30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Rais Buhari ana kibarua kigumu kwa Atiku urais 2019

JOSEPH HIZA NA MTANDAO

KAMA ilivyo kwa wanasiasa wengi barani Afrika, Atiku Abubakari, anaweza asiwe moja ya wanasiasa wasafi, lakini hakuna mwingine,  Rais Mohamed Buhari anapaswa kumuogopa zaidi yake.

Makamu Rais huyo wa zamani wa Nigeria, amekuwa na ndoto ya urais kwa karibu miongo mitatu sasa.

Ni mwanasiasa mkongwe kwa mchezo huu wa kisiasa na umri wake wa miaka 71 unatosha kumfanya ajue nini cha kufanya kushinda uchaguzi ulio mbele yake.

Pia amebarikiwa na noti nene, kitu ambacho ni kama sifa ya ziada kwa yeyote anayetaka kuwania wadhifa wa juu katika moja ya mataifa yanayoongoza kwa rushwa duniani.

Lakini hayo hayamzuii Rais mtetezi Muhammadu Buhari kumhofia Atiku katika uchaguzi wa urais uliopangwa kufanyika Februari 2019.

Jumapili iliyopita, Atiku alitabasamu kwa mbali baada ya kutangazwa mshindi katika kupeperusha bendera ya chama cha People’s Democratic (PDP) katika uchaguzi huo. Ni kwa sababu alifahamu fika kwa kutambua historia ya nyuma, hajamaliza kazi bado.

Lakini anaweza kuonekana kupata ahueni kwa kuinyaka fursa hiyo kutokana na kukumbuka huko alikotoka alivyohangaika mara kadhaa ili kuipata bila mafanikio.

Ndiyo maana alijitoa kutoka chama tawala cha All Progressives Congress (APC) Desemba 2017 ili kutafuta mahala, ambako angeweza kupata tiketi ya kumwezesha kuelekea kule iliko ndoto yake hiyo, ukizingatia pia umri alio nao.

Kuwa Rais wa Nigeria ndicho kinachomfanya Atiku asilale, amekuwa na ndoto hiyo tangu mwaka 1992.

Na kwa sababu hiyo amebadili, yaani kuhama hama vyama kufikia hapo alipo.

Amekuwa akifarakana na vigogo kama vile Chifu Olusegun Obasanjo, bosi wake wa zamani wakati akiwa makamu wake. Ameitwa kila aina ya majina mabaya. Ameitwa fisadi na amewahi kumpigia magoti Obsanjo ili kujaribu kurudisha uhusiano wao.

Huyu ni mtu aliye tayari kusalimisha kila kitu ili tu awe rais wa Taifa hili lenye watu wengi zaidi barani Afrika.

Wakati wa mkutano mkuu wa uteuzi wa mgombea urais wa PDP mwaka 2010, ambao Atiku alipoteza kwa Goodluck Jonathan, alivunjika moyo mno na kusema uchaguzi huo ulikuwa feki.

Na hivyo akaenda kuranda randa katika vyama vya Action Congress, Action Congress of Nigeria na kisha All Progressives Congress mwaka 2013 kabla ya kurudi PDP mwishoni mwa mwaka jana.

Yaani alikuwa akitafuta jukwaa, mbalo atazindulia ndoto yake ya urais. Alikuwa katika hali ya kukata tamaa na bado ana wasiwasi kwa hatua aliyobakia.

Akiwa amezaliwa Novemba 25 1946, anatokea Jada katika Jimbo la Adamawa lililopo Kaskazini Mashariki mwa Nigeria, Atiku ametokea katika utumishi wa umma alikostaafu.

Na akiwa tayari amejaribu bahati yake kuwania ugavana, aliwania tiketi ya kugombea urais mwaka 1993 na kushika nafasi ya tatu nyuma ya mfanyabiashara bilionea Moshood Abiola na  Babagana Kingibe kwa Chama cha Social Democratic Party (SDP).

Uchaguzi huo wa chama haukutoa mshindi hivyo kukawa na mrudio, ambayo Atiku alijitoa na kumuunga mkono Abiola, ambaye alishinda uteuzi na kwenda kushinda uchaguzi mkuu ambao hata hivyo ulifutwa na jeshi.

Jaribio lake la pili kuwania urais lilikuja mwaka 2006 wakati alipowania urais kwa tiketi ya Chama cha Action Congress.

Awali aliondolewa na Tume huru ya Uchaguzi, alipigania haki yake mahakamani ambayo ilimrudisha.

Aliwania chaguzi lakini akashindwa akishika nafasi ya tatu nyuma ya Umaru Yar’adua wa PDP na Muhammadu Buhari wa ANPP.

Jaribio lake la tatu la urais lilikuwa mwaka 2011 baada ya kurejea PDP mwaka 2010. Aliwania katika kura za uteuzi na kushindwa na Rais mtetezi Jonathan na kusababisha kukihama chama hicho.

Aliwania tena kuteuliwa kuwania urais mwaka 2014 kwa tiketi ya APC alishindwa kwa kushika nafasi ya tatu huku Muhammadu Buhari akiongoza na Rabiu Kwankwaso kuwa wa pili.

Buhari akashinda uchaguzi huo wa urais kwa kumshinda Jonathan na Atiku ameshinda kura ya uteuzi kwa tiketi ya PDP baada ya majaribio matano yaliyofeli.

Mwaka 2017, wakati alipoona kuna dalili APC itamwachia Buhari kutetea urais, Atiku alitangaza kukihama chama hicho na kumvurumishia Buhari na APC kila aina ya makombora.

“Chini ya APC, Nigeria haifanyi lolote, chini ya APC watu wetu hawafanyi kazi,” Atiku alisema saa chache tu baada ya kuondoka chamani humo.

“PC ilituahidi umoja na mshikamano, chini ya APC Nigeria imezidi kugawanyika na uhasama wa kidini na kikabila tangu vita ya wenyewe kwa wenyewe. APC “ilituahidi kujijenga upya, ikiwa madarakani imeukana mkakati wa kujiunda upya.

“APC iliahidi vita dhidi ya ufisadi lakini tulichoona wazi ni ni vita dhidi ya upinzani,” aliongeza.

Hata hivyo, Atiku amekuwa akituhumiwa rushwa kwa muda mrefu na ametuhumiwa utakatishaji wa fedha na mamlaka za Marekani na tuhuma za kupokea hongo akiwa ofisa wa serikali katika mkataba wa Siemens.

Aidha wakati akiwa makamu wa rais wa wakati wa utawala wa Obasanjo, alituhumiwa kuongoza harakati za ubinafishaji zilizomtajirisha.

Hadi leo hii, Obasanjo hawezi kumtazama na hawezi kumuunga mkono hata katika wadhifa wa udiwani.

“Iwapo nitamuunga mkono Atiku kwa yote nnayomjua, Mungu hatonisamehe,” Obasanjo aliwahi kukaririwa akisema.

Kashfa hizi za ufisaid zinatarajia kujitokeza zaidi wakati wa kampeni za kuwania urais siku zijazo.

Hata hivyo, utawala wa Buhari unapaswa kuwa na wasiwasi kuhusu mwelekeo wa Atiku wa kuunga mkono biashara, mtazamo wake wa kujipanga upya na fedha na umaarufu wake Kusini Magharibi na Kaskazini.

Hali yake (Atiku) ya kimjini mjini pamoja na uwezekano wake mkubwa wa kuchagua mgombea mwenza kutoka Kusini Magharibi, anaweza kugawa kura kutoka maeneo yenye mchuano mkali ya Kaskazini Magharibi na Kusini Magharibi na sababu kwamba kila mtu sasa anajua nini Atiku anasimamia kuhusu maeneo ya ukuzaj wa uchumi. Atiku anaonekana kuaminika zaidi kuhusu ukuzaji wa uchumi kuliko Buhari.

Anaweza kuwa mzee kama ilivyo kwa Buhari (75), lakin Atiku anonekana kuwa na ujana zaidi. Anakumbukwa kutangaza kwake kujitoa APC kupitia mtandao wa Facebook na mara kwa mara hutumia Twitter, kutangaza sera zake na amekiri kuwa shabiki mzuri wa Arsenal.

PDP ilikuwa tayari imejipanga kutoa upinzani mkubwa kwa kuteua mgombea mwenye nguvu ya kutisha kumtikisa Buhari, ambaye imekuwa ikimwandama kwa mapungufu yake ikiwamo ulegelege wa afya yake unaoshuhudia akienda kukaa nje kwa miezi kadhaa.

Kikiwa na uchungu wa kuangushwa katika Uchaguzi Mkuu uliopita, ulioshuhudia Goodluck Jonathan akiwa rais wa kwanza anayetetea kiti kushindwa uchaguzini, kinaamini huu ni wakati wa kurudi madarakani baada ya kufanya vizuri chaguzi ndogo za karibuni huko Osun, Ekiti na kwigineko.

Aidha Buhari hajawa rais wa aina yake kama alivyotarajiwa na kuna watu wanaojuta kumpigia kura mwaka 2015 wakisema walifanya kosa kubwa la maisha yao.

Hali hii ya kukatisha tamaa iliyooneshwa na Rais aliyetarajiwa makubwa ikiwamo kungo’a kabisa rushwa na kufufua uchumi kutokana na rekodi yake ya nyuma, kunatoa fursa kwa Atiku kujisahihisha Februari 2019.

Atiku na uwezo mkubwa wa kuwahimili APC kama alivyoonesha katika chaguzi ndogo akishinda mapambano ya ardhini, yaani kutumia pesa nene katika kampeni na silaha za kumfanya Buhari na APC kutetemeka na ni mtu anayeweza kuizidi serikali kimatumizi.

Bado ni mapema kusema nani atashinda, lakini ni moja ya fursa za mwisho kwa Atiku kuwa rais pengine asubiri akapofikisha miaka 76.

Kuibuka kwake kama mpeperusha bendera wa PDP kunapaswa kumpa Buhari na APC siku nyingi za kutolala kabla ya Februari.

Ikumbukwe Buhari ni mstaafu wa jeshini akiwa amefikia ngazi ya umeja jenerali na kuwahi kuwa mtawala wa kijeshi Desemba 31, 1983 hadi Agosti 27,1985, baada ya kuingia madarakani akimpindua Rais Shehu Shagari.

Naye ni mkongwe wa majaribio yaliyoshindwa ya kuwa rais wa Nigeria 2003, 2007 na mwaka  2011 kabla ya kumshinda Jonathan Machi 2015 na kuashiria mara ya kwanza katika historia ya Nigeria kwa rais mtetezi kupoteza kwa mgombea wa upinzani.

Lakini pia 2015, Buhari alikuwa na fursa nzuri dhidi ya Jonathan aliyekuwa mfumbia rushwa za waziwazi, kushindwa kudhibiti kundi la wanamgambo wa Boko Haramu na kuhesabiwa na Wakaskazini kuwa yu kibaraka wa Kusini aliyechukua fursa ya kifo cha mtangulizi wake na aliyekuwa bosi wake Umar Yar’adua kupata urais ulioilenga Kaskazini.

Katika mpambano wa sasa wote Buhari na Atiku ni Wakaskazini, Waislamu na wanaotoka kabila moja la Fulani na fursa hiyo aliyopata Buhari huko nyuma haipo tena.

Lakini Wanigeria wengi wanahisi kuteseka na magumu ya kiuchumi na hivyo wanaweza kugoma kumpatia Buhari muhula mwingine wa urais wa miaka minne.

Watu wanaona tofauti na Buhari yule mkali wa utawala wa kijeshi aliyekuwa mwepesi kuchukua hatua, huyu wa sasa mkongwe ni mzito mno.

Watu hawa wanamhesabu Atiku kama mchangamfu na mtu wa mjini mwenye hisia zilizoenea nchi nzima ikiwamo Kusini Magharibi.

Uzoefu wake kibiashara kiutaifa na kimataifa unahesbiwa kama sifa ya ziada kuponya machungu ya kiuchumi ya Nigeria.

Hata hivyo, bado Buhari anafurahia kama rais mtetezi na ana wafuasi wasiochoshwa naye wa upande wa Kaskazini Magharibi

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles