24.7 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 19, 2024

Contact us: [email protected]

Bila upinzani imara hakuna serikali imara

MIONGONI mwa makosa  ambayo Marais  wengi wa Afrika wanayafanya ni kudhani kuwa kuviangamiza vyama vya upinzani ndio mwarobaini wa kuleta  maendeleo.

Fikra za namna hii zinasababisha kuviona vyama vya upinzani kama uasi ni mfu kwani maendeleo kamwe hayawezi kupatikana kwa mtazamo na akili ya mtu mmoja pasipo nguvu ya mawazo kinzani kutoka kwa  wengine.

Inasikitisha sana  kwamba pamoja na mataifa mengi ya Afrika kuukubali mfumo wa vyama vingi katika miaka ya 1990 na kuendelea bado kuna hali ya sintofahamu kwani kila kukicha ni vurugu zitokanazo na mnyukano wa kisiasa.

Ni kweli wengine wanaweza kusema nchi nyingi za Afrika ziliukubali mfumo wa vyama vingi kutokana na shinikizo la mataifa magharibi na wala haukuwa utashi wao kwani watawaliwa wengi  wakiwamo wa Tanzania bado walitamani kuendelea na  mfumo wa chama kimoja lakini la kujiuliza ni nini kilisababisha wapigania uhuru wa awali kama Mwalimu Nyerere kuuridhia mfumo huu?

Je, hayati Mwalimu Nyerere ambaye wengi wetu tunamhusudu kwa  mazuri aliyoyafanya, kuubali mfumo wa vyama vingi ilikuwa ni usaliti ukizingatia alikuwa ameishastaafu au ni jicho pevu alilokuwa nalo kwa kuona yatakayotokea mbele  maana alianza kushuhudia viongozi wakigeuka miungu watu badala ya kuwatumikia wananchi?

Ni ukweli usiopingika Mwalimu Nyerere alizisoma alama za nyakati na kutambua kuwa chama tawala bila kupata nguvu ya kukosolewa kinaweza kujisahau na hatimaye siku moja kuitumbukiza nchi kwenye shimo refu la migogoro pale  wananchi watakapoanza  kuhisi kunyanyaswa kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Si tu ni  Mwanamapinduzi Nyerere aliyependelea mfumo mpya wa vyama vingi bali pia hata tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa mfumo huu unayo nguvu ya kuifanya serikali iwajibike na hatimaye kuleta maendeleo tarajiwa.

Kwa mujibu wa (Mililler 2000) anasema demokrasia ya vyama vingi, vyama vya siasa huwajibika na pia kuwa  kiungo muhimu kati ya serikali iliyoko madarakani na raia ambao kimsingi maslahi yao hupata nguvu ya utetezi kwa kuchochea sera na watunga sera ili waweze kufikia maamuzi sahihi.

Si tu kutetea nguvu ya sera na watunga sera pekee bali pia vyama vya upinzani vinao uwezo wa kuisimamia serikali ili iwatumikie raia wake ( Burnell 2004)

Wakati umewadia kwa viongozi wakuu wa nchi hususani wa Bara la Afrika kuukubali na kuuchochea mfumo wa vyama vingi kwa ajili ya kuwaletea wananchi maendeleo na kuepuka migogoro isiyo na sababu za msingi.

Ni ulevi wa madaraka ni ufinyu wa fikra kwa  kiongozi yeyote kusimama hadharani na kutamka kuwa nchi inakosa maendeleo kutokana na uwepo wa vyama vingi.

Ni kweli kuna ushahidi finyu wa kitaaluma unaoonesha uhusiano  kati ya demokrasia ya vyama vingi na maendeleo kwani China mbali na kubinya demokrasia bado maendeleo yake yanakuja kwa kasi lakini Je, vipi kwa  mataifa ya magharibi yenye maendeleo ya muda mrefu tena ndani ya vyama vingi?

Kama vyama tawala vinawajibika ipasavyo kwa  wananchi huku maendeleo yakionekana waziwazi,  hofu ya kuogopa  ukosoaji wa vyama vya upinzani inatoka wapi?

Wapigania uhuru wetu mfano Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere hawana budi kuenziwa na viongozi wa Afrika hasa  walioko madarakani kwa kuwekeza kwenye Katiba imara zitakazoimarisha mifumo ya  vyama vingi vya siasa, kuheshimu mihimili mingine ya mahakama na Bunge bila kusahau taasisi za kiraia na vyombo vya habari.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles