25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

JWTZ kulinda amani mataifa ya nje

NA OLIVER OSWALD, DAR ES SALAAM

Dk Hussein Mwinyi
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi

WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi, amesema Serikali itaendelea kushirikiana na Jumuiya ya Kimataifa kutoa ushirikiano wa ulinzi na amani katika mataifa yenye matatizo ya amani.

Hayo aliyasema jijini Dar es Salaam jana, wakati akizindua Chuo cha Mafunzo ya Ulinzi na Amani, kilichojengwa kwa msaada wa Serikali ya Canada na kulenga kutoa mafunzo maalumu kwa maofisa wa Jeshi wa kulinda amani katika nchi zenye matatizo ya amani.

Alisema mafunzo yatakayotolewa na chuo hicho yatasaidia kupunguza madhara ya ushambuliwaji wa wanajeshi watakaoshiriki katika ulinzi wa kulinda amani katika mataifa hayo.

“Chuo hicho kitakuwa kikipokea wanafunzi watakaopata mafunzo haya kutoka nchi mbalimbali zilizopo katika Jumuiya ya Kimataifa, zikiwemo Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC) na Darfur – Sudan, ambazo tumekuwa tukishiriki kupeleka wanajeshi wetu wa kulinda amani na usalama katika mataifa yao.

“Mafunzo yatakayotolewa katika chuo hicho yatahusiana na mbinu zote za kiusalama na amani kwa wanajeshi wa kulinda amani, ambao watakuwa wakijifunza jinsi ya kukabiliana na hatari pindi wawapo katika majukumu yao.

“Kutokana na mafunzo watakayoyapata, tunaamini hata madhara ya wanajeshi wetu waliokuwa wakienda kulinda katika nchi hizo yatapungua, kwani watakuwa na ujuzi zaidi, ikiwa ni pamoja na mbinu za kujilinda dhidi ya adui,” alisema Dk. Mwinyi.

Alisema kutokana na uwepo wa chuo hicho nchini, amewataka wanajeshi wa kulinda amani kuitumia fursa hiyo katika kujiimarisha kimbinu na fikra ili waweze kupata uzoefu wa kutosha kabla ya kuingia eneo la vita.

Kwa upande wake, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Tanzania, Jenerali Davis Mwamunyange, alisema wakufunzi wa mafunzo yatakayotolewa watatoka hapa nchini pamoja na baadhi ya mataifa rafiki wanaoshirikiana kutoa ulinzi na amani katika mataifa hayo.

Alisema chuo hicho kimelenga kuanza kuchukua wanafunzi 70 watakaojifunza mafunzo hayo kulingana na aina ya masomo watakayochukua.

Alisema katika kuepusha mwingilianao baina ya wananchi na chuo hicho, Jeshi limekusudia kuanza ujenzi wa wigo utakaowatenganisha ili kuepusha migogoro ya mwingiliano wa ardhi.

“Nawaomba wote watakaopata nafasi ya kujifunza mafunzo haya wawe makini na kutumia fursa hii katika kujiimarisha kimbinu, kwani itawasaidia pindi watakapokuwa katika eneo hatarishi kuweza kuchukua uamuzi sahihi wa kukabiliana na adui,” alisema Jenerali Mwamunyange.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles