23.6 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

BUNGE LAAFIKI UJENZI BOMBA LA MAFUTA, LAONYA WAVAMIZI

Na Shermarx Ngahemera

BUNGE la Tanzania limeridhia bila vikwazo ushiriki na uendeshaji mkataba wa kuwezesha bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima Uganda hadi Tanga kupitia nchini wakati wa kusafirishwa na kuuzwa nje ya nchi.

Mradi huo umelazimu kuunda kampuni ijulikanayo kama East Africa Crude Oil Project (EACOP) ambayo wadau wake wameainishwa.

Kitendo hicho ni hatima ya kwanza ya mradi huo ambao ulianzishwa mwaka mmoja uliopita na ukiwa na ushindani mkubwa kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Kenya na Tanzania, kushindana vikali kupata zabuni ya kuwezesha bomba hilo kupitishwa nchini mwao.

Mwanzoni Kenya ndio ilitegemewa kufanya hivyo, lakini Uganda ilikaa na kufikiria upya na kuipa heshima hiyo Tanzania kuwa mbia wake wa kuendeleza mradi huo unaoweka picha ya maendeleo ya baadaye ya nchi mbili  hizi za eneo la Afrika Mashariki katika maeneo ya mafuta ya petroli ulimwenguni.

Uzinduzi wa Mradi huo hapa nchini ulifanyika Tanga katika Kijiji cha Chongoleani, ambapo inategemewa kujengwa bandari ya bomba hilo na mambo mengine yahusianayo na miundombinu ya mafuta.

Marais Dk. John Magufuli wa Tanzania na Yoweri Museveni wa Uganda waliibua mambo ambayo awali hayakupatwa  kuwekwa bayana, ikiwamo Rais Magufuli  kueleza mbinu alizotumia kumpiku Rais Kenyatta wa Kenya.

Rais Magufuli  alifichua siri kwa kusema Rais  Museveni alivutiwa na historia yake na nchi hii na kuweka wazi kuwa  usalama  ndio ilikuwa turufu kwa Tanzania kushinda zabuni hiyo.

Isitoshe Tanzania iliachia madai mengi ya kiuchumi ikiwamo VAT na kodi nyinginezo ili kufanya mafuta hayo ya Uganda yawe na tija katika soko la  dunia na kuuzika kwa faida.

Kila mmoja alimshukuru mwenziwe kwa kuelewa kuwa ni kwa ushirikiano tu nchi hizo zinaweza kwenda mbele pamoja na kufanikisha ajenda zao.

Rais Magufuli alisema Museveni ambaye ni mtaalamu wa masuala ya kivita na kijeshi alizingatia hoja za ulinzi na hali madhubuti ya usalama nchini ikawa turufu, naye Museveni akakubali Tanga iwe bandari.

Magufuli alirejea kauli ya Rais Museveni mwenyewe aliyoitoa mapema kuwa wakati wa harakati za ukombozi wa Taifa la Uganda alipitisha Tanga bunduki nne ambazo zilikwenda kukomboa Uganda.

Mradi

Mradi huo wa bomba la mafuta unajengwa kwa pamoja kati ya Serikali za Tanzania na Uganda kupitia Kampuni ya CNOOC Ltd ya China, Total ya Ufaransa na Tullow ya Ireland kwa umbali wa kilomita 1,445, huku bomba hilo likiwa na kipenyo cha inchi 24 kwa gharama inayokisiwa kuwa Dola za Marekani bilioni 3.5.

Bomba hilo la mafuta ambalo ni la kwanza kwa ukubwa Afrika, litajengwa kupitia mikoa minane ya Tanzania ambayo ni Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Dodoma, Singida, Manyara na Tanga, huku likigusa wilaya 24 na vijiji 180.

Kutokana na uzito wa mafuta hayo, inabidi lipashwe moto kwa urefu wote wa usafirishaji ingawa kuanzia Singida eneo la Sekenke mafuta yatakuwa yanasafiri kwa nguvu ya mvutano wa asili (gravity) kwa kuporomoka, kwani eneo hilo liko juu hadi Tanga na kupunguza gharama  nyingi za kupiga pampu mafuta hayo kama ingepita kwenye milima ya Kenya pamoja na kuwa njia fupi kwa kilomita 500.

Fursa za kiuchumi

Fursa nyingi zitaanzishwa na mradi huo  nchini; nazo ni pamoja na kuzalisha ajira  10,000 mpya za muda katika maeneo ambayo bomba litapita na wakati wa mradi na zaidi ya Dola za Marekani milioni 200 kuingia katika mzunguko wa fedha na watu 2,000 kuajiriwa kwa kudumu kushughulikia bomba hilo.

Nyingine ni kukua kwa sekta ya viwanda, biashara katika sekta ya anga kuimarika kutokana na upatikanaji rahisi wa mafuta, kuingiza fedha za kigeni na hivyo uchumi kupanda.

Dk. Magufuli aliahidi kupanua bandari ya Tanga ili kuruhusu meli kubwa kutia nanga, ikiwa ni jibu kwa

ombi lililotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martin Shigela, aliyeomba bandari hiyo ipanuliwe ili kuongeza wigo wa ajira na ukuzaji wa uchumi wa mkoa huo hasa ikizingatiwa kuwa viwanda vingi vinaanzishwa mkoani humo vikiwamo vitatu vya saruji.

Haiwezekani tuwe na mradi mkubwa kama huu tusiwe na bandari yenye kina kirefu, nimesikia ombi la mkuu wa mkoa,” alisema Magufuli.

Dk. Magufuli na hata Bunge kupitia Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, alisema wananchi watakaojenga katika maeneo ya mradi kwa lengo la kutaka kulipwa fidia, hawatafanikiwa kwani tayari eneo lote la mradi linajulikana lilivyo.

“Tayari kuna watu wanapitia katika maeneo ambayo yatapitiwa na miundombinu ya bomba kwa ajili ya kujenga, lakini niwaambie kuwa hawataweza kulipwa fidia,” alionya Lukuvi

“Wale watakaokutwa kwenye eneo la mradi ambao picha zinaonyesha watalipwa kwa mujibu wa sheria na taratibu, lakini wale wanaojenga sasa niwaambie tu wazi imekula kwenu kwani hamtapata kitu,” alisisitiza.

Rais Museveni alitoa angalizo kwa bara la Afrika kubadilika kwani nchi zake zinatumia bidhaa zisizozalisha na inazalisha vitu isivyovitumia na hivyo kukosa urari wa kiuchumi na kupata hasara endelevu.

Alisema nchi za Afrika zinanunua zaidi bidhaa nje ya bara hilo zenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 33, huku zenyewe zikiuza nje bidhaa Dola bilioni 13.8 na kuasa nchi hizo kutumia maliasili walizonazo kuleta maendeleo katika nchi zao.

Takwimu zinaonesha kuwa biashara ndani  ya Afrika ni chini ya Dola bilioni 3 na hivyo kutishia usalama wa biashara wa bara hili na kudai juhudi za dhati ili kufanya nchi za Afrika zifanye biashara kwa zenyewe na kati yao.

Alisema kupatikana kwa mafuta Uganda  kutasaidia biashara ya usafirishaji katika sekta ya anga Afrika Mashariki kuimarika.

“…makampuni yetu ya ndege yataweza kununua mafuta hayo kwa bei ya chini kulinganisha na bei za huko Uarabuni.”

Alichukua nafasi hiyo kuiomba Tanzania ijenge bomba la gesi asilia kwenda Uganda iweze kuzalisha shaba na chuma katika eneo la Kasese.

Wafanyabiashara wachangamkia fursa

Chama cha Wafanyabiashara wa Tanzania kuhusu Mradi, yaani Association of Tanzania Oil and Gas Service Providers (ATOGS) wametiliana saini ya maelewano (MoU) na wenzao wa Uganda, yaani Chama cha  Uganda cha Watoa huduma ya Mafuta na Gesi (Association of Oil and Gas Service Providers) ya kutafuta  rasilimali fedha, teknolojia na ujuzi wa mradi ili kampuni  za nchi hizo mbili ziweze kushiriki kikamilifu  katika mradi huo wa mafuta ghafi (EACOP).

Makamu Mwenyekiti wa ATOGS, Abdulsamad Abdulrahim, anasema makubaliano hayo yanaunga mkono maono ya Serikali ya kuwa na uchumi wa viwanda na kuwa nchi ya kipato cha kati ifikapo 2025.

Anasema  mali kama bidhaa na huduma zitatolewa kwa kikoa kupitia  ushirikiano  na kampuni za nchini  ambayo itamiliki si chini ya asilimia 25 katika ubia huo.

Anasema maelewano hayo vilevile yatahusu kuwa jukwaa la kugawana na kubadilishana habari, fursa, ujuzi na kuhamishia teknolojia.

‘Tumeamua kufanya hivyo ili kufanikisha azma ya kauli ya Rais Magufuli ya kutaka kuona miradi ya mafuta na gesi inawanufaisha Watanzania,” alisema  Abdulrahim.

Alitamba kuwa wana uwezo wa kiutawala, kiufundi na kifedha kuweza kushughulika kikamilifu katika sekta hiyo.

Alifichua kuwa kazi ambazo ziko tayari kwa kuchukuliwa fursa na Watanzania wenye shughuli ya ugavimali ni ujenzi,  uhandisi, ununuzi bidhaa, ufikishaji mali (logistics ) na huduma za moja kwa moja au kupitia wengine na hivyo ATOGS kudai jukwaa la pamoja kwa ajili ya kuimarisha upatikanaji wa mikakati ya ubia wa kimataifa kufikia kazi hizo.

Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Chama cha  Uganda cha Watoa Huduma ya Mafuta na Gesi (Association of Oil and Gas Service Providers), Emmanuel Magurura, alisema kampuni za ndani zimejizatiti  na ziko tayari kufanikisha mitaji inayohitajika  ili waweze kushiriki kikamilifu katika fursa zilizojitokeza katika miradi ya mafuta na gesi.

Anasema makubaliano hayo yatawezesha wanachama wake kupata mafunzo, kupata ithibati ya kazi na kushiriki pamoja katika kutafuta zabuni za miradi.

Aonavyo yeye kampuni za ndani zina ujuzi wa kutosha  uliopatikana kutoka miradi mbalimbali ya kimataifa katika eneo hili na hivyo wakati umefika wa wao kuonesha  uwezo wao kushughulikia miradi mikubwa katika eneo hili la Afrika Mashariki.

“Wananchi wanapaswa waelewe kuwa kampuni zetu za ndani  zina uwezo  kwa maana ya teknolojia  na mtaji na wako tayari kushindana  na kampuni za nje kutoka China na kwingineko,” alisema Magurura.

Anategemea kuwa faida hiyo haitakuwa kwa kampuni wanachama tu wa vyama vyao ila itaongeza uwezo wa kampuni za nyumbani kushindana katika zabuni za soko la miradi ya mafuta na gesi kimataifa na hivyo kupata kazi huko.

Mradi umejaa faida za kiuchumi

Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Medard Kalemani, akielezea ujio wa mradi huo, alisema thamani ya mradi wote ni Dola za Marekani bilioni 3.5 (zaidi ya Sh trilioni nane).

Mbali na hilo, alisema Tanzania inayo nafasi kubwa ya kufaidika na mradi huo kwa sababu asilimia kubwa upo Tanzania kwa kilomita 1,115, huku Uganda ikiwa na kilomita 330 tu.

“Ni fursa ya kipekee kwamba mradi huo kwa kiasi kikubwa upo Tanzania na tunatarajia zaidi ya Dola za Marekani milioni 200 zitasambaa Tanga na kuchangamsha uchumi wake, huku pia Tanzania ikiingiza asilimia kubwa ya fedha za kigeni.

“Niwaombe wafanyabiashara wa Tanzania kuchangamkia fursa zote zilizo mbele yetu kwa lengo la kuhakikisha mradi huu unanufaisha jamii nzima kupitia sekta mbalimbali za hoteli, ujenzi wa hospitali, taasisi za fedha, elimu na kadhalika,” alisema Dk. Kalemani.

Naye Waziri wa Nishati na Madini wa Uganda, Mhandisi Irene Nafuna Muloni,  anasema mradi huo umedhihirisha nia njema ya viongozi wa pande zote mbili na kufungua milango ya fursa za uchumi na biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Irene alisema Uganda pekee itapandisha uchumi wake kwa asilimia 60 na mradi huo umezingatia athari za mazingira kutokana na tafiti mbalimbali zilizofanywa kitaalamu na hivyo kuongeza idadi ya fursa.

Ya kuzingatia

Bunge limepitisha azimio la kuridhia mkataba wa Serikali ya Tanzania na Uganda kuhusu mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika kwa kuweka angalizo kuhusu kodi na fidia kwa wananchi.

Akiwasilisha taarifa ya Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini Azimio la Bunge kuridhia mkataba, Makamu Mwenyekiti wa kamati, Deogratius Ngalawa Mbunge wa Ludewa (CCM), alisema Serikali inatakiwa kuwa makini na kifungu  2(c) cha Sehemu B ambayo inahusu kodi ya makampuni.

Alisema kifungu hicho kinaweza kutumiwa vibaya wawekezaji kuihujumu nchi  kwani kinaruhusu hasara iliyobainika katika utekelezaji wa mradi kabla, wakati au baada ya kipindi cha msamaha wa kodi kusogezwa mbele katika mwaka wa fedha unaofuata iwapo haikufanyiwa kazi katika mwaka husika.

“Serikali iwe makini na kifungu hiki wakati wa utekelezaji wa mradi ili kampuni zitakazohusika kutekeleza mradi zisijaribu kutangaza kupata hasara kila mwaka, ili kuikosesha Serikali mapato stahiki,” alieleza.

Wabunge waliishauri Serikali kuangalia kwa umakini Ibara ya Saba ya Mkataba inayoruhusu kampuni itakayotekeleza mradi kusafirisha fedha nje ya Uganda na Tanzania na kuzihifadhi huko bila kizuizi chochote.

“Kamati inaishauri Serikali kuangalia kwa umakini ibara hii ili kuepuka kukinzana na sheria ya mamlaka ya nchi kuhusiana na umiliki wa mali asili ya mwaka 2017 ambayo  Sheria hiyo inazuia wawekezaji kusafirisha fedha kwenda nje ya nchi isipokuwa zile zinazotokana na mgawo wa faida inayopatikana.

Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilitaka kuwepo na upembuzi yakinifu wa mradi kabla ya kuingia katika makubaliano ya utekelezaji ingawa walitoa kauli hiyo, huku wakisifu juhudi za rais kuuleta mradi huo Tanzania.

Msemaji Mkuu Kambi Rasmi ya Upinzani-Nishati na Madini, Devotha Minja, alisema lingekuwa jambo la busara kwa Bunge kutoridhia azimio hilo hadi pale mkataba utakapopitiwa vizuri na kujiridhisha kauli ambayo ilipingwa  vikali na wabunge wengine.

Akifafanua, Dk Mwakyembe alisema hakuna sheria zinazokinzana katika mkataba huo kwa kuwa Watanzania ni wasafirishaji wa mafuta ya Uganda, wakitumika kama vile lori linalobeba ndizi kutoka Kyela kwani ndizi hizo si za mwenye lori

Mbunge wa Tanga mjini CUF, Mbarouk alisema wananchi wa Chongoleani wanategemea kilimo cha minazi na matunda kuishi na kuondolewa kwao eneo hilo na fidia ndogo haitawasaidia.

Naye Profesa Anna Tibaijuka wa Muleba Kusini (CCM), aliridhia azimio hilo.

Aidha, amemtaka Waziri  wa Ardhi kuondoa utata unaofanywa sasa na wapima ardhi wanaopima maeneo yakatakayopita bomba bila taarifa hata kwa mbunge anayehusika.

Profesa  Palamagamba Kabudi, alisema Watanzania wanatakiwa kuchangamkia fursa zinazoambatana na huduma mbalimbali za msingi zinazotakiwa kuwezesha maisha ya kawaida.

Alisema mapato ya Serikali ni takribani Dola za Marekani 12.2 kwa kila pipa la mafuta ghafi litakalosafirishwa kupitia Bandari ya Tanga kulingana na kiwango cha hisa zake.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles