23.6 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

Buriani Mbunge na mwamuzi wa kimataifa

majaliwa

Na RAMADHAN HASSAN- DODOMA

FAMILIA ya michezo imepata pigo baada ya juzi kuondokewa na mwanamichezo na aliyekuwa mwamuzi wa kimataifa nchini, Hafidh Ally Tahir.

Tahir, ambaye alikuwa ni Mbunge wa Jimbo la Dimani (CCM), alifariki juzi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, saa 9 alfajiri alipokwenda kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

Kwa mujibu wa Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Dk. James Kiologwe, marehemu alikuwa akisumbuliwa na shinikizo la damu.

Juzi Tahir alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Tawi la Wabunge wa Yanga, mjini Dodoma chini ya uenyekiti wa Venance Mwamoto, pia marehemu alikuwa ni kocha msaidizi wa timu ya Bunge Sport Club.

Pia alikuwa anasifika kwa kuchezesha michezo mingi ya kimataifa pamoja na ile ya watani wa jadi, Simba na Yanga.

Tahir kila siku asubuhi kama kuna vikao vya Bunge alikuwa akionekana katika Uwanja wa Jamhuri, Dodoma, akifanya mazoezi na wabunge wenzake, lakini juzi katika uwanja huo hali ilibadilika na kuwa simanzi kutokana na taarifa za kifo chake.

Katika siku za hivi karibuni, Tahir alifanya mahojiano na gazeti hili akiwachambua waamuzi wa Tanzania pamoja na changamoto za mchezo huo.

Katika mahojiano hayo, Tahir alisimulia mchezo wa Simba na Yanga ambao hatausahau katika maisha yake na jinsi alivyokuwa akichezesha mechi ya watani wa jadi nchini Misri ya Zamaleck na Al Ahly.

“Kujitambua, kufanya mazoezi pamoja na kukwepa rushwa ndiyo sababu iliyonifanya nichezeshe michezo mingi nchini na nje ya Tanzania, kwani kila mtu aliniamini na alijua nitaweza kutafsiri sheria vizuri,” anasema.

Anasema sababu ya kuaminiwa na kupewa michezo mikubwa ni kutokana na kukataa rushwa kutoka kwa viongozi wa timu mbalimbali wakati akichezesha mpira.

Anasema ili uwe mwamuzi bora ni lazima uwe mwadilifu, kwani waamuzi wengi kwa sasa wanakuwa na tamaa ya kufanikiwa kimaisha kwa kuchukua fedha.

“Hakuna kitu kizuri katika maisha kama kuwa mwadilifu, mimi uadilifu ndio ulionisaidia, sina ushahidi kwa waamuzi wa sasa hivi kama wanachukua fedha, lakini nakwambia hiyo ndiyo sababu ya kutopata waamuzi bora.

“Hizi mnazoziita timu kubwa zilikuwa zikinifuata na kuniwekea fungu mezani, lakini mimi nilikuwa naipenda fani yangu, nilikuwa nakataa na hiyo ilinisaidia kuzidi kuaminika katika jamii na katika hizo timu,” anasema.

 MWAMUZI HAWEZI KUPIMWA KWA COOPER TEST

Anasema mwamuzi bora hawezi kupimwa kwa ‘cooper test’, bali kutokana na anavyochezesha uwanjani.

Anasema Chama cha Waamuzi Tanzania (FRAT), kinatakiwa kibadilike kwa kuwapima waamuzi uwanjani na kuachana na kuweka undugu katika kutoa beji za Fifa pamoja na kuwapandisha waamuzi madaraja.

“Unakuta mwamuzi katika ‘cooper test’ anakimbia kweli, mpe filimbi sasa unaweza ukalia, waamuzi wanapatikana uwanjani jinsi anavyokuwa na maamuzi ya haraka kwa kufuata sheria zote za mchezo,” anasema.

Anasema ili mwamuzi awe bora uwanjani ni lazima achezeshe akiwa mita 10 nyuma ya mpira ili aweze kuona kila tukio linalotokea uwanjani pamoja na wachezaji jinsi wanavyogombania mpira.

“Hebu angalia sasa hivi waamuzi wakichezesha wanakuwa mbali na mpira, sasa tukio utalionaje, unatakiwa uwe mita 10 na mpira, hapo utaona kila kitu,’’ anasema.

Anasema sasa hivi kuna mwamuzi mmoja tu anayejitahidi, Israel Nkongo.

 MECHI AMBAYO HATAISAHAU

Anasema mechi ambayo hataisahau ni kati ya timu ya Yanga na Simba mwaka 1989,  ambapo Simba waligoma kurudi uwanjani na mchezo kuisha hapo.

“Ile mechi nilichezesha mimi, ipo kichwani mwangu hadi leo, Simba waligoma kurudi uwanjani ila matokeo nimesahau, ni jambo ambalo lilinisikitisha na kunihuzunisha, wengine wakasema mimi Yanga damu.

“Lakini nakumbuka katika mechi nyingine ya Simba na Yanga nilimpa kadi nyekundu beki wa kushoto wa Yanga, Kenneth Mkapa, wakasema tena mimi Simba, lakini ilikuwa ni misimamo yangu ya kufuata haki na kanuni,’’ anasema.

ASIMULIA ZAMALEK NA AL AHLY

Anasema alichaguliwa mara nyingi kuchezesha Zamalek na Al Ahly kutokana na kuchezesha vizuri.

Anasema kutokana na kutowaamini waamuzi wa Misri, chama cha soka cha nchi hiyo hadi leo kina utaratibu wa kutoa waamuzi nje ya nchi ili kuepuka waamuzi kuipendelea timu fulani.

“Nakumbuka nilikuwa Misri katika masomo yangu, unajua mimi ni mwandishi, nimesomea masuala ya redio Cairo, hivyo nilivyofika kule niliripoti katika Makao Makuu ya CAF wakanipa mechi ya Al Ahly na Zamaleck.

“Ile ndiyo mechi yenye mambo mengi kuliko zote duniani, watu wanakufuata na fedha nyingi ili timu yao ipate ushindi, lakini mimi nilikuwa nabaki na msimamo wangu tu na uadilifu wangu,” anasema.

Anasema hakuna mwamuzi kutoka Afrika Mashariki na Kati ambaye amewahi kuchezesha Fainali za Mataifa ya Afrika na Kombe la Dunia kwa vijana mwaka 1986 nchini Scotland.

“Unajua CAF na FIFA ina waamuzi wake kulingana na daraja, mimi nilikuwa daraja la kuchezesha mzunguko wa pili, robo fainali na nusu fainali, sababu kubwa ikiwa ni uadilifu wangu, kutafsiri sheria pamoja na kwenda na kasi uwanjani,” anasema.

Anasema mwamuzi bora ni aliyewahi kucheza mpira katika maisha yake.

“Mimi nimecheza mpira African Temeke ya Dar es Salaam mwaka 1967 hadi 1971, kisha nikajiunga na Miembeni mwaka 1972 hadi 1978 na baadaye timu ya Taifa.

 

MICHEZO ILIYOMBEBA KISIASA

Anasema kutokana na kufanya vizuri katika fani ya uamuzi, ndiko kulikomfanya aweze kujulikana kisiasa na kushinda ubunge katika Jimbo la Dimani, Zanzibar.

Anasema aliachana na uamuzi mwaka 1995 na kuwa msimamizi wa mechi ambapo baada ya hapo aliamua kugombea ubunge na kukosa.

“Mwaka 1995 nilikosa ubunge, lakini Rais wa wakati ule, Salmin Amour alinichagua kuwa meneja kampeni wake katika uchaguzi.”

Anasema baada ya Salmin kushinda alimchagua kuwa Msemaji Mkuu wa Serikali na mwaka 2000 pia alimchagua kuwa Mwakilishi wa Jimbo la Raha Leo.

Anasema mwaka 2005 akaamua kwenda kugombea kwao Dimani na kushinda.

“Mwaka 2010 nilishindwa ubunge, mwanzo nilishinda kwa kura 300, baadaye wakasema uchaguzi urudiwe, uliporudiwa nikashindwa kwa kura 26, ila mwaka 2015 nimeshinda na ndiyo maana unaniona nimekuja bungeni Dodoma,’’ anasema.

USHAURI KWA WAAMUZI

Anasema ili mwamuzi aweze kuwa bora ni lazima aheshimu kazi yake pamoja na kujiheshimu yeye mwenyewe.

“Kwanza mwamuzi uwe mwadilifu na kuipenda kazi yako, kuzifahamu sheria za mchezo, maanake kuzifahamu ni tofauti na kuzitafsiri sheria kwa jinsi wewe unavyoona, bali kwa jinsi sheria inavyotaka,” anasema.

“Mimi nilichaguliwa kuchezesha Fainali za Afrika mwaka 1983 na Rais wa CAF wakati huo kutokana na kuchezesha vizuri michuano ya Chalenji  katika fainali kati ya Kenya na Uganda,” anasema.

MTOTO WA NYOKA NI NYOKA

Anasema amefanikiwa kupata watoto saba, huku kati ya watoto hao mmoja akiwa ni mchezaji hodari katika timu ya Bandari ya Zanzibar.

Watoto hao ni Said, Gombo, Hairat, Mohammed, Abdulsomal, Hairuni na Isihaka, ambaye anafuata kipaji chake.

HISTORIA

Alizaliwa Oktoba 30, 1953 Dimani, Zanzibar na elimu ya msingi alisoma Shule ya Kombeni mwaka1957-1966 na sekondari akisoma katika shule hiyo hiyo.

Baada ya kumaliza masomo yake nchini alikwenda Yugoslavia kwa masomo ya juu na baadaye nchini Misri.

Amewahi pia kufanya kazi kwa muda mrefu katika Redio ya Zanzibar (ZBC).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles