25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Lukuvi akabidhi taarifa ya mgogoro Mabwegere

Na MUNIR SHEMWETA-MOROGORO             |           


WAZIRI wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, amekabidhi taarifa ya uchunguzi wa mgogoro wa Kijiji cha Mabwegere na vijiji saba vya Wilaya ya Kilosa na mpango wa utekelezaji wake.

Pia ameagiza wote waliohusika kupotosha mipaka ya eneo hilo akiwamo Mkurugenzi Msaidizi wa Upimaji na Ramani wa Wizara ya Ardhi kuchukuliwa hatua za kisheria.

Agizo hilo alilitoa jana mkoani hapa wakati akikabidhi taarifa ya uchunguzi iliyofanywa na Jaji wa Mahakama Kuu ambaye sasa ni Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Jacob Mwambegele kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk. Kebwe Stephen kuhusu mgogoro wa mipaka ya Kijiji cha Mabwegere na vijiji jirani vya Mambegwa, Mbigiri, Dumila, Matongolo na Mfulu vilivyopo Wilaya ya Kilosa.

“Wote walioshiriki kwa namna moja ama nyingine katika ‘process’ yote ambayo kwa kiasi fulani imeigharimu Serikali fedha nyingi na kuipa maumivu Serikali katika suala hilo ni lazima wachukuliwe hatua kali,” alisema Lukuvi.

Taarifa hiyo ya uchunguzi ilibaini chanzo cha mgogoro ni kukosekana ushirikishwaji wa vijiji jirani katika kuainisha na kuweka mipaka ya Kijiji cha Mabwegere jambo lililosababisha kijiji hicho kiwe na eneo la ukubwa wa hekta 10,234 kuliko hata kijiji mama cha Mfulu chenye hekta 1,717.

Hatua hiyo ilibitishwa na ukweli kwamba mipaka ya kijiji hicho imeingia ndani ya mipaka ya kata zote tatu za Mbigiri,  Msowero na Kitete ingawa kiutawala kinaratibiwa Kata ya Kitete.

Waziri Lukuvi alisema wizara haijakifuta Kijiji cha Mabwegere bali ni kutekeleza taarifa ya uchunguzi ya kufuta mipaka ya kijiji hicho ambapo sasa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kwa kushirikiana na Wilaya ya Kilosa itatakiwa kuanza mchakato wa kuandaa upya mipaka ya vijiji hivyo kwa njia shirikishi.

Awali akiwasilisha taarifa ya uchunguzi, Jaji Mwambegere, alipendekeza kwa nia ya kuboresha utendaji kazi, weledi,  maadili na umakini na uwezo wa kulinda na kutunza kumbukumbu katika Idara ya Upimaji na Ramani na Ofisi ya Kamishna wa Ardhi hatua za kinidhamu zichukuliwe ili kuzuia migogoro ya ardhi.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Tamisemi, Joseph Kakunda alisema uanzishwaji Kijiji cha Mabwegere haukufuata sheria na kuwataka wataalamu kuacha kuwa na  nidhamu ya woga na kuzingatia kanuni na sheria katika kutekeleza majukumu yao.

Naye Naibu Waziri wa Kilimo, Dk. Mary Mwanjelwa, alisisitiza hatua kuchukuliwa kwa wote waliohusika na kusema katika Serikali hii ya awamu ya tano ni lazima kufufua makaburi kwa minajili ya kubaini wote waliohusika kuidanganya Serikali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles