23.6 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Shein ataka nchi za SADC kushirikiana zaidi

Mwandishi wetu -Zanzibar 

RAIS wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, amesisitiza umuhimu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kushirikiana ili kuzipatia ufumbuzi changamoto zinazozikabili.

Dk. Shein alisema hayo alipokutana na Katibu Mtendaji wa SADC, Dk. Stergomena Tax aliyemtembelea Ikulu.

Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa na Ikulu ya Zanzibar, Dk. Shein alisema nchi wanachama wa SADC zinakabiliwa na changamoto mbalimbali zinazofanana, zikiwamo za majanga pamoja na za kiuchumi, hivyo ni vyema zikashirikiana kuzipatia ufumbuzi.

Akigusia suala la majanga, Dk. Shein alisema ni changamoto inayoikabili dunia nzima, ambayo hutofautiana kulingana na mazingira ya kimaeneo.

Alisema kufanyika kwa mkutano wa kwanza wa kamati ya mawaziri wenye dhamana ya menejimenti ya maafa kwa nchi wanachama wa SADC, ni mwanzo mzuri katika mwelekeo wa kuzipatia ufumbuzi baadhi ya changamoto hizo.

Dk. Shein alisema Zanzibar kwa upande wake imeanza kulitafutia ufumbuzi tatizo la kutuwama kwa maji ambalo husababisha majanga (hususan katika maeneo ya ng’ambo) kwa kujenga mitaro mikubwa inayopeleka maji moja kwa moja baharini.

Aidha, Dk. Shein alisema kuna haja kwa nchi wanachama wa SADC kutafakari namna gani zitakavyoshirikiana na kusaidiana katika dhana ya kuimarisha uchumi wa nchi zao, kwa kubadilishana uzoefu pamoja na upatikanaji wa mafunzo.

Alisema kuna umuhimu wa nchi hizo kubadilishana bidhaa, hususan zitokanazo na kilimo kwa njia ya kuuziana, ikiwa ni hatua itakayopunguza gharama.

Aidha, Dk. Shein alibainisha dhamira ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania na ile ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kusimamia demokrasia nchini kwa kuzingatia sheria na katiba za nchi.

Mapema, Dk. Tax, aliishukuru Serikali kwa kukubali kuandaa mkutano huo muhimu, hatua aliyosema inatokana na kutambua mchango mkubwa wa Tanzania katika maendeleo na mustakabali wa jumuiya hiyo.

Alisema hali ya ulinzi na usalama kwa nchi wanachama wa SADC ni nzuri mbali na kuwapo kwa matukio mbalimbali yanayojiri kabla na baada ya uchaguzi. 

Alishauri kutiliwa mkazo suala la upatikanaji ajira kwa vijana katika nchi wanachama ili kuondokana na kadhia mbalimbali zinazojitokeza.

Aidha, Dk, Tax aliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Dk. Shein kwa maendeleo makubwa ya kiuchumi na kijamii iliyofikia, hivyo akabainisha azma ya SADC ya kuunga mkono juhudi hizo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles