25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Maisha ya Marita Lorenz na Fidel Castro

NA MARKUS MPANGALA            |             


NINAANZA kusimulia maudhui ya kitabu cha maisha ya Marita Lorenz cha “The Spy Who Loved Castro: How I was recruited by CIA to kill Fidel Castro.” Kitabu hiki kimeandikwa kwa lugha ya Kingereza (tafsiri hii si rasmi, pia nitaelezea matukio muhimu ambayo yanakupa picha kamili).

Baadhi ya simulizi nitaiweka kwenye mfumo wa majibizano (kufupisha) ili kumfanya msomaji aelewe kwa haraka kilichomo kitabuni pamoja na kufaidika mafunzo yaliyojaa humu, ambayo ni visa, mikasa na mapambano ya maisha ya kila siku.

Aidha, kitabu hicho kilichapishwa kwa mara ya kwanza mwaka 2017 na Kampuni ya Penguin pamoja kupewa nambari 9781785034534. Awali kitabu hicho kiliandikwa kwa lugha ya Kihispania kabla ya baadaye kutafsiriwa kwa lugha ya Kingereza na Maria White.

Kitabu hiki kimebeba habari za maisha halisi ya Marita Lorenz ambaye alitumika kama jasusi wa Shirika ya kijasusi la CIA (Central Intelligency Agency), Shirika la Upelelezi wa ndani FBI, Ofisa wa Polisi na wakati mwingine kama nesi aliyetakiwa kufanya hujuma ama upelelezi.

Maisha ya Marita Lorenz yanawahusu moja kwa moja Rais wa zamani wa Cuba, Fidel Castro, Rais wa Venezuela, Marcos Perez Jiminez na kuzigonganisha nchi za Cuba, Marekani, Hispania, Venezuela, Angola, Peru na Ujerumani.

Ilona Marita Lorenz alizaliwa nchini Ujerumani mwaka 1939 katika kambi ya Bergen-Belsen kwa baba Mjerumani na mama raia wa Marekani.

Katika kipindi cha usichana wake alisafiri huku na kule akiwa na baba yake ambaye alikuwa ni baharia. Mwaka 1959 Marita alikutana kwa mara ya kwanza na Fidel Castro.

Katika maisha yake alifanikiwa kuzaa watoto  na marais wawili, Fidel Castro (mmoja) na Marcos Perez Jiminez (mmoja), na kushuhudia njama za mauaji ya aliyekuwa Rais wa Marekani, John F. Kennedy pamoja na kuwa mwanamke aliyejihusisha na magenge ya wauzaji wa dawa za kulevya na uhalifu, Mafia.

Marita alitumia miaka 22 kuonana na mtoto wake wa kwanza kutokana na Rais wa Cuba, Fidel Castro kukataa katakata kuwakutanisha, na mazingira ya kuzaa ya kuzaliwa mtoto mwenyewe yalikuwa yenye kila dalili za hujuma dhidi ya mimba ya Marita Lorenz.

Pili, Marita alitelekezwa msituni akiwa na mtoto mwingine (mimba ya pili) ya Rais Marcoz Perez Jiminez.

Tatu, alisababisha mgongano wa kidiplomasia baina ya Cuba na Marekani, Marekani na Venezuela, Marekani na Hispania, Cuba na Peru.

Vilevile, Marita alijisahau jambo moja kubwa; alikuwa ameanzisha uhusiano wa kimapenzi na Rais wa nchi, hakutakiwa kuchukulia kila jambo kirahisi rahisi tu, tena penzi la mtu aliyeishi misituni na kwake kufanya hujuma dhidi ya binadamu (ikiwamo kuua) ni jambo jepesi hata kama atatabasamu meno yote 32 nje.

Marita na Fidel walionana kwenye meli ya baba yake Marita ambayo ilikuwa ikifanya safari kutoka Ujerumani kupitia Cuba kuendelea na safari yake.

Katika safari hiyo, Marita akiwa binti mbichi wa miaka 18 tu alikutana na Fidel Castro wakati akifanya ukaguzi kwenye meli zilizotia nanga nchini Cuba.

Ukaguzi huo ulikuwa sehemu ya kuhakikisha usalama wa nchi, baada ya kutwaa madaraka kwa njia ya mapinduzi dhidi ya Dikteta Fulgencio Batista. Tangu kuonana kwao Fidel na Marita walichipusha penzi zito ambalo liliwaletea matatizo mazito, hasa kwa upande wa Marita ambaye hakuwa na uzoefu mapenzini. Endelea kusoma kufahamu nini kilichotokea.

Marita: Hallo mpenzi, leo nimetapika sana.

Fidel: Ooh! Pole sana. Wajisikiaje kwa sasa?

Marita: Nina nafuu kidogo, lakini najihisi hali tofauti mwilini. Nina mimba Fidel!

Fidel: Usiwe na wasiwasi Marita, huyo atakuwa mtoto wa Cuba.

Miezi ikapita, mambo ni kama kawaida. Marita akaenda zake Marekani baada ya kuburudishwa na mahaba ya Fidel Castro. Lakini baadae akarejea Cuba katika hoteli ileile alipokuwa akiishi. Mimba ikakua zaidi.

Hata hivyo, wakati fulani Fidel Castro alikwenda ziarani katika majimbo mbalimbali ya nchini Cuba, Marita alibaki hotelini kwa siku tatu zaidi. Kilichotokea hata hajui, bali alizinduka akijihisi kuwa na maumivu makali mwilini.

Mwishowe akakimbia Cuba na kurudi nchini mwake Marekani. Fidel hakuwapo wakati akiumia na kufanyiwa hujuma dhidi ya mimba yake. Je, Mimba iliyeyuka?

Marita hakukubali kirahisi, akataka kufahamu nini kilichotokea katika mimba yake. Akafunga safari tena hadi nchini Cuba kwa lengo la kuonana na Rais Fidel Castro, lakini safari hii akiwa na vidonge viwili vya kumuua Fidel Castro alivyopewa na shirika la kijasusi la CIA.

Ikumbukwe CIA walikuwa walitumia mwanya wa kuhujumiwa Marita Lorenz na kumchochea kumchukia Fidel kwakuwa ndiye chanzo cha yeye kutendewa uovu ndani ya Cuba.

ITAENDELEA

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles