26 C
Dar es Salaam
Saturday, February 4, 2023

Contact us: [email protected]

Yanga yaua, kutimkia Pemba

yng*Azam yashindwa kuzoa pointi 3 Kirumba

NA JENNIFER ULLEMBO, DAR ES SALAAM

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga jana walifanikiwa kuchomoza na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Kagera Sugar katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam huku Azam FC wakiambulia sare ya bao 1-1 mbele ya Toto Africans.

Ushindi wa jana kwa Yanga umewawezesha Wanajangwani hao kufikisha pointi 53 ikiwa ni tofauti ya pointi nne nyuma ya vinara wanaoongoza katika msimamo wa ligi hiyo, Simba waliojikusanyia pointi 57 baada ya kushuka dimbani mara 24.

Baada ya ushindi wa jana, uongozi wa Yanga umepanga kuipeleka timu hiyo Pemba kujiandaa na mchezo wa kwanza raundi ya pili Klabu Bingwa Afrika dhidi ya Al Ahly ya Misri itakayochezwa Jumamosi hii jijini Dar es Salaam.

Katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, Azam FC kwa mara nyingine walishindwa kuweka rekodi ya kupata ushindi kwenye uwanja huo na kujikuta wakipunguzwa kasi kwenye mbio za kuwania ubingwa msimu huu.

Kwa matokeo ya jana, Yanga wamebaki nafasi ya pili kwa kufikisha pointi 53 wakifuatiwa na Azam waliopo nafasi ya tatu kwa kujikusanyia pointi 51 wote wakiwa wamecheza michezo 22 na kubakiwa na mechi mbili za viporo kila mmoja ili kuwafikia vinara Simba waliocheza mara 24.

Mabao yaliyoipa ushindi muhimu Yanga yalipachikwa wavuni na mshambuliaji, Donald Ngoma dakika ya 25, Amissi Tambwe dakika ya 62 na Haji Mwinyi dakika ya 89.

Katika mchezo wa jana Kagera walianza kwa kasi kwa kulishambulia lango la Yanga na dakika ya nane walifanikiwa kuandika bao la kuongoza lililofungwa na Mbaraka Yusuph, aliyemalizia pasi ndefu iliyopigwa na beki, Salum Kanoni.

Bao hilo liliwazindua Yanga na kufanikiwa kusawazisha dakika ya 25 kupitia kwa Ngoma aliyefunga kwa kichwa akiunganisha vema mpira wa krosi iliyochongwa na Juma Abdul.

Yanga waliendeleza mashambulizi langoni mwa Kagera ambapo dakika ya 34 mwamuzi, Erick Unoka, kutoka Arusha alitoa penalti kwa Wanajangwani hao baada ya Ngoma kuangushwa ndani ya eneo la hatari na beki wa Kagera, Shaban Ibrahim.

Beki wa Yanga, Kelvin Yondani, alipiga penalti hiyo na kukosa baada ya kipa wa Kagera, Andrew Ntala kuwa makini langoni na kuidaka kwa urahisi.

Timu zote zilikwenda mapumziko zikiwa zimefungana bao 1-1 na kipindi cha pili kilianza kwa Kagera kufanya mabadiliko ya kumtoa Martin Lupart dakika ya 53 na nafasi yake kuchukuliwa na Ibrahim Job.

Dakika ya 55, Salum Telela, alikosa bao la wazi akiwa ndani ya eneo la hatari ambapo kipa wa Kagera alianguka katika harakati za kuokoa lakini alipiga shuti hafifu ambalo lilitoka pembeni ya lango.

Kagera walifanya mabadiliko mengine dakika ya 59 ya kumtoa Paul Ngwai na kumuingiza Iddi Kurachi huku Yanga wakimtoa Deus Kaseke na nafasi yake kuchukuliwa na Godfrey Mwashiuya.

Mabadiliko hayo yalizaa matunda kwa Yanga ambapo dakika ya 62, Tambwe aliandika bao la pili kwa kuachia shuti kali lililojaa moja kwa moja wavuni baada ya kutengenezewa pasi ndefu na Simon Msuva.

Dakika ya 69 Kagera walimtoa Mbara Yussuf na kumuingiza Ramadhan Kipalamoto huku Yanga wakimtoa Tambwe dakika ya 78 na nafasi yake kuchukuliwa na Paul Nongwa.

Yanga waliendelea kunufaika na mabadiliko yaliyofanywa na kufanikiwa kufunga bao la tatu dakika ya 89 kupitia kwa Mwinyi aliyemalizia kwa kichwa mpira wa kona iliyochongwa na Msuva.

Kwa upande wa Azam bao lilifungwa na mshambuliaji, John Bocco kwa kichwa dakika ya 23 akiunganisha krosi iliyopigwa na Khamis Mcha huku Toto Africans wakisawazisha dakika ya 40 kupitia kwa Waziri Juma.

Katika mechi nyingine za ligi hiyo, Stand United waling’ara katika uwanja wao wa nyumbani wa Kambarage, Shinyanga baada ya kuchomoza na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mgambo Shooting kutoka Tanga.

Maafande wa JKT Ruvu walitamba katika Uwanja wa Mabatini, Mlandizi baada ya kuichapa African Sports ya Tanga bao 1-0 huku Tanzania Prisons wakitoka suluhu ugenini dhidi ya Ndanda FC katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,471FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles