27.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 8, 2024

Contact us: [email protected]

Balozi wa Marekani nchini aitwa kujieleza juu ya taarifa za corona

 MWANDISHI WETU -DAR ES SALAAM

WIZARA ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, imemwita Kaimu Balozi wa Marekani nchini, Dk. Imni Patterson, kujieleza juu ya taarifa wanazozitoa kwenye mitandao yao ya kijamii ikiwamo maambukizi ya corona nchini. 

Taarifa kwa umma iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki jana, ilisema lengo la kumwita balozi huyo ni kutoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali ambayo ubalozi huo umekuwa ukiyaandika katika mitandao yake ya kijamii bila ya uthibitisho.

Itakumbukwa Juni mwaka jana wizara hiyo pia ilimwita Kaimu Balozi wa Marekani nchini, kutoa ufafanuzi kuhusu taarifa ambayo ubalozi huo, uliitoa juu ya angalizo la kiusalama la uwezekano wa kutokea kwa shambulio la kigaidi.

Wito huo ulitokana na taarifa ya ubalozi huo juu ya angalizo la kiusalama kuhusu shambulio la kigaidi katika baadhi ya maeneo ya Jiji la Dar es Salaam ikiwemo eneo la Masaki.

Jana taarifa kwa umma iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Ndani ilisema Dk Patterson aliitwa na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Kanali Wilbert Ibuge, kwenye Ofisi ndogo za wizara jijini Dar es Salaam. 

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Ibuge alieleza masikitiko yake kutokana na namna ambavyo ubalozi huo umekuwa ukitoa taarifa mbalimbali za ushauri wa kiusafiri (travel advisory) zinazoandikwa na kusambazwa na Ubalozi wa Marekani kwenye mitandao ya kijamii ikiwemo suala la namna Tanzania inavyoshughulikia ugonjwa wa COVID-19. 

“Akitolea mfano Katibu Mkuu amezitaja taarifa zilizotolewa na Ubalozi huo Mei 13 mwaka huu Mei 25 kwenye ukurasa wa Twitter wa Ubalozi huo.

Alisema taarifa hizo zote zilionekana kukusudiwa kutoa tahadhari kwa raia wa Marekani waliopo nchini na wanaotarajia kuja Tanzania kuwa jiji la Dar es Salaam siyo salama kutokana na kuwepo idadi kubwa ya wagojwa wa COVID-19. 

“Tahadhari hizo pia zimeendelea  kudai kuwa hospitali nyingi jijini Dar es Salaam (bila ya kuzitaja hospitali hizo) zimefurika wagonjwa wa COVID-19 jambo ambalo siyo kweli na linauwezekano wa kusababisha taharuki kwa Watanzania na wageni kutoka nje ya nchi ilhali hali halisi sivyo ndivyo inavyodaiwa,” ilisema taarifa ya wizara. 

Ilisema Ibuge alimjulisha Dk Patterson kuhusu umuhimu wa Ubalozi kutoa taarifa zilizothibitishwa kwa sababu Serikali haina kizuizi cha aina yoyote kwa mabalozi kutafuta na kupata taarifa sahihi na zenye ukweli. 

Taarifa hiyo ilieleza kuwa Ibuge alimshukuru Kaimu Balozi huyo kwa ushirikiano mzuri na wa kihistoria uliopo baina ya Tanzania na Marekani katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, elimu, biashara, uwekezaji, ulinzi na usalama na maeneo mengine ya maendeleo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles