23.6 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

KIPIMO CHA PILI CHA LOWASSA

*RPC Arusha apiga kambi Monduli na vikosi mbalimbali

* Ukonga kampeni zafungwa na Heche, Matiko, Bulaya na CCM Dk. Bashiru



AGATHA CHARLES (DAR) Na ELIYA MBONEA (ARUSHA)

Wakati leo wafuatiliaji wa siasa wakielekeza macho na masikio katika majimbo mawili ya Ukonga, Dar es Salaam na Monduli, Arusha yanayofanya uchaguzi wa wabunge wake, matokeo hasa katika Jimbo la Monduli yanatazamwa kama kipimo kingine cha pili kwa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa baada ya kugeukia siasa za mageuzi tangu alipojiunga na upinzani mwaka 2015.

Kipimo cha kwanza cha Lowassa  kilionekana katika Uchaguzi Mkuu uliopita wa mwaka 2015 baada ya kuenguliwa CCM kugombea urais na kujiunga Chadema ambako aligombea nafasi hiyo akiwa na lundo la wafuasi.

Hatua ya Lowassa kujiunga upinzani ilisababisha upepo kuvuma vibaya kwa upande wa CCM na hata kusababisha Jimbo la Monduli lenye historia ya pekee kisiasa na kiserikali kwenda mikononi mwa upinzani (Chadema).

Jimbo la Monduli ambalo lina histori ya kutoa mawaziri wakuu wawili, Lowassa na hayati Edward Sokoine ndilo ambalo katika uchaguzi huu linatolewa macho kwa nguvu na vyama hivi viwili vya CCM na Chadema pengine kuliko hata Ukonga.

Wagombea Yonas Laizer (Chadema) na Julius Kalanga aliyesimamishwa na CCM baada ya kuhama chama hicho cha upinzani, wanaonekana kuchuana kwa ukaribu katika kampeni hizo  wakisaidiwa na wanasiasa wengine, wakipambana kusaka kura za wananchi 82,242 waliojiandikisha katika vituo 256.

Kama ambavyo inajulikana pengine kwa historia, siasa za Monduli zimetofautiana na maeneo mengine kwani linaongozwa sana na imani juu ya mtu na si chama.

Hisia za wengi na hasa wananchi wa Monduli  kwa Lowassa kama ilivyokuwa kwa marehemu Sokoine, ni kwamba mtu akishikwa mkono kunadiwa na Waziri Mkuu huyo wa zamani lazima atapita na hicho ndicho kinachosubiriwa sasa.

Itakumbukwa Lowassa ndiye aliyemwachia Kalanga jimbo hilo baada ya kulitumikia kwa miaka 20 kuanzia 1995 hadi 2015 alipoingia katika kinyang’anyiro cha urais.

Kalanga ambaye alishikwa mkono na Lowassa katika kinyang’anyiro hicho cha mwaka 2015, alimbwaga mtoto wa hayati Sokoine, Namelock.

Wachambuzi wa mambo wanasema hata Namelock angeshikwa mkono na Lowassa wakati huo asingeangushwa na Kalanga.

Katika Uchaguzi Mkuu wa 2015, Kalanga wakati huo akigombea kupitia Chadema, aliibuka mshindi kwa kura 35,024 huku Namelock akipata 25,925 na hivyo kuandika ukurasa mpya wa siasa za jimbo hilo kwa upinzani.

Kutokana na hilo, Lowassa anatazamwa kuwa na kibarua kikubwa cha kuhakikisha Laizer aliyemshika mkono kumnadi anapita na kurudisha jimbo hilo mikononi mwa Chadema.

Lakini pia wafuatiliaji wa siasa wanasema endapo uchaguzi huo utakuwa huru na haki, Kalanga akishinda na kulipeleka jimbo hilo CCM pasipo kushikwa mkono na Lowassa, pia naye atakuwa ameandika historia yake.

Uchaguzi unaofanyika leo Monduli na Ukonga, umebeba taswira moja ambayo msingi wake ni hamahama ya wabunge na madiwani wa upinzani kwenda CCM ambako wamechaguliwa tena kugombea nafasi hizo.

Kutokana na vuguvugu hilo, hadi mwezi uliopita, iliripotiwa kwa Monduli pekee madiwani 10 waliojiuzulu na kujiunga na chama tawala ni wale waliohama na Lowassa awali kujiunga na Chadema.

Kampeni za uchaguzi unaofanyika leo katika majimbo hayo na kata 22 zilimalizika jana huku kila chama kikiacha rekodi ya kutumia wanasiasa wake machachari, wakiwamo wabunge kuweka kambi ili kuhakikisha mgombea wao anashinda.

Miongoni mwa wanasiasa ambao CCM  iliwatumia kupiga kambi Monduli ni Meneja wa kampeni William ole Nasha (Ngorongoro),  Joseph Kasheku maarufu Musukuma (Geita Vijijini), Waziri wa Tamisemi, Selemani Jafo, Sixtus Mapunda (Mbinga), Edward Sanda (Kondoa Mjini), Catherine Magige (Viti Maalumu), Dk. Godwin Mollel (Siha), Jitu Son (Babati Vijijini) na Dk. Stephen Kiruswa (Longido).

Wakati CCM ikiwa na safu hiyo, Lowassa ambaye alikwenda Monduli kuongeza nguvu, alisema hata wangekwenda zaidi ya wabunge 100 wangenyooshwa.

Lowassa ambaye alikuwa akimnadi Laizer, alisema alimpigania Kalanga kupata ubunge lakini aliwasaliti, hivyo aliweka kambi huko akiwa na  wanachama na wabunge kadhaa wa Chadema  pamoja na mwanawe Fredy kwa lengo la kunusuru nafasi hiyo kurudi CCM.

Vyama tofauti vya siasa vinashiriki uchaguzi huo, lakini mchuano mkali ni baina ya CCM na Chadema huku CUF ambacho kina mgogogoro kwa upande wa Bara kikipita kati yao.

 

RPC ARUSHA APIGA KAMBI MONDULI

Akizungumza mjini Monduli jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Ramadhan Ng’anzi, alisema atasimamia kwa karibu usalama kipindi chote cha kupiga kura na kutangaza matokeo.

Katika kuimarisha ulinzi, RPC Ng’anzi aliwataka wananchi wilayani Monduli wenye sifa za kupiga kura, kujitokeza vituoni ili kutimiza haki yao ya msingi na ya kikatiba.

“Kampeni zilikuwa tulivu, tutahakikisha utulivu huo unaendelea, askari kutoka vikosi mbalimbali watakuwapo kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa usalama.

“Niwatake wananchi wa Monduli wakishapiga kura kuondoka na kuendelea na majukumu yao ya kawaida wakati wakisubiria matokeo,” alisema Kamanda Ng’anzi.

Aidha, RPC Ng’anzi alitumia fursa hiyo kuwaonya baadhi ya watu wanaopanga kufanya fujo akisema watachukuliwa hatua kali za kisheria, ikiwa ni pamoja na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

 

UKONGA

Kwa upande wa Jimbo la Ukonga, Mwita Waitara aliyejiondoa Chadema na kujiunga na CCM akipeperusha bendera ya chama hicho tawala, ana kibarua cha kupambana na binti mdogo aliyesimamishwa na chama hicho cha upinzani, Asia Msangi.

Pamoja na kueleza atakachofanya katika jimbo hilo huku akitumia mwongozo ambao ni ilani ya CCM, Waitara pia alikuwa akitumia muda mwingi kujibu hoja za wapinzani wake ambao ni chama chake alichokihama – Chadema.

Miongoni mwa hoja zilizotumiwa sana na Chadema na ambazo wengi wanasubiri kuona kama zitaleta athari endapo uchaguzi utakuwa huru na haki, ni ile ya kudai kuwa eti Waitara alinunuliwa na CCM.

Waitara mwenyewe amekuwa akikanusha hoja hiyo na kutaja sababu kadhaa, miongoni mwake kutofurahishwa na mwenendo wa upinzani, lakini pia akidai CCM kuna mwongozo ambao ni ilani iliyonadiwa na Rais Dk. John Magufuli wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka 2015.

Kwa upande wa Chadema, jana kampeni zilifungwa na Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko, Ester Bulaya (Bunda Mjini), John Heche (Tarime Vijijini) na Anatropia Theonest (Viti Maalumu) ambao wote walimwombea kura Asia.

Septemba 7, mwaka huu, Mkurugenzi wa Operesheni wa Uchaguzi (Chadema) Jimbo la Ukonga, Benson Kigaila, aliwaambia waandishi wa habari katika mkutano uliofanyika ngome ya jimbo hilo, kuwa mwaka 2015 kulikuwa na vituo 659 na watu waliojiandikisha walikuwa 293,000 idadi inayoweza kupungua au kuongezeka wakati wananchi wa jimbo hilo watakapokuwa wanapiga kura leo.

Kwa upande wa CCM kampeni katika jimbo hilo zilifungwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Bashiru Ally.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles