MAHAKAMA YAZUIA WABUNGE 8 CUF KUVULIWA UANACHAMA

0
109

NA KULWA MZEE, DAR ES SALAAM

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam imezuia wabunge wanane wa viti maalumu wa Chama cha Wananchi (CUF) na madiwani wawili wa viti maalumu kujadiliwa na kuvuliwa uanachama hadi uamuzi wa kesi yao ya msingi utakapotolewa.

Uamuzi huo ulitolewa jana na Jaji Lugano Mwandambo, kutokana na maombi yaliyofunguliwa na waliokuwa wabunge wa wanane wa viti maalumu na madiwani wawili wa viti maalumu.

Wabunge na madiwani ni wale waliofukuzwa uanachama wa CUF na nafasi zao zilijazwa na wabunge (Rukia Ahmed Kassim, Shamsia Aziz Mtamba, Kiza Hussein Mayeye, Zainab Mndolwa Amir, Hindu Hamis Mwenda, Sonia Jumaa Magogo, Alfredina Aporinary Kahigi, Nuru Awadhi Bafadhili) ambao Mwenyekiti wa chama hicho anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba, alipeleka majina yao Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Mahakama imetoa uamuzi huo dhidi ya Bodi ya CUF, Profesa Lipumba na Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Magdalena Sakaya.

Pia mahakama hiyo imesema imeizuia Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ambayo pia ilikuwa ni mmoja wa wadaiwa kuwa haina mamlaka ya kuchunguza uamuzi wake.

Jaji Mwandambo alitupilia mbali maombi ya wadaiwa wengine ambao ni wakurugenzi wa Manispaa ya Ubungo na ya Temeke kwa kuwa wadai walikiuka taratibu za kuwashtaki na alisema mahakama haiwezi kutoa nafuu zozote zilizoombwa na waombaji hao dhidi yao.

Waombaji waliiomba mahakama hiyo itoe amri ya zuio la muda dhidi ya Wakurugenzi wa Manispaa za Ubungo na Temeke kutowateua madiwani wengine badala yao na kuwaapisha, kusubiri kumalizika kwa kesi yao ya msingi, waliyoifungua wakipinga kuvuliwa uanachama.

Katika maombi hayo, waombaji walikuwa wakiiomba mahakama kutoa amri ya zuio la muda dhidi ya Bunge kutokuwaapisha wabunge wapya walioteuliwa na NEC, badala yao, lakini zuio hilo dhidi ya Bunge lilitupiliwa mbali mapema baada ya kuwekewa pingamizi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Katika kesi ya msingi namba 143 ya mwaka 2017, wadai hao wanaiomba mahakama hiyo itamke kuwa, uamuzi wa kuwavua uanachama na hatimaye kupoteza nafasi zao ni batili kwa kutokuzingatia kanuni za haki za msingi.

Pia wanaiomba mahakama itamke kuwa, mchakato wote wa kuwashughulikia kinidhamu uliohitimishwa kwa kuwavua uanachama ni batili, kwa kukiuka kanuni za kisheria.

Wadai hao wanadai kuwa, hawakupewa fursa ya kutosha kujitetea, kwa kuwa hawakupewa taarifa kamili kuhusiana na tuhuma zao na kwamba wameadhibiwa adhabu hiyo, na kwamba tayari wameshakata rufaa katika Mkutano Mkuu wa CUF.

Pia wanadai kuwa, adhabu waliyopewa ni kubwa mno kulinganisha na makosa wanayotuhumiwa, huku wakidai kuwa, uamuzi huo umechukuliwa bila kuzingatia hasara si tu watakayoipata wao, bali pia kwa chama na kwa uchumi wa nchi katika mchakato wa kujaza nafasi hizo.

Wadai wengine waliokuwa wabunge wa viti maalumu ni pamoja na Savelina Silvanus Mwijage, Salma Mohamed Mwassa, Raisa Abdallah Musa na Riziki Shahari Mngwali.

Wengine katika nafasi ya ubunge ni Hadija Salum Al-Qassmay, Halima Ali Mohamed na Saumu Heri Sakala, wakati madiwani ni Elizabeth Alatanga Magwaja na Layla Hussein Madib.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na chama hicho kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai, wadai hao walivuliwa uanachama wa chama hicho kwa makosa mbalimbali, yakiwamo ya kukihujumu na utovu wa nidhamu dhidi ya viongozi wakuu wa chama hicho.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here