24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Kijiji cha mauaji chakimbiwa

Mkazi wa Kitongoji cha Kibatini Kata ya Mzizima, mkoani Tanga, akiwa amebeba mizigo yake akihama eneo hilo baada ya kutokea mauaji ya kuchwa kwa watu nane hivi karibuni.

NA OSCAR ASSENGA, TANGA

NI ukimya umetawala. Ndiyo hali unayoweza kukutana nayo pindi unapofika katika eneo la Kibatini, Mtaa wa Mleni, Kata ya Mzizima jijini Tanga, ambako ni eneo yalipotokea mauaji ya kuchinjwa watu wanane.

Tukio hilo la kuhuzunisha lilitokea Juni Mosi mwaka huu. Inadaiwa watu wanaoaminika kuwa majambazi, walivamia duka moja lililoko katika mtaa huo na kuwateka watu wanane wa familia mbili, kisha kuwachinja na kuiba mchele na biskuti.

Katika tukio hilo, wauaji hao waliwaua kinyama kwa kuwachinja Mikidadi Hassan (70), Issa Ramadhani (25) na watu wengine waliotajwa kwa jina moja moja la Kadir, Salim ambao ni wachunga ng’ombe na Mahamudu ambaye ni raia wa Kenya, anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 35 na 40.

Watu hao walianza kuvamia nyumbani kwa mjumbe wa Serikali ya mtaa huo, Issa Hussein (50), aliyekuwa na duka lililokuwa na vitu hivyo na kisha kuwachukua wengine; Mkola Hussein (40) na Hamisi Issa (20), ambao wote walichinjwa.

Kutokana na hali hiyo, MTANZANIA ilifanya ziara maalumu katika mtaa huo na kukuta kuna watu wawili tu waliosalia, ambao wanalindwa na vikosi vya ulinzi na usalama chini ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Kati ya watu hao waliobaki katika eneo hilo ambao wote ni wazee, yupo Mohamed Abdulrahman (70), ambaye alisema kuwa hawezi kuhama kwani ndipo alipozaliwa na zilipo mali alizoachiwa na wazee wake.

“Ni bora waniue hapahapa, lakini siwezi kuhama hata kidogo, sasa nipo peke yangu nahangaika, sina hata wa kunipikia maana familia yangu wote wamekimbia kwa hofu ya kuuawa.

“Kila jambo lina wakati, eneo letu ambalo tulikuwa tukiishi kwa raha sasa limegeuka kuwa la mateso na huzuni mithili ya watu ambao tumefanya dhambi kubwa na sasa tunawindwa. Nitabaki hapahapa ili kama wakiweza waje watumalize mimi na mwenzangu tulioamua kubaki,” alisema Abdulrahman.

Diwani wa Kata ya Mzizima, Fredrick Charles (CCM),  alisema tukio la kuchinjwa limeleta hofu kwa wananchi wa maeneo hayo, ingawa Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na JWTZ bado wanaendelea kuimarisha doria.

 

Alisema hali hiyo imejenga hofu miongoni mwa wananchi waliokuwa katika eneo hilo, ambao kwa sasa karibu mtaa mzima wamehama makazi yao.

“Watu wengi ambao si raia walikuwa wakitumia eneo hili, wakazi wa hapa inadaiwa kuwa walikuwa wakipokea wahamiaji haramu ambao walikuwa wakitokea nchi mbalimbali ikiwemo Ethiopia, ambao walikuwa wakielekea nchini Afrika Kusini.

“Na hili eneo kama unavyoliona, sehemu kubwa ni pori  ambalo limezungukwa na mashamba ambayo yanafikia ukubwa wa kilometa nane kutoka Tanga mjini. Na hapa hata watu waovu huweza kujificha na usijue kama kuna waovu,” alisema Diwani Charles.

Akisimulia tukio hilo, mjane wa marehemu Mkola Hussein,  aliyejitambulisha kwa jina la Asha Saidi, ambaye amehamia Tanga mjini, alisema hatasahau tukio la kuuawa kwa mume wake na watu hao ambao anaona ni kama ‘wachawi’ wa maisha yake.

“Siku ile usiku nilisikia watu hao wakimuita mume wangu (marehemu Mkola) na kumwambia atoke nje na aseme wapi walipo watoto wetu, aliwauliza “nyie kina nani”, wakajibu “sisi ni maaskari”. Alipotoka walianza kumpiga huku wakimwambia aonyeshe walipo.

“Baada ya muda nikasikia kelele za mume wangu ndipo nilipolazimika kutoka na kukuta amefungwa macho kwa vitambaa vyeusi akiwemo na kaka yake, shemeji yangu Issa  Husein pamoja na Hamisi Issa, ambao wote walinyang’anywa uhai wao. Kwangu ni kidonda ambacho hakiwezi kukauka katika moyo wangu hadi ninakwenda kaburini,” alisema Asha huku akibubujikwa na machozi.

Akizungumza na MTANZANIA, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Leonard Paul, alithibitisha kusalia watu wawili katika eneo hilo.

Alisema watu hao waliobaki katika eneo hilo ni wanaume  ambao kwa sasa wanaendelea na maisha yao, huku vyombo vya dola vikiendelea kuimarisha ulinzi usiku na mchana.

“Ni kweli wamebaki watu wawili katika eneo la Kibatini, lakini pamoja na hayo sisi kama Jeshi la Polisi ni wajibu wetu kulinda usalama wa raia na mali zao. Na tutahakikisha huu mtandao wa wahalifu tunaukomesha kabisa,” alisema Kamanda Paul.

Alisema kuwa matukio hayo ya uhalifu yanayotokea mkoani Tanga yamekuwa yakifanywa na watu ambao si wema na wamekuwa wakishirikiana na wanyeji wa maeneo hayo.

 

“Ukiangalia tukio hilo, baadhi ya watu waliohusika ni wakazi wa Mkoa wa Tanga, hivyo ninapenda kuiasa jamii kuachana na kufanya vitendo viovu kwani sisi kama Jeshi la Polisi hatutawavumilia, lazima tuwashughulikie ili kukomesha hali hiyo,” alisema.

Akizungumzia hali ya usalama katika mapango ya Amboni, alisema kwa sasa hali imekuwa shwari na Jeshi la Polisi linaendelea na majukumu yake kwa mujibu wa utaratibu.

“Hali ya usalama katika mapango ya Amboni kwa sasa yapo salama na tumefanya msako mkali sana ndani na nje, tena kwa kushirikiana na vyombo vyote vya dola. Tunaamini wananchi wataendelea kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi kwa kuwafichua watu ambao si wema.

“Tunawaomba wananchi wa Mkoa wa Tanga pindi wanapoona kuna mtu yupo katika eneo lao na hawamfahamu, ikiwa ni pamoja na kumtilia shaka, watoe taarifa kwetu nasi tutachukua hatua haraka,” alisema Kamanda Paul.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles