25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Jaji Mkuu atumbua mahakimu 11 kwa kukiuka maadili

6353827365_04c5dc8aff_b
Jaji Mkuu, Mohammed Othman Chande

JONAS MUSHI NA HADIA KHAMIS,DAR ES SALAAM

TUME ya Utumishi wa Mahakama imewafukuza kazi watumishi 34 wa mahakama mbalimbali nchini wakiwamo mahakimu 11 na maofisa 23 kutokana na makosa ya nidhamu, sheria na mzaha wa sheria.

Akizungumza na waandishi wa habari   Dar es Salaam jana baada ya kupokea taarifa ya utendaji wa Mahakama, Jaji Mkuu, Mohammed Othman Chande, alisema miongoni mwa mahakimu hao wapo mahakimu wakazi, wafawidhi na wa mahakama za mwanzo.

Alisema mahakimu hao wamechukuliwa hatua kwa makosa   mbalimbali ya  nidhamu ikiwamo kutumia vibaya muhuri wa mahakama.

Makosa mengine ni kumsaidia mtu kufungua kesi moja kwenye mahakama mbili tofauti kinyume na maadili na hakimu kufungua kesi ya mirathi bila kuwapo hati ya kifo.

“Kikao cha Tume ya Utumishi wa Mahakama cha Agosti 18 mwaka huu ndicho kilichoamua kuwafukuza kazi watumishi hawa baada ya kuwahoji na kujiridhisha kwamba wametenda makosa ya nidhamu ambayo yanatia doa mahakama,” alisema Jaji Chande.

Alisema hatua hiyo haitaathiri utendaji wa mahakama kwa vile idadi ya waliofukuzwa ni ndogo ikilinganishwa na watumishi wote wa mahakama.

“Mahakama ina watumishi 6,406, hawa 34 waliofukuzwa ni sawa na asilimia 0.005 ya watumishi wote hivyo hakuna athari yoyote,” alisema Chande.

Alisema pia Tume hiyo inatafakari hatma ya mahakimu 30 walioshtakiwa mahakamani kwa tuhuma za rushwa na kushinda kesi huku wengine 32 walioshtakiwa kwa tuhuma za jinai na kushinda wanatarajiwa kufikishwa mbele ya Kamati ya Maadili na Nidhamu ya Mahakama.

Licha ya watumishi hao kushinda kesi mahakamani watafunguliwa kesi za  nidhamu kwa sababu katika kushtakiwa kwao kuna masuala yaliyojitokeza ambayo yanaitia doa mahakama, alisema.

Akizungumzia ripoti za utendaji wa Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa, Jaji Chande alisema katika historia ya mahakama hiyo imeweza kumaliza kesi za uchaguzi kwa muda mfupi.

Hata hivyo, alisema bado kuna uhaba wa majaji na kwamba baada ya kutangaza nafasi za ujaji watu 145 wameomba kazi hiyo.

Akizungumzia kuhusu mahakama ya mafisadi, Jaji Chande alisema  kanuni za uendeshaji wa mahakama hiyo zipo tayari na zinatarajiwa kuchapishwa wiki ijayo.

“Kanuni hizi ndizo zinazoeleza utaratibu wa ufunguaji wa kesi, jinsi ya kufungua kesi na utaratibu wa kushughulikia kesi,” alisema Jaji Chande.

Akisoma ripoti ya Mahakama Kuu mbele ya Jaji Mkuu, Msajili wa Mahakama Kuu, Ilvin Mugeta, alisema tangu Uchaguzi Mkuu wa 2015 umalizike zimekwisha kufunguliwa kesi 247 za ubunge na udiwani.

Alisema kati hizo, kesi 53 ni za ubunge na 48 zimeshafanyiwa uamuzi huku 194 zikiwa ni kesi za udiwani kati yake 186 zikiwa zimekwisha kufanyiwa uamuzi.

Chande alisema inatarajiwa kesi zilizobaki ambazo tano ni za ubunge na nane za udiwani, zitamalizika kufikia  Oktoba mwaka huu.

Alisema kwa vile  kesi za uchaguzi zilipewa kipaumbele, zimeathiri umalizaji wa mashauri mengine yasiyo ya uchaguzi.

Hata hivyo, alisema kwa kipindi cha Januari hadi Agosti mwaka huu wastani wa uwezo wa umalizikaji wa kesi kuanzia Mahakama Kuu hadi mahakama za mwanzo, ni asilimia 100.

“Kesi zilizobaki mwaka jana zilikuwa 99,448, zilizosajiliwa ni 1,67,865 na zilizosikilizwa ni 197,794 hivyo wastani wa uwezo wa umalizikaji wa kesi ni asilimia 100,” alisema Mugeta.

Naye Msajili wa Mahakama ya Rufani, John Kahyoza, alisema kwa mahakama hiyo changamoto kubwa ni upungufu wa majaji.

Alisema mahakama hiyo ina majaji 16 ambao hufanya kazi kwa jopo la majaji watatu hivyo kuna majopo matano.

Alisema uwezo wa kila jopo ni kumaliza rufani 147 kwa mwaka lakini wingi wa rufani zilizopo ni 475 kwa jopo moja, idadi ambayo ni kubwa.

“Idadi ya rufani 475 kwa jopo moja ni kubwa na haiwezekani  kumalizika kwa mwaka hivyo kuna uhitaji mkubwa wa majaji,” alisema Kahyoza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles