Walimu: Kipaji cha Ndungulu kilitushangaza wengi – 3

0
1614
Katibu wa Idara ya Taaluma, Shule ya Sekondari ya Wavulana Songea (Songea Boys), Mwalimu Oreda Ng’olo

Na MAREGESI PAUL-ALIYEKUWA SONGEA


WIKI iliyopita, tulizungumza na mfanyabiashara wa madini, Ferdinand Masawe, ambaye alieleza jinsi alivyokutana barabarani na mwanafunzi mwenye uoni hafifu, Geofrey Ndungulu, akaamua kumtibu na kumsomesha.

Pia tulizungumza na mama mzazi wa mwanafunzi huyo, Veronica Nditi (63) aliyeko nchini Msumbiji ambaye alieleza jinsi mtoto wake alivyotibiwa na kusoma bila yeye kutarajia.

Katika makala haya, baadhi ya walimu waliomfundisha Ndungulu akiwa shule ya msingi na sekondari, wanaeleza kwa kina maajabu aliyokuwa akiyaonyesha katika masomo.

MWALIMU SHULE YA MSINGI

Mkuu wa Idara ya Wenye Ulemavu katika Shule ya Msingi Luhira, Manispaa ya Songea, Mwalimu Humange Nickson, ambaye ni miongoni mwa walimu waliomfundisha Ndungulu, anasema tangu aanze kufundisha watoto wenye mahitaji maalumu

mwaka 2008, hajawahi kukutana na mwanafuzi mwenye uwezo mkubwa wa kuelewa kama Ndungulu.

Katika maelezo yake, Nickson anasema alipoanza kumfundisha mwanafunzi huyo akiwa darasa la pili, alikuwa akionyesha maajabu kwa kufanya

mambo ambayo hakuyatarajia.

“Yule mtoto pamoja na ulemavu wa macho alionao, IQ yake iko juu kwa sababu nilipokuwa namfundisha darasa la pili, alifanya

hesabu kwa njia ndefu kwa kutumia ubao uitwao A4 frame wakati wenzake huwa wanashindwa.

“Yaani, unaweza kuwapa wanafunzi swali kama 25 mara 25 ili walifanye kwa njia ndefu, wenzake wanashindwa isipokuwa yeye tu.

“Kwa kifupi, tangu nianze kufundisha watoto wenye mahitaji maalumu, sijawahi kukutana na mtu wa aina yake na sidhani kama nitakutana naye tena kwa sababu huyo dogo ana uelewa wa kipekee.

“Kitu kingine nilichokuwa nikimshangaa ni kwamba, yeye hataki kushindwa, yaani ukiwafundisha kitu akashindwa kukielewa sawasawa, atakusumbua kwa kukuuliza maswali hadi atakapokuwa ameelewa vizuri.

“Kwa hiyo, ninachotaka kusema hapa ni kwamba, kwa kuwa huyo kijana ameonyesha nia ya kusoma, naiomba Serikali imuunge mkono kwa sababu inavyoonekana familia yake haina uwezo wa kumlipia ada kwa masomo ya elimu ya juu,” anasema Mwalimu Nickson.

WALIMU SONGEA BOYS

Naye Katibu wa Idara ya Taaluma, Shule ya Sekondari ya Wavulana Songea (Songea Boys), Mwalimu Oreda Ng’olo, anasema alimfundisha Ndungulu alipokuwa kidato cha tatu na cha nne.

“Huyo kijana nilimfundisha ‘form three na form four’ somo la fasihi ya Kingereza kwa maana ya ‘literature’.

“Mwanzoni nilifikiri ni mwanafunzi wa kawaida kama walivyo wengine kwa sababu tumezoea kuona wenye ulemavu wakiwa na akili za kawaida.

“Baadaye nikagundua si mwanafunzi wa kawaida kwa sababu ukiwafundisha kitu darasani, yeye anaelewa haraka zaidi na hata yale ambayo hujawafundisha, anakuwa ameshayajua.

“Kwa kawaida, somo la literature halina ‘material’ nyingi kama masomo mengine kwani mara nyingi tunasoma vitabu.

“Kwa hiyo, ukieleza kitu kwa kifupi, yeye anakwambia kama iko hivi, basi maana yake ni kwamba unamaanisha hivi, jambo ambalo ukiliangalia unakuta ni kweli.

“Hata kwenye kufafanua poems (mashairi), alikuwa vizuri tofauti na wenzake na hapo ndipo nilipokuwa nikimshangaa zaidi,” anasema Mwalimu Ng’olo.

Wakati mwalimu huyo akisema hayo, Mkuu wa kitengo cha elimu shuleni hapo, Mwalimu Ally Thabit, anasema mwanafunzi wake huyo alikuwa na uwezo mkubwa wa kuelewa vitabu alivyokuwa hawezi kuvisoma tofauti na wanafunzi wasiokuwa na matatizo ya macho.

“Huyo kijana nilimfundisha somo la Kiswahili kuanzia kidato cha kwanza hadi kidato cha nne, nakumbuka pamoja na kuwa vizuri katika somo langu, alikuwa akifanya vizuri pia katika masomo mengine.

“Kwa kuwa ana matatizo ya macho, alitakiwa awe anatumia vitabu vya nukta nundu ambavyo ni maalum kwa watu wenye ulemavu wa macho ambavyo sisi hatukuwa navyo.

“Jambo la ajabu ni kwamba, pamoja na kwamba haoni sawasawa, alikuwa akifaulu vizuri kupitia vitabu hivyo hivyo asivyoweza kuvisoma, kuliko hata wanafunzi wasiokuwa na matatizo ya macho.

“Sasa, mpaka hapo unaweza kuona alikuwa na uwezo gani wa kuweza kufaulu kitu ambacho alikuwa hakisomi japokuwa nilikuwa nawafundisha darasani

“Kwa hiyo, naweza kusema ni kati ya watu wenye akili za kuzaliwa na naamini atafika mbali kama Mungu atampa maisha marefu,” anasema Mwalimu Thabit.

WALIMU MPWAPWA SEKONDARI

Mwalimu wa taaluma shuleni hapo, Mhoja Balele, anasema alimfundisha Ndungulu somo la general studies kidato cha sita.

“Yule mwanafunzi ana tabia moja, kwamba anataka kujua kila kitu na ukiona anataka kuuliza swali darasani, basi unatakiwa ujipange kwa sababu anahoji kupita kiasi na kila kitu anataka akijue muda huo huo.

“Wakati mwingine tulikuwa tunamchukia kutokana na uliza yake maana ana tabia ya kuuliza swali analolijua ili kumpima mwalimu uwezo wake.

“Kama sikosei, alipofika kidato cha tano, hakuwahi kushika nafasi ya pili, yaani kila mtihani alikuwa ni wa kwanza na ilikuwa ni lazima apate alama zaidi ya 80.

“Darasa lao lilikuwa na wanafunzi 47 na kumbuka hao aliokuwa akiwaongoza, wengine siyo walemavu, lakini yeye alikuwa akisoma kwa kutumia mashine ya nukta nundu na kufanya maajabu.

“Lakini, alipokuwa kidato cha sita, alionekana kuwa na mawazo mengi na kusababisha kupata division two katika mtihani wa ‘mock’.

“Baada ya kuona matokeo hayo, walimu walishtuka na tulikaa naye na kumuweka sawa na baada ya hapo, akarudi katika hali yake ya kawaida.

“Kwa hiyo, ile ‘division two point’ saba aliyopata kidato cha sita, sisi kama walimu wake hatukubaliani nayo kwani tulijua atapata ‘division one ya point tatu.

“Pamoja na hayo, tunamuombea na kumtakia kila la kheri katika maisha yake ila yule dogo ni kichwa na ni mpambanaji wa kweli,” anasema Mwalimu Balele.

Kwa mujibu wa Mwalimu Balele, uwezo wa Ndungulu unamkumbusha mwanafunzi mwenye uoni hafifu aliyemaliza shuleni hapo mwaka 2012, Farid Abdallah na kupata division one ambaye kwa sasa yuko nchini Uturuki akisoma shahada ya uzamili ya elimu.

Naye Mwalimu wa somo la Historia II, Baraka Ng’umbi, anasema katika somo hilo, Ndungulu hakuwahi kupata chini ya ufaulu wa alama A.

“Alikuwa ‘the best’ unamfundisha anaelewa hadi unashangaa na kikubwa alikuwa ukimfundisha kitu hasahau hata asiposoma tena.

“Alikuwa mwanafunzi wangu wa kipekee kabisa na nasema atabaki kuwa kwenye rekodi ya wanafunzi bora niliowahi kuwafundisha.

“Pamoja na uwezo wa darasani, pia ana kipaji cha kuwaongoza wenzake ikiwa ni pamoja na kuwahimiza wawahi darasani na wasome kwa bidii na alikuwa na nidhamu ya hali ya juu.

“Yaani, mwalimu ukiingia darasani, mtu wa kwanza kutaka kujua kama yupo alikuwa ni Ndungulu kwani tulijua mwishowe atatutoa kimasomaso kwa kupata matokeo mazuri kwenye mtihani wa mwisho.

“Kwa hiyo, hata mimi niliumizwa na matokeo yake ya kwa sababu alitakiwa kupata division one, point tatu au nne,” anasimulia Mwalimu Ng’umbi.

Wakati hao wakisema hayo, Mwalimu wa Elimu Maalum shuleni hapo, Thomas Lendo, anasema hatamsahau Ndungulu kutokana na uwezo wake darasani.

“Huyo kijana sitamsahau maana alikuwa akifanya maajabu kama yaliyowahi kufanywa na wenzake waliohitimu kidato cha sita mwaka 2014 ambao ni Elias Nsimbila na Edward Chengula.

“Wakati mwingine unakosa maelezo ya kutoa, lakini itoshe tu kusema kwamba ana akili za kuzaliwa na mimi ndiye nilikuwa namwandalia notisi kupitia mashine ya nukta nundu,” anasema.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Mpwapwa,Nestory Sanga

Kwa upande wake Mkuu wa shule hiyo, Mwalimu Nestory Sanga, anasema Ndungulu ni alama ya shule yao kutokana na uwezo aliokuwa nao darasani.

“Huyo ni alama yetu kwani nakumbuka aliwahi kuandika barua nyingi kwa waziri mkuu akiomba msaada na mara kadhaa wataalamu kutoka serikalini walikuwa wakija kwa ajili ya kumuona na kutuletea mahitaji mbalimbali,” anasema Mwalimu Sanga.

Wiki ijayo, makala yetu itahusisha kauli ya Serikali kwa watu wenye mahitaji maalum pamoja na Chama cha Wasioona Tanzania.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here