24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Azam yaandaa mbinu kuivaa Mwadui

azam-fcNA MWALI IB RAHIM, DAR ES SALAAM

UONGOZI wa klabu ya Azam FC umetamba kuwa tayari umeandaa mbinu za kuwamaliza wapinzani wao Mwadui FC katika mchezo wa nusu fainali ya michuano ya Kombe la FA keshokutwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Azam inatarajiwa kurejea leo ikitokea nchini Tunisia ambako ilikwenda kukutana na timu ya Esperance katika mchezo wa marudiano wa raundi ya pili ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika na kuondoshwa kwa jumla ya mabao 4-2 ikiwa ni ushindi wa 2-1 nyumbani na 3-0 ugenini.

Baada ya kutua jijini Dar es Salaam, ‘Wanalambalamba’ hao wataunganisha usafiri wa ndege na kwenda moja kwa moja mkoani Mwanza kwa ajili ya kujiandaa na mchezo huo.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Ofisa Habari wa Azam, Jaffar Iddy, alisema wanatambua kuwa wanakabiliwa na mchezo mgumu lakini kocha Mwingereza Stewart Hall tayari ameandaa mbinu zitakazowawezesha kuvuka hatua hiyo na kitinga fainali.

“Mchezo utakuwa mgumu kutokana na ubora wa timu ya Mwadui, lakini benchi la ufundi chini ya kocha Hall tayari limeandaa mbinu za kimchezo zitakazosaidia kupatikana ushindi ambao utatuwezesha kusonga mbele na kupata nafasi ya kuiwakilisha tena nchi katika Kombe la Shirikisho Afrika,” alisema.

Alisema wachezaji wamechoshwa na safari ndefu ya kutoka Tunisia lakini hali hiyo haiwezi kuwagharimu na kusababisha kupoteza mchezo huo muhimu kwani akili zimeelekezwa katika pambano hilo.

“Safari ni ndefu sana kutoka Tunisia hadi kufika Mwanza, wachezaji watafika wamechoka kwani watalazimika kupumzika siku moja kusubiri kuingia uwanjani Jumapili, ni lazima tukamilishe ratiba kama ilivyopangwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF),” alisema.

Jaffar alisema baada ya kutolewa kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho watapambana kuhakikisha wananyakua ubingwa wa Kombe la FA na Ligi Kuu Tanzania Bara.

Azam ambayo iliwakosa nyota wake kadhaa katika mchezo dhidi ya Esperance, sasa inatarajia kumtumia mshambuliaji Kipre Tchetche na mlinzi Pascal Wawa baada ya afya zao kuimarika.

Lakini timu hiyo itaendelea kumkosa beki Shomari Kapombe anayeendelea kupatiwa matibabu kutokana na maumivu ya mbavu yanayomsumbua na Farid Mussa ambaye anakwenda kwenye majaribio katika klabu za Union Deportiva Las Palmas na Malaga za nchini Hispania.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles