25.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 8, 2024

Contact us: [email protected]

ACT-Wazalendo: Tutaungana na Chadema uchaguzi mkuu

MWANDISHI WETU

CHAMA Cha ACT-Wazalendo kimesema kipo tayari kuungana na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Mwezi Oktoba mwaka huu.

Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Ado Shaibu wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi zake ndogo zilizopo Magomeni jijini Dar es Salaam jana ambapo alisema kuwa wanahitaji ushirikiano wa vyama vya upinzani vyenye malengo thabiti ya kukiondoa Chama Cha Mapinduzi (CCM) madarakani na kuleta mabadiliko kwenye maisha ya wananchi.

Shaibu alisema tayari wamekiandikia barua Chadema kuhusu nia ya chama chake kuunga mkono juhudi zozote za kuunganisha nguvu katika uchaguzi huo ambao unasubiriwa kwa hamu kubwa na Watanzania walio wengi.

“Mara baada ya Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika kutangaza kufungua milango ya ushirikiano wa vyama, siku iliyofuata nilimwandikia barua ya kupokea hatua hiyo kwa mikono miwili na kuonyesha utayari wa ACT-Wazalendo katika suala hilo muhimu.

“Tunajua CCM haipendi umoja wa vyama vya upinzani, itafanya kila njia kutugawanya, na sisi ACT Wazalendo tupo tayari kwa umoja na tutalisimamia hilo kwa nguvu zote”alisema Shaibu.

Aidha mapema wiki iliyopita, Chadema kupitia kwa Katibu Mkuu wake, John Mnyika kilitangaza kukaribisha majadiliano ya ushirikiano na vyama vinavyotaka kushirikiano nacho.

Mnyika alisema Chadema kinafungua milango miwili muhimu kuelekea uchaguzi mkuu wa 2020, ambapo aliutaja mlango wa kwanza kuwa wanaufungua kwa watia nia wote wa urais na mlango mwingine niwa majadiliano na vyama ambavyo vina dhamira ya kweli ya kushirikiana katika uchaguzi huo.

“Dhamira hii inahusu ngazi zote kuanzia udiwani, uwakilishi, ubunge na urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tukifikia makubaliano tutaeleza uamuzi wowote ambao tutakuwa tumeufikia.

“Marekebisho ya sheria ya vyama vya siasa kuliingizwa vifungu vinavyohusu ushirikiano na kuna masharti ya muda wa kupeleka mkataba kwa msajili na masuala mengine kadhaa, hivyo tutakapokaa na wenzetu ambao tumefungua milango ya majadiliano watakaokuwa tayari kutumia hii fursa ya pamoja tutaona ni namna gani ya ushirikiano inayowezekana katika mazingira ya sasa”alisema Mnyika.

Aidha katika hatua nyingine, mwishoni mwa wiki Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu aliwaomba wanachama wa chama hicho kuanza kutangaza nia ya kugombea urais kumkabili mgombea wa CCM visiwani humo.

Hata hivyo, Shaibu alipoulizwa endapo ushirikiano huo utafanikiwa baada ya Chadema kuwataka wanachama wake kutangaza kugombea urais kwa upande wa Zanzibar, alisema hilo halina tatizo kwa sababu chama chochote cha siasa kina haki ya kujiandaa na uchaguzi ikiwemo kuandaa wagombea wa ngazi zote, sehemu yoyote ya nchi ikiwemo Zanzibar.

Hata hivyo hatua hiyo inaelezwa na wadadisi wa mambo ya siasa kuwa kama Chadema kitasimamisha mgombea wa urais Zanzibar, basi ushirikiano wake na ACT–Wazalendo utakuwa shakani.

Wadadisi hao wanakwenda mbali zaidi wakiwa na mtazamo kwamba katika muktadha wa kisiasa uliopo sasa ambapo ACT- Wazalendo kina nguvu na ngome kubwa Zanzibar huku Chadema kikiwa kimejikita zaidi Tanzania bara kwa kiasi kikubwa.

Wanasema ushirikiano wowote wa vyama hivyo viwili kunaweza kuwa tishio kubwa kwa CCM katika pande mbili bara na visiwani kama ilivyokuwa kwa Muungano wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) mwaka 2015 ambapo vyama vinne viliungana na kusimamisha mgombea mmoja wa urais wakati huo, Edward Lowassa.

Vyama vilivyounda Ukawa ni Chadema, NCCR-Mageuzi, CUF na NLD.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles