumwa kote Saudia na nchi za falme za kiarabu kutokana na hali ya wasiwasi na jirani yao Iran.

Lakini kuwepo kwa kambi za vikosi vya Marekani Saudia kulizua utata katka siku za nyuma.

Licha ya kwamba vilialikwa na mfalme wa Saudia, uwepo wao ulitumika na Osama bin Laden kuwavutia wapiganaji wa kijihadi kupinga kile alichokitaja kuwa uvamizi wa rasi ya Uarabuni.

CHANZO

Waasi wa Houthi mara kwa mara wamerusha makombora na ndege zisizo na rubani katika maeneo yanayokaliwa na raia nchini Saudia.

Wanapigana dhidi ya vikosi vya muungano wa Saudia ambavyo vinamuunga mkono rais ambaye waasi hao walimtimua wakati mgogoro huo wa Yemen ulipokoma.

Iran ndio mpinzani wa Saudia na ndio mpinzani mkuu wa Marekani ambayo iijiondoa katika makubaliano ya kinyuklia ya Iran baada ya Trump kuchukua mamlaka.

Wasiwasi kati ya Marekani na Iran umeongezeka zaidi mwaka huu.

Marekani iliituhumu Iran kwa kuhusika na mashambulio ya meli mbili za mafuta katika Ghuba mwezi Juni na Julai , pamoja na meli nyingine nne mwezi Mei.

Iran inapinga madai hayo yote ikidai kuwa Marekani imeamua kuichokoza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles