24.8 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

JUBILEE INAHOFIA KUSHINDWA OKTOBA 26?

RAIS Uhuru Kenyatta amekuwa akisisitiza kuwa uchaguzi wa marudio wa Oktoba 26 lazima ufanyike kama ulivyopangwa, licha ya kuwa Muungano wa upinzani wa National Super Alliance (NASA) unasisitiza hautashiriki iwapo Jubilee haitaachana na mapendekezo ya kubadili sheria za uchaguzi.

Kadhalika NASA wanataka maabadiliko ya  maofisa wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), ambao wanatuhumiwa kuchakachua matokeo ya uchaguzi wa Agosti 8, uliompa ushindi Kenyatta na ambao ulifutwa na mahakama.

Akizungumza wakati wa mkutano wa hadhara mjini Kakamega hivi karibuni mwishoni mwa mwezi uliopita, Kenyatta pamoja na Naibu wake William Ruto walitetea kama kitu cha lazima mapendekezo ya Jubilee ya kubadili sheria za uchaguzi.

Wawili hao wanasisitiza kuwa mageuzi hayo, ambayo yanapingwa hadi na jumuiya ya Kimataifa yamelenga kuziba mianya iliyoelezwa na Mahakama ya Juu wakati wa uchaguzi wa urais wa Agosti 8.

Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wa mambo wanasema wakati NASA ikilaumiwa kutoa visingizio vingi kukwamisha uchaguzi huo wa marudio ikihofia kushindwa, kundi la Ruto pia liko katika mkondo huo likihofia uwezekano wa kuanguka.

Jubilee wanawatuhumu NASA haitaki uchaguzi bali Serikali ya nusu mkate.

Iwe ni kweli au uongo, Chama cha Jubilee nacho kinadaiwa hakina uhakika wa kushinda uchaguzi huo na hivyo kufanya kila njia kuhakikisha kinabaki madarakani.

Suala la kutumia wingi wa wabunge wake kutaka kubadili sheria sasa kinaonwa kuwa ni sehemu ya njama za Jubilee, ikijua fika NASA haitakubali asilani na hivyo uchaguzi kukwama lawama zikiiendea NASA. Inadaiwa kuna mtandao ndani ya chama hicho unaojigamba kuibua sera mbovu kwa madhumuni hayo.

Unafanya hivyo ukijua mgombea urais wa upinzani wa NASA, Raila Odinga na washirika wake watapinga hatua zao hizo za sera tata.

Kwa mujibu ya vyanzo vya habari kupitia mkakati huo, wafuasi wa NASA watakapojitokeza kupinga sera hizo, wanamtandao huo nao wataibuka ghafla kudai pinga pinga hizo za NASA zinaaashiria kile wanachodai kila siku kuwa haiko tayari kwa uchaguzi.

Ndani ya Serikali ya Jubilee taharuki imeikumba, ikihofia uwezekano Odinga kuibuka mshindi katika marudio ya Oktoba 26, 2017.

Licha ya kuwa majukwaani wakati mwingine Kenyatta anaonekana kuzungumzia misimamo mikali kama inavyojionesha mwanzoni mwa makala haya, anaonekana kutobabaishwa na uwezekano wa kushindwa.

Wakati Kenyatta akiwa hivyo, hali ni tofauti kwa Naibu wake, William Ruto.

Wakati wawili wakitoa hotuba ya kwanza tangu Mahakama ya Juu ifute ushindi wao ile Septemba Mosi, Kenyatta alizungumza kwa hali ya ukomavu huku Ruto picha za video mtandaoni zikionekana kama mtu aliyechanganyikiwa anayezungumza zungumza peke yake.

Hali hiyo inaonesha hajajiandaa kuwa nje ya mamlaka wakati huu, ambao pia anaendesha harakati za kuwania urais mwaka 2022.

Wakati huu kuelekea Oktoba 26, Ruto anadaiwa kutumia mtandao wa Ikulu kuzuia uwezekano wowote wa wao kushindwa katika uchaguzi huo.

Lugha ya kampeni ya Ruto ina uwiano na wengi kuwa ile ya makali kupindukia na inayoonyesha ‘kubakia kwetu mamlakani kwa sasa na kisha kurithi majukumu ya urais ni suala la kufa kupona.’

Wadadisi wa masuala ya kisiasa wanasisitiza kuwa kuna taswira ambayo inajitokeza katika siasa za kuelekea kura hiyo ya marudio ambayo inamwangazia Rais Kenyatta kama asiyejali kupokezana mamlaka iwapo ataanguka kura, huku Ruto akionekana kuwa aliye mwingi wa tumbo joto ya kupoteza.

Ni katika hali hiyo ambapo Rais Kenyatta amekuwa akinukuliwa mara kwa mara akisisitiza kuwa “haijalishi ni nani atachaguliwa kuwa rais, bora tu amani idumu nchini na atakayekuwa chaguo la Wakenya aendeshe mbele Taifa la Kenya.”

Ingawa kuna wanaosisistiza kuwa msimamo huo wa Rais ni ule tu wa ujanja kisiasa wa kujiangazia kama mpenda amani na katika hali hiyo akilenga kukubalika kama mtu wa amani, Ruto hajanukuliwa kamwe akiwa na msimamo wa kushindwa.

Ruto anaangaziwa kama anayeongoza mkusanyiko wa maafisa wakuu katika utawala wa Jubilee ambao kwa udi na uvumba hawako tayari kuona wakishindwa katika kura hiyo na wanaweza wakafanya lolote liwezekanalo kubakia mamlakani.

Festus Wangwe ambaye ni mwanauchumi mchanganuzi pia wa masuala ya kisiasa anasema kuwa “hali iliyoko ndani ya mrengo huo wa Ruto ni ile ya kuhofia kuvunjwa kwa miaka 54 ya utawala wa mfumo wa unyakuzi ambao umeishia kurejesha Taifa hili nyuma huku mataifa mengine yakipaa zaidi katika ufanisi wa kiuchumi.”

Anasema kuwa Taifa hili lilikuwa sambamba kiuchumi miaka ya 1963 na mengine mengi duniani ambayo kwa leo ndiyo wababe kiuchumi duniani, Kenya ikiwa bado imekwama katika kuombea wananchi wake misaada ya chakula wakati wa kiangazi.

Anasema kuwa sera za Odinga haziwezi kamwe zikakubalika na washirika wa mtandao huo ambao umejengwa kisiasa na utapeli huo wa mali ya umma kiasi kwamba ‘waliokuwa wakijitafutia riziki kwa kuteka maji wakitumia uchukuzi wa punda miaka 10 iliyopita, leo hii ndio mabilionea wakubwa baada ya kupenyeza guu lao ndani ya utawala huo wa utapeli.”

Anasema kuwa wale walio na hofu zaidi ya kupoteza raha iwapo Odinga atatawazwa kuwa Rais kwa sasa ndio vivuli ambavyo vinasukuma uchaguzi uvurugike kwa kutumia hila na njama za kuleta sheria mpya za uchaguzi.

Kadhalika kuunga mkono maafisa wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), ambao wana dosari wabakie mamlakani na ikiwa hilo halitafua dafu, uchaguzi usifanyike ili Kenyatta abakie tu kuwahifadhi kama Rais.

Katika hali hiyo, wanasemwa kuwa ndio wanasukuma sera zisizofaa kutekelezwa kuthibiti uchaguzi huo wa marudio, wakijua fika Odinga na washirika wake watapinga na katika hali hiyo, wajitokeze mtaani kudai pingamizi za Nasa ni za kuvuruga uchaguzi usifanyike.

Hofu ni kuwa, Odinga anatazamiwa kuendesha operesheni ya kuwakung’uta walio ndani ya mitandao hiyo ya utapeli waliolowea katika tawala za vyama vya Kanu, PNU na sasa Jubilee.

“Si siri kuwa ukijipa imani ya mtandao huo wa utapeli katika utawala huwa unatuzwa kwa kupewa kazi ndani ya Ofisi ya Rais.

Vigogo hawa ndio wale ambao kwa sasa wanawika katika uongozi wa usalama hasa katika kaunti. Si jambo la kushangaza kuwa makamishna wa Kaunti, mawaziri na makatibu wao ndio wanaonekana kupishana katika kampeni hata kuliko Rais Kenyatta anayewania,” asema Wangwe.

Katika mtazamo huo, asema, machifu wamepewa amri ya kumpigia debe Rais Kenyatta mashinani.

Ndiyo maana Mbunge wa Kajiado ya Kati, Kanchori Memusi kwa sasa yuko vitani na Kamishna wa Kaunti ya Kajiado, Harsama Kello kwa madai kuwa ameamrisha machifu wa eneo hilo wachapie kampeni utawala wa Jubilee.

Gavana wa Kajiado, Joseph Ole Lenku akiwa ni mmoja ambaye amejengwa kisiasa hivi majuzi aliponyakuliwa kutoka Taasisi ya Elimu ya Utalii amemrukia Memusi akimwambia “koma kuhujumu kampeni za Jubilee hapa Kajiado.”

Harsame Kello naye anatilia mkazo hali halisi ya tumbo joto ndani ya mtandao huo kwa vile Odinga amekuwa akiangazia suala kuwa makamishna wa Kaunti kuwa hawako katika Katiba.

Kwa sababu hiyo atakapoingia Ikulu, wao ndio watakuwa wa kwanza kutemwa  na ikiwa hatafutilia mbali ofisi hizo, atateua walio na imani na utawala wake.

Ni hivi juzi tu Ofisa Usalama wa eneo la Pwani, Nelson Marwa aliutetea kwa nguvu utawala ambao Odinga daima husema ni wa ukabaila, ambapo katika eneo hilo amekuwa akimjenga kwa kiasi kikubwa Gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho.

Akiwa mwiba mkali dhidi ya utawala wa Serikali ya Jubilee, Joho alikuwa na mazoea hata ya kumkabili bila woga wawapo jukwaa moja na Rais Kenyatta.

Lakini Marwa amekuwa akifikiria anamlinda Rais kwa kuwa na mazoea ya kumweka gavana huyo kwa kifungo cha nyumbani na kuishia kumjenga badala ya kumbomoa.

Kwa mujibu wa Mbunge Peter Opondo Kaluma, “Rais Kenyatta si tatizo kubwa kwa kuwa amejiangazia kwa kiasi kikubwa kama asiye na nia ya kubakia mamlakani kwa mabavu tutakapomshinda Oktoba 26. Shida kubwa iko kwa Ofisi ya Naibu Rais Ruto na washirika wake wa ngazi za juu serikalini.”

Anasema kuwa “kuna taswira inayojitokeza ndani ya Serikali ya Jubilee ya kuhofia zaidi utawala wa Odinga ni Ruto kufuatia kashfa nyingi za kiutawala ambazo hudaiwa kutekelezwa na wandani wake na ambazo zinaweza kumweka gerezani katika kipindi cha wiki mbili baada ya Odinga kuapishwa kuwa Rais iwapo ataamua.”

Akiwa katika mahojiano na kituo cha redio cha Citizen, Kaluma alisema kuwa “hata zile pesa za Idara ya Huduma kwa Vijana (NYS) ambazo husemwa ziliporwa na Gavana wa sasa wa Kirinyaga, Anne Waiguru, kuna ushahidi kuwa alishirikiana na wandani wa Ruto.”

Ruto amekuwa akikanusha kuhusika na kashfa hiyo ya NYS ambapo mabilioni hudaiwa yalizama katika mifuko ya mtandao wa utapeli ndani ya Jubilee, Waiguru naye akisisitiza kuwa wa kuandamwa ni washirika wa karibu wa Ruto.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles