30.2 C
Dar es Salaam
Sunday, September 25, 2022

ZUMA ATAJWA KUUNDWA CHAMA KIPYA

JOHANNESBURG, AFRIKA KUSINI

KUNDI la wanasiasa na wafuasi wengine wa Rais mstaafu wa Afrika Kusini, Jacob Zuma, wameanza mikakati ya kuanzisha chama kipya cha siasa kwa lengo la kukidhoofisha chama tawala cha ANC pamoja na kuhakikisha kuwa kiongozi huyo wa zamani anarejea madarakani.

Kwa mujibu wa mtandao wa gazeti la Mail and Guardian la nchini humo, nyendo za kundi hilo limepanga pia kumdhoofisha rais wa sasa wa nchi hiyo, Cyril Ramaphosa, ikiwa ni mbinu ya kuibuka na ushindi kwenye uchaguzi mkuu mwakani.

Mail and Guardian limesema linazo taarifa za mnyukano wa makundi mawili ndani ya Kamati Kuu ya chama cha ANC kati ya lile linalomuunga mkono Rais Ramaphosa na Jacob Zuma.

Kundi linalomuunga mkono Zuma linaitwa Mazibuyele Emasisweni ambalo linajumuisha viongozi wa dini, wafanyabiashara, viongozi wa jadi na madereva teksi, wamepania kuzindua chama kipya cha African Transformation Congress (ATC) siku chache zijazo na kudai kuwa na wanachama milioni 6.8.

Mmoja wa wanachama wa kundi hilo ni Frank Fakude, amebainisha kuwa wanachama wao wanafahamu katiba ya chama hicho kipya kitakachoanzishwa. Kundi hilo limekuwa likimuunga mkono Zuma tangu alipoondolewa madarakani na limesisitiza kuzungumza na kiongozi huyo wa zamani kwa lengo la kuidhinisha mpango wa kuanzisha chama kipya.

“Tumekutana na Zuma, tunamwelewa anamaanisha na ana msimamo kwamba, Ramaphosa hapaswi kuungwa mkono kwa sababu yuko njia moja na wazungu wachache,” amesema mratibu mmoja wa kundi linalomuunga mkono Zuma.

Aidha, kundi hilo limedhamiria kuendesha maombi katika miji ya Nkandla na KwaZulu-Natal, ikiwa ni njia ya kuonyesha mshikamano miongoni mwao.

Nalo gazeti la Sunday Times liliwahi kuripoti kuwa Askofu Caesar Nongqunga, ambaye ni kiongozi wa Kanisa la Twelve Apostles Church na rafiki wa Zuma, wamepanga kukisajili chama cha ATC na kuhakikisha kinashiriki uchaguzi mkuu ujao. Chama cha ATC kinatajwa kushirikiana na kundi la Black First Land First kama njia ya kumng’oa madarakani Ramaphosa.

Hata hivyo, taarifa kutoka watu wa karibu wa Zuma zimesema kiongozi huyo amekanusha uvumi huo na kusisitiza kuwa wale wote wanaodhani ataanzisha chama kipya hawana ufahamu wa kutosha kuhusiana na harakati zake za kisiasa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
201,896FollowersFollow
553,000SubscribersSubscribe

Latest Articles