24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

LULU AELEZA YOTE YALIYOTEKEA USIKU ALIOFARIKI KANUMBA

Msanii wa filamu, Elizabeth Michael ‘Lulu’ (kushoto), akipitia mafaili baada ya kukutwa na hatia kujibu mashtaka katika kesi inayomkabili ya tuhuma za kumuua bila kukusudia msanii mwenzake, Steven Kanumba.

PATRICIA KIMELEMETA

BAADA ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, kueleza kuwa Msanii wa Bongo movie, Elizabeth Michael ‘Lulu’ (22) ana kesi ya kujibu juu ya kifo cha marehemu, Steven Kanumba, Lulu ameieleza mahakama mambo yote yalitokea usiku aliofariki msanii huyo.

Akitoa utetezi wake mbele ya Jaji wa mahakama hiyo, Sam Rumanyika, Lulu alisema Kanumba alikuwa akimpiga mara kwa mara na siku ya tukio alitumia panga kumpiga nalo katika sehemu mbalimbali za mwili.

Alisema awali walikuwa wana uhusiano wa kawaida na marehemu Kanumba, lakini miezi minne kabla ya Kanumba kufariki waliingia kwenye uhusiano wa kimapenzi.

Alidai kabla ya marehemu kufariki, alikuwa na tabia ya kumpiga mara kwa mara na kwamba hata siku ya mwisho alitumia panga kumpiga nalo sehemu mbalimbali za mwili wake.

Alieleza kuwa, siku ya tukio ilikuwa Ijumaa Kuu ya Pasaka ya mwaka 2012, ambapo saa mbili usiku alienda nyumbani kwa rafiki zake Mikocheni kwa ajili ya kujiandaa ili aongozane nao kwenda klabu kucheza disko.

Alieleza kuwa, ilipofika saa tano usiku wakati yupo Mikocheni, alipigiwa simu na marehemu Kanumba ambaye alimtaka aende nyumbani kwake Sinza ili watoke wote.

Alieleza kuwa, kwa sababu Kanumba alikuwa anamsumbua kwenye simu mara kwa mara, akalazimika kuwaomba ruhusa rafiki zake ili aende nyumbani kwa Kanumba kwa ajili ya kusikiliza anachomwitia.

Alieleza kuwa, wakati huo alikuwa saa sita kasoro usiku ambapo aliendesha gari hadi nje ya nyumba ya Kanumba na kumpigia simu ya kumweleza kama alishafika.

“Marehemu alikuwa anapenda kupiga sana, niliogopa… Nikalazimika kuondoka Mikocheni na kwenda nyumbani kwake ili nimsikilize anachoniitia,” alieleza.

Alieleza kuwa alipofika alimpigia simu na kumwambia yupo nje ya geti, ambapo Kanumba alimjibu kuwa, mlango uko wazo aingie ndani.

Alieleza kuwa, alishuka kwenye gari lake alilokuwa anaendesha na kuingia ndani ya nyumba hiyo ambapo alimkuta Kanumba kwenye korido, huku akiwa amevalia taulo kiunoni na mkononi ameshika chanuo anachana nywele zake.

Alieleza kuwa, kwa sababu Kanumba alikuwa msafi, anajipenda, alikuwa anatumia mafuta maalumu kwa ajili ya kupaka kwenye nywele zake.

Alieleza kuwa, wakaingia wote chumbani, Kanumba alimwambia Lulu amemwita ili waende wote kwenye bendi ya muziki, lakini Lulu alikataa kwa madai kuwa hapendi muziki wa wazee bali anapenda kwenda disko kwa vijana wenzake.

Alieleza kutokana na hali hiyo, kulitokea mabishano ya muda kuhusiana na wapi waende, ndipo Lulu alipomwambia Kanumba ya kwamba yeye atabaki nyumbani.

“Kanumba alikuwa anapenda kwenda kwenye bendi za muziki mimi nilikataa kwa sababu wazee ndiyo wanaopenda muziki na mimi napenda kwenda disko,” Lulu alieleza.

Alieleza kuwa, marafiki zake walimpigia simu ya  kumuuliza kama watakwenda disko au laa, ambapo alielekea kwenye korido ili awajibu wamsubiri kidogo.

Alieleza kuwa, wakati yupo kwenye korido anaongea na simu, Kanumba alikwenda na kumwambia kuwa, kwanini anaongea na mwanamume mwingine mbele yake, ambapo alimjibu kuwa, hakuwa mwanamume bali ni rafiki zake.

“Tulianza kubishana na baadaye akanivuta na kuniingiza chumbani, nikaangukia kitandani, akaanza kunipiga, nikaogopa kupiga kelele kwa sababu hatukutaka waandishi wa habari wala magazeti kujua habari zetu,” alieleza.

Alieleza kuwa, alipoona kipigo kimeongezeka, alilazimika kukimbia nje ya nyumba hiyo kwa ajili ya kuomba msaada lakini Kanumba alimkimbiza hadi nje ya geti huku akiwa amevalia taulo.

“Nilipoona amenifuata hadi nje, nikaogopa, nikalazimika kukimbia hadi ukumbi wa Vatican ambao kipindi hicho ulikuwa pagala tu, wala hakukuwa na kitu chochote huku nikidhani kwamba hawezi kunifuata, lakini alinifuata hadi uko Vatican huku akiwa amevaa taulo,” alieleza.

Lulu alieleza kuwa baada ya hapo alimburuza na kumrudisha nyumbani kwake, walipoingia ndani alimburuza hadi chumbani na kumtupa kitandani huku akiendelea kumpiga.

Alieleza kuwa, wakati huo umeme umekatika na chumbani kulikuwa na taa ya mshumaa, lakini aliendelea kumpiga hivyo hivyo na baadaye alichungulia chini ya uvungu wa kitanda na kuchukua panga na kuanzia kumpiga nalo huku akimwambia kuwa atamuua.

“Alinipiga sehemu mbalimbali za mwili kwa kutumia panga lakini nilishindwa kujitetea, baadaye aliniinua na kunisukuma, nilipopata upenyo nikainua.

“Wakati huo alijigonga kwenye ukuta, wakati anainuka tena, nikakimbilia chooni ndani ya chumba hicho na kujificha.

“Baadaye nikasikia mlio mwingine wa kitu kizito kama kimeanguka chini, nikadhani amebamiza mlango  kutokana na hasira zake na kudondoka au  kuna kitu kimeanguka au labda hasira zake zimemfanya agonge kitu,” alieleza.

Lulu alieleza kuwa, baadaye kidogo akasikia Kanumba anahema kwa sauti nzito sana, alidhani amepandwa na hasira hivyo anaweza kumuua kwa sababu alishamtamkia kumuua.

Alieleza kutokana na woga aliyonayo, alilazimika kubaki chooni kwa muda ili kusubiri kinachotokea na alipoona kimya kimezidi ndipo alipotoka chooni na kumkuta Kanumba ameanguka chini huku anahema sana.

Alieleza kuwa, kutokana na hali hiyo, alimwambia Kanumba kuwa, asijifanye ameanguka makusudi na kwamba watu wakiingia ndani atawaambia kuwa amempiga muda mrefu na amemuumiza.

“Nilimwambia Kanumba hata kama anajifanya amezimia, wakija watu nitawaambia umetoka kunipiga na panga, lakini hakunijibu, ila nikaendelea kumwambia hivyo hivyo,” alieleza.

Lulu alieleza alipoona hamjibu tena, akamwita mdogo wake Seth Bosco ambaye alikuwa akiishi naye na kumwambia Kanumba  amempiga na kuanguka.

Alieleza, Bosco akaingia chumbani na kuanza kumwamsha lakini hajaamka, ndipo alipomwambia amsubiri ili aende kumwita daktari wake ambaye ni Paplas ili aje kumwangalia.

Alieleza, wakati Bosco alipoenda kumwita daktari, alimwambia yeye anaondoka kwa sababu anaogopa Kanumba akiinuka anaweza kumpiga tena na kumuumiza.

Alieleza kuwa, wakati huo alikuwa hajui kama Kanumba alikuwa ameshafariki, alidhani amezimia ili akiamka aweze kumpiga tena.

“Nikamwambia Seth hauwezi kunikuta kwa sababu akiamka hapa anaweza kunipiga tena, lakini Seth alinilazimisha nibaki lakini mimi niliondoka.

“Niliwasha gari hadi fukwe za Coco (Coco Beach) ambapo nilienda kupumzika peke yangu saa tisa usiku, lakini wakati huo niliendelea kuwasiliana na Dk. Paplas kujua kinachoendelea,” alieleza.

Alieleza kuwa, wakati yupo Coco Beach, alikuwa akitumiwa meseji na rafiki zake za kumuuliza kama ana taarifa za kifo cha Kanumba, kwa sababu wengi wao walikuwa wanajua uhusiano wao wa kimapenzi.

Lulu alieleza kwa sababu alikuwa hajui chochote na hivyo aliendelea kuwasiliana na Dk. Paplas ambaye hajamweleza chochote kuhusiana na suala hilo, licha ya kumuuliza mara kwa mara lakini alikuwa akimjibu kuwa hajafa, bali yupo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) anapatiwa matibabu.

Alieleza, baadaye Dk. Paplas alimpigia simu ya kumuomba waonane Bamaga ambapo alikubali na kwenda kwenye eneo hilo kwa ajili ya kukutana na Dk. Paplas ndipo alipokamatwa na Polisi.

Alieleza kuwa alipelekwa Kituo cha Polisi Oysterbay na kuhojiwa zaidi ya mara tatu na maofisa mbalimbali wa Polisi.

Alieleza kwa sababu mwili ulikuwa unamuuma, alilazimika kuwaambia Polisi kwamba anaumwa ili waweze kumpeleka hospitali kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

Alieleza, ndipo alipokabidhiwa kwa mpelelezi wa kesi hiyo aliyemtaja kwa jina moja la Renatus ambaye alimchukua na kumpeleka Hospitali ya Mwananyamala ili aweze kutibiwa.

“Wakati wote huo, nilikuwa nazunguka na Renatus kila mahali, nilikuwa sijui kama Kanumba amefariki ila baadaye niliporudi mahabusu, wakati nipo ndani mahabusu wenzangu wakanambia kuwa Kanumba amefariki,” alieleza.

Wakati Lulu anaendelea kujitetea, Jaji Rumanyika alimuuliza mshtakiwa huyo kuwa, leseni ya kuendesha gari aliipata wapi, ambapo alijibu kuwa, wakati huo alikuwa anaendesha gari bila ya kuwa na leseni yoyote.

Wazee wa baraza walimuuliza kuwa, wanataka mahakama ifanyeje katika kesi hiyo, ambapo alijibu kuwa hajafanya kosa lolote kama alivyoeleza hapo awali.

Katika kesi hiyo, upande wa utetezi kupitia kwa Wakili wake, Peter kibatala, aliiomba mahakama hiyo kuongeza shahidi mwingine ambaye ni mke wa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Josephine Mushumbus, ili atoe ushahidi wake.

Kibatala alidai kuwa, shahidi huyo ni muhimu lakini yupo Canada na kuiomba mahakama hiyo kumpa hati ya wito wa mahakama ili aweze kufika na kutoa ushahidi wake.

Awali, kabla ya Lulu kujitetea, upande wa Jamhuri ulileta shahidi wa mwisho ambaye ni daktari bingwa wa uchunguzi wa magonjwa mbalimbali ya binadamu na vifo vyenye utata kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Inocent Mosha.

Akiongozwa na wakili wa upande wa Jamhuri, Faraja George, Daktari Mosha aliileza kuwa, Aprili 9, mwaka 2012 akiwa Muhimbili alipokea amri halali ya Polisi ikiamuru kufanya uchunguzi wa mwili wa Kanumba uliokuwa umehifadhiwa chumba cha kuhifadhia maiti.

Alieleza kuwa, kutokana na hali hiyo, walichukua maiti na kuanza kuikata vipande vipande ili waweze kuipeleka kwa mkemia kwa uchunguzi zaidi.

Alieleza kuwa walichukua kipande cha utumbo ili kuangalia na chakula, kipande cha ini, figo, mkojo, damu, maji maji kwenye jicho na kucha.

Alieleza kuwa wakati wa uchunguzi huo, walikuwa na mashahidi wawili walisaidia kutambua mwili wa marehemu ambapo walianza kuangalia kama kuna majeraha yoyote nje ya mwili.

“Tuliangalia kwenye kucha zake za vidole ambazo zilikua na rangi ya bluu, tulifungua viungo vya ndani vya mwili pamoja na kwenye kisogo  ambapo tuliona damu imevilia, ikabidi tufungue fuvu la kichwa ambalo tuliona ubongo umevimba,” alieleza.

Dk. Mosha.

Alieleza kuwa kwenye mishipa midogo midogo ya ubongo inayosambaza damu kichwani ilikuwa imevilia damu na sehemu ya chini ya ubongo kulikuwa na mkandamizo wa damu.

Alieleza kuwa walifungua mapafu, moyo, figo, maini, tumbo na mifumo mingine ya mwili ili kuangalia kama kuna jeraha lolote lakini walikuta hakuna tatizo.

Dk. Mosha alieleza kuwa, taarifa yake aliyoiandaa kwenda kwa mkemia, ilionyesha kuwa marehemu alikuwa na tatizo kwenye mfumo wa upumuaji ambapo ulishindwa kufanya kazi kutokana na majeraha kwenye ubongo.

“Marehemu hakuwa na jeraha lolote la nje, lakini mapafu yake yalikuwa yamejaa damu ikabidi tumkate  kucha ii kuangalia vinasaba, tulichukua majimaji ya kwenye jicho kuangalia kiasi cha pombe na sukari kwenye mwili,” alieleza Dk. Mosha.

Alieleza kuwa, pombe haiwezi kusababisha matatizo hayo moja kwa moja  badala yake mabadiliko ya tabia yanayotokana na unywaji ndio yanaweza kuchangia.

Alieleza kuwa, wakati wanafanya upasuaji, si lazima ndugu wa marehemu wawepo, kwa sababu suala hilo ni la kitaalamu zaidi ambalo linahitaji uchunguzi wa kina.

Hata hivyo, Jaji Rumanyika alimwambia mshtakiwa ana kesi ya kujibu kutokana na upande wa Jamhuri kumaliza mashahidi wake na kutoa muda wa nusu saa ili kujiandaa na utetezi.

Jaji Rumanyika aliahirisha kesi hiyo hadi leo kwa ajili upande wa mashtakiwa kueleza taarifa za ushahidi kwa shahidi wao Josephine.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles