24.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Mfahamu mkali wa muziki wa dansi Mjusi Shemboza-1

??????????

VALERY KIYUNGU

BILA shaka utakuwa na afya njema msomaji wangu wa Old Skuli. Leo tena tunakutana kwenye safu hii inayokujia kila siku za Jumamosi na kikubwa ambacho huwa tunakiangazia hapa ni muziki wa zamani na wanamuziki wake.

Old Skuli leo inakukutanisha na mwanamuziki mkongwe anayefanya shughuli zake za muziki akiwa kama mpiga gitaa wa kutegemewa kwenye bendi ya Sikinde Ngoma ya Ukae, huyu si mwingine, bali ni Mjusi Shemboza Shekungu. Karibu.

HISTORIA YA MAISHA YAKE

Mjusi Shemboza hakutaka kuweka wazi mwaka aliozaliwa, ila anasema yeye ni mwenyeji wa Tanga vijijini ambapo baada ya kuzaliwa na kukua mpaka kufika umri wa kusoma, wazazi wake walimpeleka shule ili apate elimu ya kumwezesha kupambana na changamoto za maisha.

Licha ya kuwa na mapenzi makubwa na muziki, wazazi wake walimsihi kutojiingiza huko, kwani asingeweza kufanya vizuri kwenye masomo, ambapo yeye alikubali na kutulia mpaka alipofanikiwa kumaliza elimu yake.

“Baada ya kumaliza shule ya msingi nilijiunga na Shule ya Sekondari Popatlal mpaka nilipomaliza kidato cha nne, nilimaliza elimu ya sekondari kwa taabu, kwani mawazo yangu yalikuwa kwenye muziki, kwa kweli sikuweza kufanya vizuri katika mtihani wangu wa mwisho,” anasema.

DHAMIRA YAKE IKATIMIA

Shemboza anasema siku chache baada ya kumaliza elimu ya sekondari, aliweka mawazo yake kwenye muziki wa dansi akiwa na nia ya kujifunza, hivyo akawa ni mtu wa kuhudhuria kwenye maonyesho ya bendi za jijini Tanga.

Lengo lake kubwa la kujitokeza kwenye maonyesho ya bendi hizo lilikuwa ni kujifunza muziki, hasa upigaji wa ala kama vile gitaa, tena lile la rhythm.

Ameutaja mwaka 1977 kuwa ndipo alipoanza kujishughulisha na muziki wa dansi, alijiunga na kikosi cha pili cha bendi ya Jamhuri Jazz au Less Kisancho. Baada ya kuweza kulipiga gitaa hilo akawa huru kulicharaza kwenye maonyesho ya bendi ya Less Kisancho.

AONDOKA TANGA ATUA DAR

Mwaka mmoja baadaye, yaani mwaka 1978, mkongwe huyo aliamua kusafiri kutoka Tanga hadi Dar es Salaam akiwa na lengo la kutafuta bendi ya kuifanyia kazi ili atengeneze maisha yake pamoja na kuendeleza kipaji cha upigaji gitaa.

Baada ya kuwasili hapa jijini alituma maombi kwenye bendi nyingi, ila alijibiwa kwenye bendi moja tu inayoitwa Dar es Salaam Jazz, ambayo ilifahamika kama Majini wa Bahari.

Itaendelea wiki ijayo…

Maoni yalete hapa 0714 288 656

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles