24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

BoT, Bandari Kuchunguzwa

Asha Bani -Dar es salaam

MAMLAKA ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imetoa ripoti ya tathimini ya utendaji kwa mwaka  2018/19, ambapo pamoja na mambo mengine taasisi mbalimbali zikiwepo Benki Kuu (BoT), Mamlaka ya Bandari (TPA), Shirika la Reli (TRC), Shirika la Viwango (TBS) baadhi ya manunuzi yake yameonekana kuwa na viasharia vya rushwa na ukiukwaji wa sheria na kanuni.

Kutokana na hali hiyo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, aliitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kufanya uchunguzi wa viashiria hivyo na ifikapo Oktoba 15 apate ripoti.

Ukiukwaji sheria

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa PPRA, Dk. Matern Lumbanga, akisoma taarifa yake kwa Waziri Mpango, alisema mbali na kufanya ukaguzi wa kawaida, mamlaka pia ilifanya uchunguzi wa tuhuma za ukiukwaji wa sheria na taratibu za manunuzi.

“Katika mwaka wa fedha 2017/18, PPRA ilifanya uchunguzi nunuzi tano kuhusu mikataba au zabuni 13 za manunuzi zilizokuwa na thamani ya Sh bilioni 375.

“Taasisi hizo ni pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA), Wakala wa Umeme Vijijini (REA) na Shirika la Viwango (TBS).

“Uchunguzi huu ulitokana na maagizo kutoka mamlaka za juu ama taasisi zenyewe. Kupitia uchunguzi huo Serikali iliokoa Sh bilioni 3.39 lakini ilipata hasara ya Sh bilioni 4.36 kwa kukosa ada ambazo zingelipwa na wazabuni na taasisi nunuzi kufanya mabadiliko katika usanifu wa miradi.

“Mamlaka imependekeza hatua za kinidhamu zichukuliwe kwa wahusika na pia imepeleka taarifa za uchunguzi Takukuru kwa hatua zaidi,” alisema.

viashiria vya rushwa

Kwa upande wa taasisi zilizokutwa na viashiria vya rushwa, Dk. Lumbanga, alisema ukaguzi wa PPRA pia ulipima uwezekano wa uwepo wa viashiria vya rushwa katika taasisi au miradi husika.

“Tathimini ya jumla ya viashiria vya rushwa inaonyesha miradi 12 yenye thamani ya Sh bilioni 25.8 ilibainika kuwa na viwango vikubwa vya viashiria vya rushwa kwenye baadhi ya miradi katika hatua mbalimbali za manunuzi, ikimaanisha kuwepo kwa uwezekano wa mkubwa wa vitendo vya rushwa katika miradi hiyo.

“Miradi hiyo inahusu taasisi tisa, ambazo ni Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Shirika la Reli (TRC), Mamlaka ya Bandari (TPA), Shirika la Viwango (TBS) Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Singida, Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Wang’ing’ombe, Halmashauri za Manisipaa za Kigamboni na Ubungo na Halmashauri ya Mji wa Kahama,” alisema Dk Lumbanga.

Thamani ya fedha

Alisema PPRA ilifanya ukaguzi wa kupima thamani halisi ya fedha kwenye miradi 290 ya manunuzi yenye thamani ya Sh trilioni 8.478.

Alisema miradi hiyo inajumuisha ya ujenzi wa miundombinu ya majengo, madaraja, barabara, reli, umeme, maji na umwagiliaji na miradi ya huduma za ushauri wa kitaalamu.

Alisema katika miradi 290 iliyofanyiwa ukaguzi, 239 ilipata wastani mzuri, 49 ilipata alama ya kiwango cha kati na miwili yenye thamani ya Sh milioni 95.33 ilipata kiwango kisichoridhisha.

Miradi iliyopata kiwango kisichoridhisha inahusu uchimbaji wa mashimo ya kuchakata taka ngumu katika Halmashauri ya Mji wa Kahama na usambazaji wa mita za maji katika Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Kahama na Shinyanga (Kashwasa).

Uzingatiaji sheria

Alisema PPRA ilifanya ukaguzi katika mikataba 7,738 ya manunuzi yenye thamani ya Sh trilioni 9.12 kutoka katika taasisi nunuzi 104 zikiwepo 43 katika kundi la wizara, idara na wakala wa Serikali.

Alisema taasisi nyingine 28 zinatoka Mamlaka ya Serikali za Mitaa, 33 mashirika ya umma na matawi matano ya taasisi nunuzi yaliyokasimiwa mamlaka ya kufanya manunuzi.

“Ni vyema ikafahamika kuwa asilimia 96.3 ya miradi yote iliyokaguliwa ni ile iliyotekelezwa na taasisi zenye manunuzi makubwa, yaani zile taasisi ambazo kila moja manunuzi yake yana thamani ya Sh bilioni 20 au zaidi,” alisema Dk Lumbanga.

Alisema matokeo ya ukaguzi wa uzingatiaji wa sheria ya manunuzi ya umma, yanaonesha wastani wa jumla wa uzingatiaji kwa taasisi zilizokaguliwa ni asilimia 76 ambayo ni ongezeko la asilimia mbili ilinganishwa na mwaka uliopita.

Alisema wastani huo wa asilimia 76 bado uko chini ya lengo ambalo ni asilimia 80.

“Uchambuzi zaidi unaonesha kuwa taasisi zote zilizofanyiwa ukaguzi, 38 zilipata wastani mzuri, (80% au zaidi). 63 zilipata wastani wa kuridhithisha (60-79%) wakati taasisi sita zilipata wastani hafifu au usioridhisha chini ya aslimia 60,” alisema Dk. Lumbanga.

Alizitaja taasisi hizo sita kuwa ni Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta), Wakala wa Mbegu za Kilimo, Taasisi ya Utafiti wa Dawa (NIMR), Kituo cha Diplomasia na Halmashauri za Wilaya za Kaliua na Nsimbo.

Mapendekezo

Alisema kutokana na matokeo ya ukaguzi wa ukidhi wa sheria ya manunuzi na upimaji wa thamani halisi ya fedha, PPRA imewataka wakuu wa taasisi saba zilizofanya vibaya kwenye eneo hilo kujieleza kwa mamlaka zao za nidhamu.

Alisema pia PPRA imeagiza hatua za kinidhamu kuchukuliwa dhidi ya watumishi wa KASHWASA na Halamashauri ya Mji wa Kahama ambao walihusika kwenye miradi iliyopata alama mbaya.

Dk Mpango

Akizungumza baada ya kupokea ripoti hiyo,  Dk. Mpango aliiagiza Takukuru, kuanza uchunguzi ili kubaini wala rushwa, waliofanya manunuzi yasiyozingatia kanuni ili hatua dhidi yao zichukuliwe.

Alisema ni vyema kuanza na taasisi ambazo manunuzi yake yanaanzia Sh bilioni 20 na kuendelea.

 “Hali hii mimi naiita ni kama kansa inayotafuna na haistahili  kufumbiwa macho wala kupapaswa, kwanza hizo asilimia 76 ambazo PPRA wameona zimekidhi lengo ni ndogo mno, hazijafika hata asilimia 80 ambayo ndio lengo lililotakiwa kufikia hivyo ni lazima tufanyie kazi,’’alisema  Dk. Mpango

Dk. Mpango alisema ni lazima uchunguzi ufanyike  na kisha wahusika wote wachukuliwe hatua kali ikiwemo viongozi wao kujitathimini na maofisa ugani waliohusika kukaa pembeni kupisha uchunguzi.

“Narudia tena kwa kusisitiza, wanatakiwa kukaa pembeni kupisha uchunguzi na wakibainika wanatakiwa kurudisha fedha ambazo walizichukua au kuzipoteza kwa namna yoyote ikiwemo rushwa.

“Kama wangekuwa hapa waliotajwa ningeagiza Takukuru waondoke nao, na Wizara ya Maji pia namuagiza waziri wake aanze kuchukua hatua kabisa.

 “Oneni kama Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi, BoT, TAA , REA na TBS hawa ni lazima Takukuru waingie kazini wafanyiwe kazi, ni lazima tufike mahala tuwaonee uchungu wananchi wetu, hizo ni fedha zao,’’alisema Dk.Mpango.

Dk. Mpango alisema mpaka kufika Oktoba 15 Takukuru wawe wameshawasilisha ripoti hiyo na iweze kumfikia Waziri Mkuu na Rais John Magufuli pia.

Waziri Mpango  pia ameagiza mpaka kufikia mwisho mwaka huu, taasisi zote za Serikali ziwe zimeingia katika mfumo wa manunuzi ya umma kwa njia ya mtandao (TANePS) .

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles