26.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

Zitto: Sheria ya mafuta, gesi imekiukwa

Na FREDRICK KATULANDA-DODOMA

MBUNGE wa   Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, amesema sheria ya mafuta na gesi iliyotungwa mwaka 2015  mpaka sasa haijatekelezwa.

Akizungumza kwenye kongamano lililoandaliwa na Asasi ya HakiRasilimali, Zitto alisema  sheria ya usimamizi wa fedha za Mafuta na Gesi Na. 22 ya mwaka 2015  kifungu cha 8 inaitaka serikali kuanzisha mfuko maalumu wa fedha za sekta hiyo.

Mbunge huyo alisema bado sheria hiyo haijatekelezwa na Serikali imekuwa ikitumia fedha za gesi kinyume cha sheria.

Alisema Serikali ilipaswa kufungua akaunti ya mfuko huo maalumu Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa ajili ya kutunza fedha hizo.

Hata hivyo, alisema  tangu ipitishwe hadi leo Serikali haijafungua akaunti hiyo wala fedha hizo hazijakaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kama kifungu cha 14 (3) cha sheria kinavyoagiza.

Mwaka 2015 Bunge lilitunga sheria ya kusimamia fedha za mapato yote ya mafuta na gesi yanayokusanywa na   TPDC na kodi ya mapato inayokusanywa na TRA ili zielekezwe na sheria kwenda kwenye akauti maalumu BoT lakini serikali haijafanya hivyo,” alisema.

Alisema sheria hiyo ilipopitishwa   mwaka 2015 ilielekeza  kuwa kuanzia mwaka wa fedha 2016/17 fedha zote ziende kwenye mfuko huo lakini  tangu mwaka huo hakuna hata senti iliyokwenda huko.

“Nasema hakuna hata senti moja ambayo imekwenda, angalia fedha za TPDC pekee kwa mwaka 2016/17 zilizopaswa kwenda kwenye mfuko huo ni Sh bilioni 158, mwaka 2017/18 Sh bilioni 477.

“Kwenye vitabu vya bajeti ya mwaka 2018/19 zinapaswa kwenda Sh bilioni 394, zote hizi jumla Sh trilioni 1.029 hazijaenda kwenye mfuko na zinatumika bila kufuata sheria,” alisema.

Awali, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu Mstaafu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh, ambaye ni Mkurugenzi wa Asasi ya Wajibu, akizungumza katika kongamano hilo alisema sheria hiyo inapaswa kufanyiwa mabadiliko  iweze kuhusisha na fedha za dhahabu.

“Hatuna mfuko wa fedha za dhahabu, hivyo nadhani sheria hii nzuri inapaswa kuangaliwa na kufanyiwa mabadiliko  iweze kuelekeza kuwapo  mfuko kwa fedha za dhahabu,” alisema.

Meneja Mkazi wa Kanda ya Afrika Mashariki wa Shirika la Kufuatilia Usimamizi wa Rasilimali za Asili (NRGI), Silas Olang, alisema sheria hiyo inao utaratibu mzuri wa namna ya kuingiza fedha za gesi kwenye mfuko pamoja na zile za mafuta kama yakipatikana lakini bado inapaswa kuangaliwa.

“Sheria hii inapaswa kufanyiwa mabadiliko  iweze kuangalia madini yote kwa kuwa dhahabu pia inapaswa kuwekewa mfuko kama huo,” alisema.

Zitto alipinga hoja hizo na kusema kati ya sheria ambayo ilitungwa na yenye nguvu ambayo inaizuia serikali kutumia fedha zake zaidi ya ukomo ni hiyo, hivyo alionya iwapo itapelekwa bungeni kwa mabadiliko serikali itaondoa ukomo wa matumizi yake.

“Hii sheria inataka iwapo serikali ikitaka kuzitumia fedha za mfuko huo zaidi ya kiwango kilichopangwa italazimika kuliomba Bunge ambalo litapiga kura na theluthi mbili  wakubali, ukipelekea bungeni wataiondoa na hiyo hawa serikali,” alisema.

Alisema kwa sasa sheria hiyo ni nzuri hivyo aliwaomba wabunge wa vyama vyote na asasi za raia pamoja na wananchi kuibana serikali iweze kutekeleza sheria hiyo na siyo kuifanyia mabadiliko.

Alisema serikali inapaswa kuitekeleza sheria kwa kuwa tangu mwaka 2016/17 wamekuwa wakikwepa kuitekeleza kwa kuweka fedha katika akaunti maalum BoT kwa kuwa wakiziweka huko hawatazitumia.

Zitto alisema bunge la sasa  halina nguvu kama la (Bunge la 9) Mwakyembe, Dk. Slaa ambalo lilikuwa na meno.

Alisema kudai sheria hiyo irudishwe bungeni itaipa mwanya serikali kuondoa vifungu vikwazo kwa kuwa imeibana  serikali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles