23.3 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Bashe afumua madudu

DERICK MILTON- MWANZA.

NAIBU Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amefichua upotevu wa fedha za wakulima zaidi ya Sh. bilioni 120  kwenye vyama vya ushirika nchini.

Hatua hiyo ni muendelezo wa nyingine kama hizo alizochukua huko nyuma ikiwapo ile ya siku nne zilizopita ambapo alibaini Bodi ya Korosho imechepusha Sh. bilioni 10 zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya ununuzi wa mbolea na viuatilifu.

Akinukuu ripoti ya ukaguzi ya Shirika la Ukaguzi wa Vyama vya Ushirika (COASCO), Bashe alisema, wamebaini kuwepo kwa upotevu wa jumla ya Sh. bilioni 123 kwenye vyama hivyo.

Bashe aliyasema hayo jana wakati akifungua kikao cha wadau wa Bodi ya Pamba nchini kilichofanyikia ukumbi wa Benki Kuu (BoT) jijini Mwanza ambapo alieleza kuwa wahusika wote watachukuliwa hatua kali.

“Hapa nina kabrasha, nitawapatia wakuu wa mikoa wote, na nitamkabidhi kiongozi wa tume, kwa ripoti ya COASCO ushirika kumetokea jumla ya upotevu wa Sh. bilioni 123, na niseme hapa hatua kali zitachukuliwa kwa wahusika wote,” alisema Bashe.

“ Niwahakikishie wote maana hizi ni fedha za wakulima, wote waliohusika katika huu upotevu watachukuliwa hatua kali, na wakuu wa mikoa tutawapa majina ya Amcos gani wanahusika na mnatakiwa kuchukua hatua,” aliongeza Bashe.

Alisema ushirika uliopo kwa sasa unahitaji mabadiliko makubwa kwani hauwezi kutatua matatizo ya kilimo hasa kwenye zao la pamba.

Alisema mfumo unatakiwa kubadilishwa kutoka ushirika wa kuhudumia wakulima na kuwa ushirika wa kibiashara.

“Lazima tuwe na ushirika ambao unaongeza thamani kwenye pamba ya wakulima na siyo kuwa na ushirika ambao umeendelea kuongeza gharama kwa wakulima,  na sisi kama wizara hili jambo ndiyo kipaumbele cha kwanza kwetu hivi sasa,” alisema Bashe.

“Tumeanza mikakati ya kubadilisha mfumo wa ushirika huu, tunataka tuwe na mtalaamu wa fedha kwenye ushirika ngazi ya kata ambaye atahusika na kilimo, fedha na masoko mtu mwenye elimu ya fedha,” alisema Bashe.

Aidha Naibu Waziri huyo alisema Serikali haitajiingiza tena kwenye kupanga bei ya pamba na badala yake wataliachia soko ndilo liweze kusema bei halisi ya pamba kwa mwaka husika.

“Serikali hatutaingilia suala la bei ya pamba tena, soko lenyewe ndilo litazungumza, Serikali tutabaki katika kuhakikisha wakulima wanazalisha vizuri na tunawawekea mazingira mazuri ya kilimo chao ili wasiweze kupata hasara kali tena,” alisema Bashe.

Katika kikao hicho Bodi ya pamba imesema kuwa kuelekea msimu mpya kilimo hicho 2019/20 utaratibu wa kuwakopesha pembejeo wakulima wa zao hilo zikiwemo mbegu na madawa hautakuwepo na badala yake vitauzwa.

Akitoa utaratibu huo Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi hiyo, Marco Mtunga amesema haina uwezo wa kukopesha tena wakulima pembejeo na bado inadaiwa madawa na mbegu vilizotumika msimu uliopita.

” Katika mkoa tulitoa pembejeo kwa wakulima zenye thamani ya Sh. bilioni 12 lakini hadi sasa tumekusanya milioni 400 tu, na bado tunadaiwa bilioni 45 za mbegu na dawa kutoka kwa wazalishaji na wasambazaji maana tuliwaambia watukopeshe lakini urejeshaji wa fedha hizo kutoka kwa wakulima ni mgumu,” AlisemaMtunga.

Aliongeza kuwa katika msimu huu bodi hiyo itasambaza tani 25,000 za mbegu, chupa milioni nane za dawa pamoja na vinyunyuzi 20,000 ambapo alisema vyote hivyo vitauzwa.

“Tulifanya maamuzi hapa ya kupunguza Sh.70 kwenye mfuko wa kuhudumia zao la pamba, haya ndiyo madhara yake, kama bodi hatuna uwezo wa fedha za kuweza kuwakopesha wakulima pembejeo, hii ndiyo ilikuwa kazi ya huo mfuko,” alisema Mtunga.

Wakizungumza katika kikao hicho baadhi ya wadau wa pamba wameunga mkono uamuzi wa Serikali wa kurekebisha vyama vya ushirika kutokana na viongozi wake wengi kudaiwa kutokuwa waadilifu na kutuhumiwa kufanya ubadhilifu mkubwa wa fedha.

Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Agrey Mwanri alisema ikiwa ushirika hautaimarishwa na kuwa na nguvu ikiwemo kuwa na viongozi wenye udailifu zao la pamba haliwezi kuwa na manufaa kwa mkulima.

MAAMUZI MAKUBWA YALIYOFANYWA HIVI KARIBUNI KILIMO

Septemba 23, mwaka huu Bashe aliitaka Bodi ya Korosho kurudisha Sh. bilioni 10 zilizotolewa na kwa ajili mbolea na viuatilifu lakini wao wakabadilisha matumizi.

Alisema uamuzi huo umesabaisha mbolea na viuatilifu kubaki bandari kavu.

Mbali na kuagiza kuchukuliwa hatua za kinidhamu kwa viongozi wote waliohusika kubadilisha matumizi ya fedha hizo pia

aliagiza kulipwa kwa deni lililopo BoT ambalo limebaki  Sh. bilioni mbili.

KOROSHO

Miongoni mwa maamuzi makubwa ya hivi karibuni yaliyofanywa na wizara hiyo ni pamoja na kuja na mkakati mpya wa ununuzi wa zao la korosho kwa njia ya mnada wa wazi kupitia  mtandao ambao utaanza kutumika katika mwaka wa mavuno 2019/2020.

Waziri wa wizara hiyo, Japhet Hasunga, alisema uamuzi wa kutumia mfumo huo umetokana na uzoefu walioupata wakati wa ununuzi wa zao hilo msimu uliopita.

SUALA LA MAHINDI

Aidha suala lingine lililotekelezwa na wizara hiyo ni hatua kufumua urasimu wa biashara ya nafaka kati ya Tanzania na Kenya.

Katika uamuzi huo itakumbukwa Bashe aliagiza makubaliano ya nchi hiyo jirani kuuziwa tani milioni moja za mahindi na unga.

Aliagiza kuchukuliwa hatua za kuondoa vikwazo vyote vinavyokwamisha usafirishaji mazao kwenda nchini humo ikiwamo kufanyika utaratibu utakaomwezesha mfanyabiashara atakayenunua mahindi kutoka katika vituo vitakavyotengwa kupewa taarifa itakayomwezesha kuyasafirisha moja kwa moja bila kulazimika kukaguliwa tena njiani.

Aidha hivi karibuni Waziri, Hasunga alikaririwa akithibitisha taarifa za Zimbabwe kununua tani 100,000 za mahindi kutokana na nchi hiyo  kukabiliwa na ukame.

Waziri Hasunga alisema pia Zimbabwe iliomba kiasi kikubwa cha mahindi, na hivyo kuweka masharti ya kuuziana kwa fedha taslimu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles