23.4 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

Corona yawarudisha wachezaji Yanga majumbani

THERESIA GASPER – DAR ES SALAAM

BAADA ya Serikali kusitisha shughuli za michezo kwa siku 30 kuanzia juzi, Yanga imewapa mapumziko wachezaji wake, lakini kocha wa timu hiyo Luc Eymael amewapa kila mmoja program maalum  ya kufanya kipindi hicho.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa juzi akihutubia Taifa kupitia Televisheni ya Taifa(TBC)alitangaza uamuzi wa serikali kupiga marufuku kwa siku 30, shughuli mbalimbali zinazosababisha mikusanyiko ya watu ikiwemo michezo, ikiwa ni tahadhari ya kuepuka kusambaa kwa virusi vinavyosababisha ugonjwa wa corona.

Ugonjwa wa corona ambayo ambao unaambukizwa kwa hewa pale mtu anapopiga chafya au kukohoa pamoja na kugusana, ulianza China kabla ya kusambaa maeneo mengine duniani na mpaka sasa umesababisha vifo vya maelfu ya watu.

Jumanne wiki hii, Waziri wa Afya, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alitangaza kubainika kwa mgonjwa wa kwanza mwenye maambulizi ya corona.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Hassan Bumbuli, alisema baada ya agizo hilo la serikali na kisha Shirikisho la Soka Tanzania(TFF) kusitisha Ligi Kuu Tanzania Bara, Ligi Daraja la Kwanza na Ligi Daraja la Pili, wameamua kuwapa mapumziko wachezaji wao.

“Tayari tumeshawaruhusu wachezaji wetu kwenda mapumziko,  hata hivyo Kocha Mkuu ametoa program maalumu kwa kila mchezaji ambayo atatakiwa kuifanya akiwa mapumziko,” alisema.

Alisema baada ya katazo la serikali kumalizika,  benchi lao la ufundi chini ya Eymael litafuatilia kama maagizo waliyoyatoa yamefanyiwa kazi.

Bumbuli alisema kwa wachezaji wa kimataifa, wamewashauri waendelee kuwepo hapa nchini badala ya kwenda makwao ili kuepuka hatari ya kupata maambukizi ya corona.

“Tumewashauri wachezaji wetu wakimataifa waendelee kuwa hapa nchini kwa kipindi hiki cha mwezi mmoja kwa usalama zaidi kwani huwezi  kujua huko watakapoenda maambukizi yapo kwa kiasi gani,” alisema.

Alisema wakirejea wataendelea na kasi yao kuhakikisha wanafanya vizuri katika mechi zilizosalia za Ligi Kuu, ili kumalize msimu wakiwa kwenye moja kati ya nafasi mbili za juu.

Yanga inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu, ikijikusanyia pointi 51 katika michezo 21, iliyokwishacheza, ikishinda14,  sare tisa na kupoteza mitatu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles