25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Waziri atishia kufunga kiwanda kwa unyanyasaji

JenistaNa GUSTAPHU HAULE, PWANI
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Walemavu, Jenister Mhagama, juzi aligeuka mbogo na kutaka kukifungia kiwanda cha kutengeneza yeboyebo kiitwacho Unfly Trading, kilichopo wilayani Mkuranga, Mkoa wa Pwani.

Mhagama alitaka kuchukua hatua hiyo baada ya kupata taarifa kwamba viongozi wa kiwanda hicho wanawanyanyasa wafanyakazi wao.

Kabla ya kutaka kuchukua uamuzi huo, Ofisa Rasilimali Watu kiwandani hapo, Denis Steven, alimwambia waziri huyo kwamba kiwandani hapo hakuna mgogoro wa wafanyakazi na kumfanya waziri huyo kuitisha mkutano wa dharura wa wafanyakazi wote.

Katika mkutano huo, baadhi ya wafanyakazi walisema uongozi wao unawafanyia vitendo vya kikatili na hivyo kuitaka Serikali iwasaidie kuvitatua.

Katika maelezo yao, walisema wanafanya kazi bila kupumzika, hawana mikataba ya ajira, hawapewi fedha za chakula na wanaoumia kazini hufukuzwa bila malipo yoyote.

Baada ya maelezo hayo na mengine, Waziri Mhagama alisema Serikali haiko tayari kuona wananchi wakinyanyaswa na kwamba anaweza kukifunga kiwanda hicho kama uongozi utaendelea kuwanyanyasa wafanyakazi wao.

Pamoja na hayo, alimwagiza ofisa rasilimali watu huyo, kutoa mikataba ya ajira kwa wafanyakazi wote ndani ya wiki moja kabla hajawachukulia hatua.

Naye Mbunge wa Mkuranga, Abdallah Ulega (CCM), alionyesha kusikitishwa na mwenendo wa kiwanda hicho kwa kuwa amewahi kupata malalamiko kutoka kwa wafanyakazi kiwandani hapo.

“Mheshimiwa waziri, ndani ya kiwanda hiki kuna matatizo ya watu kukatika vidole na wengine kufa, lakini hakuna msaada unaotolewa zaidi ya kuwafukuza kazi.

“Kwa kuwa leo umekuja, nimefarijika na ujio wako na naomba hatua za haraka zichukuliwe ili kuokoa vijana hawa,” alisema Ulega.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles