23.1 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 8, 2024

Contact us: [email protected]

Gwajima: Huwezi kutenganisha siasa na dini

Pg 2NA ELIZABETH MJATTA, DAR ES SALAAM
MCHUNGAJI kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, amesema viongozi wa dini hawawezi kujitenga na siasa kama inavyoelezwa na baadhi ya watu katika jamii.
Gwajima alitoa kauli hiyo wakati akitunukiwa tuzo ya heshima ya udaktari kutoka katika Chuo Kikuu cha Biblia na Theolojia cha Omega Global (OGU) cha Afrika Kusini, jijini Dar es Salaam juzi.
Alisema kumekuwa na dhana kwamba viongozi wa dini kujihusisha na siasa ni kwenda kinyume na kazi wanayoifanya.
“Huwezi kutenganisha siasa na dini, kwa sababu siasa inahusu watu na dini inahusu watu, kwahiyo ni vitu vinavyotegemeana, watu wanaosema kwamba viongozi wa dini wakijihusisha na siasa ni kupotoka si kweli,” alisema Gwajima.
Wengine waliotunukiwa tuzo hizo za heshima pamoja na Gwajima ni Mchungaji Gospel Odome (Londoni), Mchungaji Alexander Mugunda (Kigoma), Mchungaji Brown Mwakipesile (Dodoma), Mchungaji George Madaha (Shinyanga), Mchungaji Stephen Masanga (Dodoma) na Mchungaji Praygod Mgonja.
Akikabidhi tuzo hizo, mkuu wa chuo hicho kutoka Afrika Kusini, Profesa Vusumuzi Nehemia, alisema wameona na kutambua mchango mkubwa unaofanywa na viongozi hao katika jamii.
“Chuo hiki kimeona na kutambua mchango wa viongozi hawa kwamba wamefanya mambo makubwa bila kuwa na elimu kubwa, hii ni heshima kubwa kwao, ukiangalia hapa kuna wazee wametumikia jamii katika utumishi uliotukuka kwa miaka arobaini, hii ni heshima kubwa kwao,” alisema Profesa Vuzumuzi.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Chuo cha OGU nchini Tanzania, Dk. Damas Mukasa, alisema heshima iliyotolewa na chuo hicho kwa Watanzania ni fursa tosha ya kuendelea kushirikiana na chuo hicho katika mambo mengi ya kielimu.
“Hii ni fursa kubwa na ya kipekee, ndugu zetu hawa wako tayari kuendelea kushirikiana na sisi, na kwa sababu tumeshakuwa wawakilishi wengi sasa hivi, tutakaa kupanga mipango ikiwezekana tuanzishe chuo kikuu hapa nchini,” alisema Dk. Mukasa.
Alisema elimu ndiyo kitu pekee kitakachomwokoa mtu katika mambo mengi ikiwamo haki yake ya kikatiba.
“Ni vyema tukaongeza elimu ili tuweze kupata maarifa zaidi, rai yangu kwa Watanzania wenzangu hususan katika kipindi hiki tunachoelekea katika Uchaguzi Mkuu, tusibaki nyuma, tujiandikishe katika daftari la kudumu, lakini pia tuipigie kura rasimu ya Katiba Inayopendekezwa,” alisema Dk. Mukasa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles