MAHAKAMA YAFUTA KESI YA DIAMOND, HAMISA MOBETO

0
236

Na KULWA MZEE -DAR ES SALAAM

MSANII Nasib Abdul maarufu Diamond, ameibuka kidedea katika hatua za awali baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuifuta kesi iliyofunguliwa na mwanamitindo, Hamisa Mobeto dhidi yake kutokana na makosa ya kisheria.

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilifikia uamuzi huo jana baada ya kukubaliana na pingamizi la awali lililowasilishwa na Diamond akiomba kesi itupiliwe mbali.

Katika hoja za kupinga kuendelea kwa kesi hiyo, Diamond alidai madai hayo yamefunguliwa mahakamani kimakosa, kwa sababu kifungu cha sheria kilichotumika kufungua kesi si sahihi.

Inadaiwa kifungu hicho hakiipi mahakama mamlaka ya kuendelea kusikiliza kesi hiyo, hivyo aliomba itupwe.

Baada ya hoja hizo Hakimu Mkazi, Devotha Kisoka, anayesikiliza kesi hiyo alikubaliana na hoja za mdaiwa na kuifuta kesi hiyo. Hata hivyo, Mobeto anayo nafasi ya kuirudisha kesi hiyo baada ya kurekebisha upungufu wa kisheria uliojitokeza.

Hivi karibuni Diamond alimjibu Mwanamitindo Hamisa Mobeto kwamba   Sh milioni tano anazotaka kulipwa kila mwezi kwa ajili ya matunzo ya mtoto ni kubwa hivyo hawezi kuzimudu.

Diamond aliwasilisha majibu hayo  baada ya Mobeto kumfungulia kesi ya madai katika mahakama hiyo ya watoto akidai mambo mbalimbali ikiwamo matunzo ya mtoto.

Mobeto katika maombi yake anaiomba mahakama imwamuru Diamond kutoa matunzo ya mtoto wao kila mwezi.

Katika madai yake, Hamisa kupitia mawakili wake, Abdullah Lyana na Walter Godluck wa Kampuni ya Uwakili ya Century Attorneys, pia anamtaka Diamond amuombe msamaha kwa umma kwa kumsababishia madhara yaliyoishtua familia yake.

Mobeto kupitia wakili wake walimpa notisi Diamond ya kutaka amwombe radhi na kupeleka matunzo ya mtoto ndani ya siku saba, lakini notisi hiyo haikutekelezeka hivyo aliamua kulifikisha suala hilo mahakamani.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here