24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

LIGI KUU NI MOTO

NA AYOUB HINJO



KADIRI siku zinavyosonga, Ligi Kuu Tanzania Bara inazaidi kushika kasi na kufanya kuwa na ushindani zaidi licha ya kutokuwa na mdhamini mkuu mpaka sasa.

Wakati mwingine ni ngumu kwa timu ambazo hazina vyanzo vingi vya mapato kukaa sawa kiuchumi, ikiwa kila timu inategemea mapato ya milangoni ili kujiendesha.

Hivi karibuni timu ya Ndanda ilijikuta kwenye wakati mgumu iliposhindwa kulipa huduma ya malazi ikiwa mkoani Singida ambako ilikwenda kucheza mechi dhidi ya wenyeji wao, Singida United.

Inawezekana kila mmoja alishangazwa na taarifa hiyo, lakini kiuhalisia Ndanda ni sehemu ndogo tu ya matatizo yetu ya kila siku yanayoendelea kutokea katika Ligi Kuu Tanzania Bara.

Pamoja na hayo yote, bado ligi imekuwa na ladha ya kuvutia kwa kila timu kujitoa kisawa sawa inapokuwa uwanjani ili kupata pointi tatu zitakazofanya kushinda ubingwa au wengine waepuke kushuka daraja.

Msimu huu wa Ligi Kuu ulianza Agosti 22 na kushuhudia ongezeko la timu hadi kufikia 20 kutoka 16.

Ili kutengeneza idadi hiyo ilibidi zishuke timu mbili ambazo zilikuwa Njombe Mji na Majimaji, huku sita zikipanda ambazo ni KMC, Biashara United, Alliance FC, JKT Tanzania, Coastal Union na African Lyon.

Makala haya yanakuletea uchambuzi wa michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyopigwa hivi karibuni katika viwanja mbalimbali hapa nchini.

YANGA YAENDELEA KUITESA SIMBA

Kwa kiasi kikubwa mashabiki wa timu ya Simba kabla ya kuanza kwa ligi walionekana kutamba kwa kiasi kikubwa kutokana na ubora wa kikosi chao kilivyo.

Walifanya usajili wa wachezaji wazuri ambao walitamba katika timu mbalimbali hapa nchini na nje ya nchi.

Pamoja na hayo yote, Yanga inaonekana kuwa katika kiwango kizuri, huku ikifanikiwa kufunga mabao mengi zaidi tofauti na ilivyotegemewa na wengi.

Mpaka kufikia mzunguko huu wa 10, timu ya Yanga ndiyo inayoongoza kwa kupachika mabao mengi kuliko timu nyingine yoyote katika Ligi Kuu Tanzania Bara.

Yanga imepachika mabao 14, ikifuatiwa kwa ukaribu na Mbeya City na Azam zilizopachika mabao 12, huku timu za Simba, Singida United na Mtibwa Sugar zikifunga mabao 11 mpaka sasa.

Mabingwa hao mara 27, wamecheza michezo saba, huku wakishinda sita na kutoa sare mmoja na kuwafanya kuvuna pointi 19, nyuma ya vinara Azam wenye pointi 21, baada ya kucheza mechi tisa, wakishinda sita na sare tatu.

Simba inakamata nafasi ya tatu, baada ya kucheza michezo nane na kupata pointi 17, ikishinda mitano, sare mbili na kufungwa mmoja.

AZAM UKUTA HATARI, STAND OVYO

Mpaka kufika katika mzunguko wa tisa kwa Azam, safu yao ya ulinzi imeruhusu kufungwa mabao mawili tu, idadi ndogo zaidi kuliko timu yoyote mpaka sasa.

Simba iliyopo nafasi ya tatu na JKT Tanzania inayokamata nafasi ya nane, imeruhusu mabao matatu, huku Yanga nyavu zao zikiguswa mara nne tangu msimu kuanza.

Lakini timu ya Stand United ipo katika wakati mgumu, imecheza michezo 10 na kuruhusu mabao 15 ambayo ni mengi zaidi kuliko timu yoyote mpaka sasa.

Timu za Mbeya City na Alliance FC zinakamata nafasi ya pili kwa kufungwa mabao mengi, zote zimepigwa 13.

ALLIANCE, AFRICAN LYON  MMH!

Mpaka sasa katika mzunguko wa 10 kwa Alliance na African Lyon zimefanikiwa kuvuna pointi sita tu, sawa na Mwadui waliocheza michezo tisa ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Timu hizo tatu zinakamata mkia zikitofautiana idadi ya mabao waliyofunga na kufungwa, Alliance wamefungwa michezo sita, sare tatu na ushindi mara moja sawa na African Lyon huku Mwadui wakifungwa mitano, sare tatu na kushinda mmoja.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles