KAMPENI UNYWAJI SALAMA SBL KUCHANGIA KUOKOA BILIONI 800/- KWENYE AJALI

0
800
Ajali za barabarani husababisha hasara kutokana na uharibifu wa mali na nguvu kazi kutokana na ulemavu wa kudumu pamoja na vifo.
Ajali za barabarani husababisha hasara kutokana na uharibifu wa mali na nguvu kazi kutokana na ulemavu wa kudumu pamoja na vifo.

Na JUSTIN DAMIAN

WAKATI Tanzania ikiadhimisha wiki ya nenda kwa usalama barabarani, taarifa mbalimbali zimekuwa zikionyesha kuwa nchi inapoteza zaidi za shilingi bilioni 800 kwa mwaka kutokana na matukio mbalimbali yanayotokana na ajali za barabarani.

Hasara hii kubwa inatokana na uharibifu wa mali pamoja na nguvu kazi unaosababishwa na ajali za barabarani.

Kwa upande mwingine, ripoti mbali mbali za Shirika la Afya Duniani (WHO), zinaonyesha kuwa Tanzania ni moja kati ya nchi zenye idadi kubwa ya watu wanaopoteza maisha kwa ajili ya ajali za barabarani.

Januari mwaka huu aliyekuwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro, ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini alisema wakati akizungumza na waandishi wa habari kuwa, mwaka 2016 kulikuwa na ajali 5,219 ukilinganisha na ajali 3,710 zilizotokea mwaka 2015 ikiwa ni ongezeko la asilimia 35.

Maadhimisho ya wiki ya nenda kwa usalama barabarani mwaka huu yamechagizwa na kaulimbiu kutoka Jeshi la Polisi Kitengo cha Usalama Barabarani inayosema, ‘Zuia Ajali; Tii Sheria-Okoa Maisha’.

Ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya wiki hii ambayo hufanyika kila mwaka, shughuli mbalimbali zitafanyika kama vile utoaji wa elimu kwa umma juu ya sheria za usalama barabarani, namna sahihi ya kutumia vivuko vya waenda kwa mguu, kuheshimu sheria za barabarani kwa waendesha pikipiki pamoja na ukaguzi wa magari.

Jitihada mbalimbali ambazo zimekuwa zikifanyika na wadau mbalimbali ikiwamo Jeshi la Polisi zinalenga kufikia lengo la Umoja wa Mataifa linalosisitiza ‘Watu Salama’, ‘Vyombo vya Moto Salama’, ‘Barabara Salama’ na ‘Mwendo Salama’.

Malengo ya kupunguza ajali za barabarani yatakuwa vigumu kufikiwa ikiwa majukumu yataachiwa kikosi cha usalama barabarani peke yake pasipo ushirikiano wa wadau wengine na umma kwa ujumla.

Hata hivyo, wadau mbalimbali yakiwemo makampuni yamekuwa yakijitokeza kuiunga mkono Serikali kwenye suala hili. Moja kati ya wadau ambao wamekuwa wakitoa mchango wao ni Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) ambayo imekuwa ikitilia msisitizo kwenye suala la unywaji wa kiasi ambao ni moja kati ya vipaumbele vyake vikubwa.

Vipaumbele vyake vingine ni ‘Maji ya Uhai’ ambacho kinasisitiza upatikanaji wa maji safi na salama kwa jamii zinazozunguka viwanda vyake na kipaumbele kingine ni Utunzaji wa Mazingira na ‘Ujuzi kwa ajili ya Maisha’. Chini ya Kipaumbele cha Ujuzi kwa ajili ya Maisha, wanafunzi wanaofanya vizuri na ambao wanatoka kwenye familia masikini hupata ufadhili wa masomo kutoka SBL.

Ni hatua ya kijasiri kwa SBL kwa kuwa katika hali ya kawaida tungetarajia kampuni inayotengeneza na kuuza bia ikisisitiza wateja wake wanywe kwa wingi ili wafanye biashara zaidi na kupata faida nono. Kusema watu wanywe kwa kiasi ni kama kudhoofisha mkakati wao wakimasoko!

Akijibu kuhusiana na swala hilo, Mkurugenzi wa Mahusiano wa SBL, John Wanyancha, anasema: “Lengo letu ni kuwasisitiza wateja wetu kunywa kwa ustaarabu ili waweze kushiriki kwa ukamilifu shughuli za ujenzi wa taifa.” Wanafanya hivyo kwa sababu wanajali usalama wa wateja wao na kuwa nao kiendelevu.

Kwa mujibu wa Wanyancha, SBL imekuwa mstari wa mbele kusisitiza unywaji wa kistaarabu kupitia kampeni ya ‘Usinywe na Kuendesha gari’. Kampeni hiyo, inalenga kuwafikia vijana na watu wengine ikiwaelezea hatari ya kuendesha wakiwa wamelewa na kuwafanya wachukue hatua juu ya usalama wao wanapokuwa wakitumia vyombo vya moto.

Kampeni hii tayari imeshafanyika katika mikoa ya Arusha, Moshi na Dodoma ikihusisha uelimishaji kwa njia ya burudani, mijadala ambayo huwaleta pamoja wadau mbalimbali kama Polisi, madereva, Tanroads, Sumatra, wazazi, walimu, wanafunzi na umma kwa ujumla.

“Kampeni zetu zinalenga kuongeza uelewa kwa makundi mbalimbali kuwa ni vyema matumizi ya pombe yakawa ya kistaarabu ili waweze kukifurahia kinywaji chao bila matokeo mabaya,” anaeleza Wanyancha.

Kampeni hiyo, imepokelewa vyema na Serikali kama ambavyo alivyofanya Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama barabarani Mkoa wa Kilimanjaro, Peter Mizambwa ambaye wakati wa uzinduzi wa kampeni hizo zilizofanyika mjini Moshi mwaka 2015, aliipongeza SBL na kusema kampeni hiyo imekuja wakati sahihi ambapo Serikali imekuwa ikitafuta mwarobaini wa ajali za barabarani ambazo baadhi zimekuwa zikisababishwa na madereva walevi.

“Unywaji wa pombe kupindukia unahusishwa na ajali ambazo husababishwa na uendeshaji mbovu na kusababisha madhara kwa jamii. Athari za ajali haziishi tu kwa madereva bali hata kwa watu wengine ambao hujikuta wakipoteza maisha au kupata ulemavu na kujikuta wakishindwa kuchangia katika ujenzi wa taifa,” Mizambwa alinukuliwa na vyombo vya habari akisema.

Alisema pamoja na vifo, ajali za barabarani zimekuwa zikiongeza mzigo kwa sekta ya afya kutokana na matibabu na huduma wanazopatiwa manusura wa ajali ambazo zingeweza kuepukika.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here