24.8 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

BUTIKU: MWALIMU NYERERE HAKUAMINI VIWANDA NI MAENDELEO

Na EVANS MAGEGE

NI miaka 18 imepita tangu Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, afariki dunia mwaka 1999.

Kilele cha maadhimisho kimefanyika jana visiwani Zanzibar, huku Rais John Magufuli akiwa mgeni rasmi.

Kumekuwapo na utamaduni wa kufanyika midahalo ya kujadili mambo kadhaa wa kadha, hususan falsafa alizozitumia Mwalimu Nyerere wakati wa utawala wake.

Mara nyingi midahalo hiyo imekuwa ikiitishwa wiki moja kuelekea kuadhimisha siku ya kifo chake kila ifikapo Oktoba 14 ya kila mwaka.

Jumatano wiki hii, Kibweta cha Mwalimu Nyerere, ambacho huandaliwa kila mwaka na Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, kiliitisha kongamano la kitaifa kujadili dhamira ya Mwalimu katika kujenga uchumi imara wa nchi.

Mada kuu ya kongamano hilo  ilikuwa; “Mtazamo wa Mwalimu Nyerere katika Uchumi wa Viwanda na Maendeleo ya Jamii”.

Joseph Butiku, ambaye ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, alikuwa miongoni mwa wachokoza mada, amejikita zaidi kuelezea uongozi bora katika ustawi wa Uchumi wa Viwanda.

Katika hoja hiyo, analenga kuwajengea picha wananchi juu ya uhusiano uliopo kati ya msimamo wa Mwalimu Nyerere kuhusu uchumi, viwanda na maendeleo ya jamii katika mtazamo wa uongozi bora kwenye ustawi wa Uchumi wa Viwanda.

Utawala wa Awamu ya Tano chini ya Rais Dk Magufuli, umejielekeza zaidi katika ujenzi wa viwanda, lengo likiwa ni kupaisha uchumi na maisha ya Watanzania.

Katika makala haya, Butiku anaelezea kuwa, Mwalimu Nyerere aliamini katika usawa, ikiwa ni msingi wa kujenga uchumi wenye kuleta maendeleo kwa kila Mtanzania.

Aidha, anasema Mwalimu Nyerere pia aliamini uongozi bora ni ule unaotambua na kuamini katika falsafa na msingi mkuu wa usawa, kwa maana ya kuweka maisha ya kila siku ya Mtanzania kwa umoja.

Butiku anasema Mwalimu Nyerere kama kiongozi bora wa Tanzania na duniani, hakuchukia viwanda kutokana na uwekezaji wa wageni au wazalendo, bali alitambua viwanda vikubwa kama vile vya dhahabu, gesi, mafuta, almasi, mkaa na vyuma, kwamba  huhitaji fedha nyingi ambazo nchi haina.

“Aliiona hatari ya kuwa na viwanda vingi vikubwa vinavyotegemea fedha za wawekezaji wengi kutoka nchi za nje na fedha zisizo za Watanzania kuwa fedha hizo zinaweza kutufanya Watanzania kuwa watumwa wa hao wenye fedha nyingi na mantiki yake ni kutawaliwa tena.

“Mwalimu Nyerere alipenda na alitaka Tanzania iwe nchi ya viwanda. Aliamini kwamba, viwanda na uchumi wa viwanda, ni kielelezo bora cha watu walioendelea.

“Lakini hakuamini kwamba viwanda ndiyo maendeleo, bali aliamini kwamba, viwanda ni matokeo ya watu walioendelea kwa kuwa na uwezo mkubwa wa elimu ya ufahamu, maarifa na ufundi,” anasema Butiku.

Anasema Mwalimu Nyerere aliamini kwamba, nchi inaweza ikawa na viwanda vingi vikubwa, lakini isiwe na maendeleo ya watu wa nchi hiyo.

Kwa muktadha huo, Butiku anasema maendeleo ya viwanda yanatokana na uongozi bora unaoleta maendeleo ya watu wenye uwezo wa kujiendeleza.

Alitolea mfano kuwa mashamba makubwa yanayopata kulimwa hapa nchini hayajawahi kuwaletea maendeleo watu husika, badala yake yamewanufaisha watu wengine walioendelea.

Kutokana na hoja hiyo, Butiku anaeleza kuwa, vinaweza kuwapo viwanda vya watu na makampuni ya nchi za kigeni na vikaajiri watu wazalendo wachache au wengi, lakini wakifanya kazi kama vibarua au wataalamu wasioiva au wenye maarifa duni ya kazi.

Kwa tahadhari ya mazingira hayo, anasema katika malengo ya Azimio la Arusha, Mwalimu Nyerere alidiriki kusema kuwa amekazania viwanda vya kati ili kumjali mkulima, kwa sababu maendeleo ya watu yataletwa na kilimo.

Butiku anasema lengo la viwanda ni nyenzo muhimu ya maendeleo ya wananchi. Lakini viwanda havitawaletea wananchi maendeleo bila wananchi wenyewe au wengi wao kuwa wameendelea kwa njia ya kujitegemea.

Butiku anasema Azimio la Arusha katika kipengele cha kujitegemea, Mwalimu Nyerere ametoa maelezo marefu sana ya kujenga hoja ya kuainisha uwezo wa nchi wa kujenga viwanda na uwezo wa wananchi wa kuchangia malighafi ya viwanda, kwa maana ya kutokana na ushiriki wao katika kilimo, ambacho ndicho kiwanda mama kwa wananchi walio wengi.

Kwamba Mwalimu Nyerere aliamini pia kilimo ni kiwanda kinachoweza kuajiri wananchi wengi na kuwawezesha kuongeza mapato kwa kuuza mazao yao.

Anasema kwa ujumla huo ndio ulikuwa mtazamo wa Mwalimu Nyerere kuhusu viwanda.

Butiku hakuishia hapo, anasema Mwalimu Nyerere aliamini kwamba ili viwanda viendelee na kuleta tija kwa wananchi, ni lazima wananchi wajengewe uwezo; wapate elimu yenye ubora ya ufahamu, elimu yenye ubora ya maarifa kwa maana ya ufundi, ubunifu, sayansi na teknolojia ya kisasa.

Sambamba na hayo, Butiku anaeleza kuwa, elimu itolewe ikiwa na lengo la kuwajengea uwezo wananchi, hata kama kujitegemea ni kwa viwango tofauti na katika ngazi za kuanzia elimu ya awali, hadi ya juu lazima itolewe kwa nadharia na ujuzi.

Butiku anakwenda mbali kuijenga hoja hiyo ya Mwalimu kwa kutumia maelezo yaliyopo katika Azimio la Arusha juu ya umuhimu wa kuandaa viongozi.

Anasema katika suala la kukazania viwanda, Mwalimu Nyerere aliandika kwamba, kwa sababu ya kutilia mkazo fedha; “Tumefanya kosa kubwa la pili, tumekazania mno viwanda, kama vile tulivyosema bila fedha hakuna maendeleo na kama twasema pia viwanda ndiyo maendeleo.

“Bila viwanda hakuna maendeleo. Bila fedha hakuna maendeleo, ama twasema pia viwanda ndiyo maendeleo. Bila viwanda hakuna maendeleo. Hivi ni kweli siku tutakapokuwa na fedha nyingi tutaweza kusema kwamba tumeendelea! Kadhalika siku tutakapokuwa na viwanda tuna haki ya kusema kuwa tumeendelea,” anasema Butiku kwa kumnukuu Mwalimu Nyerere.

Aidha, anaeleza kuwa, Mwalimu Nyerere alipata kusema kuwa, maendeleo yatakuwa yametuwezesha kupata viwanda, lakini kosa tunalofanya ni kudhani kuwa maendeleo yetu yataanza kwa viwanda.

Butiku anasema ni kosa kuwa na fikira hizo, kwa maana hatuna uwezo wa kuanzisha viwanda vingi vya kisasa katika nchi yetu.

Katika nukuu nyingine ya Mwalimu Nyerere aliliona hilo na ndiyo maana alisema: “Hatuna fedha zinazohitajiwa na hatuna ufundi unaohitajiwa. Haitoshi kusema kuwa tutakopa fedha za kutosha na kuazima mafundi wa kutosha kutuanzishia viwanda hivyo tunavyotaka.

“Siasa ya kualika msururu wa mabepari kuja kuhodhi viwanda katika nchi yetu ingefanikiwa kutupatia viwanda vyote tunavyovitaka, basi ingefanikiwa pia kuzuia maendeleo ya Ujamaa. Ila labda tuwe tunaamini kwamba bila kuujenga ubepari kwanza hatuwezi kuujenga Ujamaa.” Anamnukuu Mwalimu Nyerere.

Anasema kwamba, Mwalimu Nyerere alihimiza kumjadili zaidi mkulima vijijini ili anufaike na viwanda.

Anasema kwamba, Mwalimu alitambua kwamba, hatuwezi kupata fedha za kutosha kuleta maendeleo katika kila kijiji na ambayo yatamfaa kila mwananchi na alijua kabisa hawezi kujenga kiwanda kila kijiji ili kisaidie kuleta maendeleo ya fedha na viwanda katika kila kijiji.

“Kwa ajili hiyo basi, fedha zetu huzitumia zaidi katika miji na viwanda vyetu, pia hujengwa katika miji, na zaidi ya fedha hizi huwa mikopo. Japo zijenge shule, hospitali, majumba au viwanda, ni fedha za mikopo na hatimaye lazima zilipwe. Lakini ni dhahiri kwamba haziwezi kulipwa kwa fedha zinazotokana na maendeleo ya viwanda.

“Hazina budi zilipwe kwa fedha tunazopata kutokana na vitu tulivyouza katika nchi za nje. Kutokana na viwanda vyetu hatuuzi, na kwa muda mefu sana hatujauza vitu vingi katika nchi za nje. Viwanda vyetu zaidi ni vya kutusaidia kupata vitu hapa hapa ambavyo mpaka sasa tunaviagiza kutoka nchi za nje.” Anamnukuu Mwalimu.

Kwa hoja hiyo hiyo, Butiku anamkariri Mwalimu Nyerere akisema kwamba, itapita miaka mingi kabla ya kuweza kuuza katika nchi za nje vitu vinavyotokana na viwanda vyetu.

Kwamba fedha tutakazotumia kulipa madeni haya ya mikopo ya fedha kwa maendeleo na viwanda mijini hazitatoka mjini na wala havitatokana na viwanda. Zitatoka wapi basi? Butiku alijibu kuwa, zitatoka vijijini na zitatokana na kilimo.

Butiku anatoa jibu hilo kwa kuamini maendeleo ya Watanzania yataletwa kwa kilimo, kwa sababu ndicho kinaajiri watu wengi, hasa maeneo ya vijijini.

Anasema kwamba, sehemu kubwa ya eneo la Tanzania ni ardhi yenye rutuba na mvua za kutosha na kwamba wakazi wengi wako huko. Nchi yetu inaweza kutoa mazao ya aina mbalimbali ambayo tunayahitaji kwa chakula na kwa fedha na kwa viwanda pia.

Anasema ardhi ni nguzo ya maendeleo ya watu, kwa mfano uchumi wa Tanzania unategemea kilimo kuendelea, kwa mantiki hiyo, ardhi ni ufunguo wa maisha ya binadamu, kwa hiyo Watanzania wote waitumie ardhi kama rasilimali yao kwa maendeleo ya baadaye.

Hata hivyo, Butiku anasema Tanzania ilishindwa kudumisha viwanda vingi na mashirika mengi kwa sababu viongozi na watendaji wakuu wote hawakufundishwa uongozi bora.

Anaongeza kuwa, uongozi unazo sura nyingi, lakini sura ya muhimu zaidi katika zote ni ile ya ubora na uwezo wa fikra na mawazo yanayojidhihirisha miongoni mwa watu wengine.

Pamoja na hilo, Butiku anaeleza kuwa, ubora wa kufikiri kwa mtiririko sahihi wa mawazo, uwezo wa kujieleza, na uwezo wa kuelewa na kutenda vema kazi zilizopangwa ni sifa pia za uongozi bora.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles