26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Sugu, Kubenea, Milya ‘Out’ bungeni

SUGUNa Kulwa Mzee, Dodoma

WABUNGE wengine watatu wa Chadema wamesimamishwa kuhudhuria vikao kumi vya Bunge na wengine vitano kwa makosa mbalimbali ya kukiuka kanuni za Bunge.

Wabunge walioadhibiwa jana ni Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi maarufu Sugu, Mbunge wa Simanjiro, James Ole Millya na Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea ambao kila mmoja alipewa adhabu yake kutokana na kosa alilotenda .

Mbilinyi

Mwenyekiti wa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, Kapteni mstaafu George Mkuchika, alitoa taarifa ya kamati kuhusu shauri la Mbilinyi la kuonyesha ishara ya matusi bungeni kwa kunyoosha juu kidole cha kati.

Alisema Juni 6,  mwaka huu katika kikao cha 37, mkutano wa tatu wa Bunge la 11 ,Mbilinyi aliombewa mwongozo na Mbunge wa Viti Maalum, Jackline Msongezi (CCM), kwamba alionesha kidole kimoja cha mkono wa kulia bungeni, kitendo ambacho ni ishara ya matusi.

Mbilinyi alifanya tukio hilo baada ya kuwasilisha hotuba yake kwa Wizara ya Habari ,Utamaduni ,Sanaa na Michezo kuhusu kuridhia mkataba wa Kimataifa wa Udhibiti wa matumizi ya dawa na mbinu za kuongeza nguvu michezoni ambapo akiwa anatoka alionesha kidole chake cha kati kwa juu akiwa amekunja vidole vingine vilivyobaki kama ishara ya matusi .

Alipohojiwa na kamati Mbilinyi alidai maana ya kuonesha kidole hicho na kukunja vingine ni lugha ya alama ambayo haina maelekezo ya moja kwa moja na kwamba kwa uelewa wake ishara hiyo siyo matusi.

Mkuchika alisema Mbilinyi anakiri kunyoosha kidole cha kati cha mkono wa kulia na kukiri kwake kunaungwa mkono na ushahidi wa video iliyochukuliwa siku hiyo na studio ya Bunge ambayo inaonesha dhahiri Mbilinyi akinyoosha kidole hicho.

Alisema kitendo hicho kinaonyesha Mbilinyi alidharau Mamlaka ya Spika aliyekuwa anaongoza kikao cha Bunge.

Kutokana na kosa hilo Mbilinyi amepewa adhabu ya kutohudhuria vikao 10 vya Bunge kutokana na kosa la kuonesha kidole bungeni  ambayo imeelezwa kuwa ni ishara ya matusi, adhabu ambayo ilitolewa na Spika na kuungwa mkono na wabunge wote.

Kubenea

Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson,  alisema ofisi yake ilipokea malalamiko kutoka kwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi kwamba Mei 10 mwaka huu wakati Kubenea akichangia Wizara ya Ulinzi alitoa tuhuma dhidi yake na kutaka uthibitisho wa tuhuma hizo kutoka kwa mbunge huyo.

Kubenea, alitoa tuhuma dhidi ya Jeshi la Wananchi Tanzania  kwamba limeingia mkataba wa ujenzi wa nyumba za makazi ya wananajeshi na Kampuni ya Heinang Industry Company Limited  yenye ekari 26,082 katika ploti namba 1,255 Masaki, Dar es Salaam,

Ilidaiwa kwamba kampuni hiyo itaendesha mradi huo kwa miaka 40 na baada ya hapo eneo hilo litarudishwa jeshini.

Dk. Tulia alisema Kubenea alieleza katika mkataba huo Dk.Mwinyi atajengewa nyumba yake binafsi katika kiwanja namba 2455/6 eneo la Upanga Dar es Salaam .

“Baada ya tuhuma hizo Dk.Mwinyi aliwasilisha barua ya malalamiko kwa Spika na kutaka kiti cha Spika kumtaka Kubenea athibitishe tuhuma hizo na endapo atashindwa achukuliwe hatua stahiki kwa mujibu wa kanuni za Bunge.

“Kutokana na malalamiko hayo nilitoa mwongozo bungeni Mei 13 mwaka huu ambapo Kubenea alitakiwa kufuta sehemu ya mchango wake uliolalamikiwa lakini alikataa kufuta kauli yake hivyo akatakiwa kuthibitisha kauli yake,”alisema Dk. Tulia.

Baada ya uchunguzi kwa kuwahoji Dk. Mwinyi na Kubenea Kamati ya Haki,Maadili na Madaraka ya Bunge ilijiridhisha kwamba Kubenea alisema uongo kwa kushindwa kuthibitisha madai yake.

Kutokana na makosa hayo Kubenea alisimamishwa kuhudhuria vikao vitano vya Bunge kutokana na kushindwa kuthibitisha madai aliyoyatoa dhidi ya Dk. Mwinyi.

Millya

Kwa upande wake Ole Millya amepata adhabu  ya kutohudhuria vikao vitano vya Bunge kutokana na kusema uongo dhidi ya Waziri wa Nchi,Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira,Vijana na Walemavu, Jenista Mhagama kwamba ana uhusiano wa kindugu na mmoja wa wabia wa Kampuni ya Sky Associate aliyodai ilinunua mradi wa madini ya Tanzanite One na kudai ilikuwa inanyanyasa wananchi.

Mhagama alisema ni uongo na kwamba hana undugu na mbia huyo na kumtaka Mbunge huyo kuthibitisha kauli yake

Alisema Millya alitoa uthibitisho wa kauli yake kwa maandishi na hatimaye uthibitisho huo ulipelekwa kwa Kamati ya Haki,Maadili na Madaraka ya Bunge ili ifanye uchunguzi na kujiridhisha juu ya madai hayo.

“Kamati ilikutana na kuwaita wahusika na ilibaini Millya alisema uongo kwani alishindwa kuthibitisha madai yake,”alisisitiza.

Dk.Tulia alisema kwa mujibu wa kanuni za Bunge,wabunge waliolalamikiwa walipaswa kupata nafasi ya kujitetea ili Bunge lijadili kuhusu adhabu zao.

Hata hivyo alisema kwa kuwa wabunge walioadhibiwa hawakuwepo bungeni, hivyo hakukuwa na haja ya wabunge kujadili adhabu hizo na badala yake aliwahoji wabunge ambao kwa pamoja walikubaliana na adhabu walizopewa wabunge hao.

Kutokana na uamuzi huo hadi sasa Bunge limewasimamisha wabunge 11 wa upinzani kwa makosa mbalimbali, ambapo yupo mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), Esther Bulaya (Bunda Mjini), John Heche (Tarime Vijiji), Tundu Lissu (Singida Mashariki), Halima Mdee (Kawe), Godbles Lema (Arusha Mjini) pamoja na Pauline Gekul ( Babati Mjini) wote wa Chadema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles