Imechapishwa: Mon, Sep 11th, 2017

BEKI AZAM AFICHUA SIRI YAKE NA BOCCO

Na THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM

BEKI wa Azam FC raia wa Ghana, Yakubu Mohamed, amesema anafahamu mshambuliaji wa Simba, John Bocco, ni hatari hivyo alilazimika kuwa makini naye ili asiwaletee madhara.

Azam ililazimishwa suluhu na Simba katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliopigwa juzi kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Yakubu aliisifu Simba kwa kusema ina kikosi bora na ndiyo maana kwa kutambua hilo walilazimika kucheza kwa tahadhari ili kuhakikisha hawapotezi mchezo.

“Namfahamu Bocco tangu alivyokuwa anacheza hapa, ni mchezaji mzuri sana ambaye usipokuwa naye makini anaweza akaleta madhara.

“Kwa kufahamu hilo nilikuwa makini kiasi cha kutosha kuhakikisha hasababishi matatizo kwa upande wetu,” alisema.

Beki huyo alisema baada ya kuambulia suluhu, wanajipanga kuhakikisha wanavuna pointi tatu katika kila mchezo wao utakaofuata.

“Mpira ndivyo ulivyo, unaingia uwanjani ukiwa na matarajio lakini wakati mwingine yanakuwa kinyume.

“Tunasahau yaliyopita tunajipanga upya kuhakikisha tunapata matokeo mazuri  katika michezo ijayo,” alisema.

Kabla ya kujiunga na Simba msimu huu, Bocco aliichezea Azam takribani miaka 10 na kuiwezesha kupata taji moja la ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Weka maoni yako

XHTML: You can use these html tags: <a href="" title=""> <abbr title=""> <acronym title=""> <b> <blockquote cite=""> <cite> <code> <del datetime=""> <em> <i> <q cite=""> <s> <strike> <strong>

YOUTUBE

BEKI AZAM AFICHUA SIRI YAKE NA BOCCO