25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

YANGA ITAITUMIA ALLIANCE KUJITIBU?

Theresia Gasper -Dar Es Salaam

LIGI Kuu Tanzania Bara, inatarajia kuendelea leo kwa michezo tisa kupigwa kwenye viwanja tofauti.

Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, mabingwa wa kihistoria wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga itaikaribisha Alliance Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Yanga yenye rekodi ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu mara 27, itaumana na wageni wao Alliance ikiwa na kumbukumbu ya mbaya  ya kuvuna sare  nne kupitia michezo yake minne mfululizo iliyopita.

Ilianza na sare ya bao 1-1 na Mbeya City, Uwanja wa Taifa, ikatoka suluhu na Tanzania Prisons 0-0,  ikabanwa  sare ya bao 1-1 na Polisi Tanzania 1-1 kabla ya kutoka suluhu na Coastal Union.

Matokeo hayo yalikuwa kama sindano ya ‘ sumu’ kwa mashabiki wa Yanga, kwani wanaamini yameipa Simba ambayo ni mpinzani wao mkuu tiketi ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu.

Hata hivyo ushindi wa bao 1-0 dhidi ya timu ya Daraja la Kwanza ya Gwambina ya Wilayani  Misungwi mkoani Mwanza, kwa kiasi fulani umewapa faraja mashabiki wa Jangwani.

Ikumbukwe kuwa, ushindi huo uliifanya Yanga kufuzu robo fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho(ASFC), ambayo bingwa wake ataiwakilisha Tanzania katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Kwakukukumbusha, kama Simba atafanikiwa kweli kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu, maana yake ni kwamba ataiwakilisha Tanzania katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika,  fursa itakayobakia kwa Yanga na timu nyingine kucheza michuano ya kimataifa ni ubingwa wa ASFC.

Kwa upande mwingine,  Alliance  yenye maskani yake  jijini Mwanza itaingia Uwanja wa Taifa ikiwa imetoka kuvuna sare ya bao 1-1 dhidi ya Singida United, mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Nyamagana.

Timu hizo zilipokutana katika mzunguko wa mzunguko wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Kirumba, Mwanza,  Yanga ilishinfa mabao 2-0.

Yanga inashika nafasi ya nne katika msimamo wa ligi hiyo, ikijikusanyia pointi 41, katika michezo 22 iliyoshuka dimbani, ikishinda 11,  sare nane na kupoteza tatu.

Alliance yenyewe ipo  nafasi ya 13 miongoni mwa timu 20 zinazoshiriki ligi hiyo ikiwa na pointi 29, baada ys kushuka dimbani mara 24.

Wachezaji wa Yanga wanafahamu kwamba wanahitaji ushindi tu na si kingine katika mchezo huo ili kuwapa raha mashabiki wao ambao siku za karibuni wamekuwa na presha kubwa.

Mchezo  huo unatarajiwa kuwa wa ushindani kutokana na kuikutanisha Yanga inayohitaji matokeo mazuri ili kutibu nafsi za mashabiki wake na Alliance inayoundwa na wachezaji wengi wenye umri mdogo wanaocheza soka la kufundishwa.

Miamba mingine katika ligi hiyo, timu ya Azam itakuwa mgeni wa JKT Tanzania, mchezo utakaochezwa Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.

JKT Tanzania inatumia uwanja huo kwa michezo yake ya nyumbani, tangu Makao Makuu ya Jeshi la Kujenga  Taifa(JKT), yalipohamisha makao makuu ya nchi, yaani Dodoma.

Kabla ya kuhamia Dodoma, maskani ya JKT Tanzania yalikuwa jijini Dar es Salaam, ambapo timu hiyo ilikuwa chini ya JKT Makao Makuu.

Katika mchezo huo, Azam yenye maskani yake eneo la Chamazi jijini Dar es Salaam, itaingia uwanjani ikiwa na jeraha, baada ya kuchapwa bao 1-0 na Namungo, katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Majaliwa,  Lindi.

Vipute vingine leo, Mwadui itapepetana na Coastal Union  ya Tanga kwenye uwanja wake wa nyumbani wa Kambarage,  Shinyanga.

Singida United itaikaribisha Polisi Tanzania,  Uwanja wa Liti mjini  Singida, Kagera Sugar itapimana ubavu na Tanzania Prisons, Uwanja wa Kaitaba, Kagera.

Ruvu Shooting itakuwa mwenyeji wa Mbao, dimba la Mabatini mkoani Pwani, Lipuli itakuwa nyumbani Uwanja wa Samora mjini Iringa kutoana jasho na Namungo.

Biashara United itakuwa nyumbani kupepetana na Mbeya City,  dimba la Karume mjini Msoma, Mtibwa Sugar itaikaribisha Ndanda, Uwanja wa CCM Gairo mjini Morogoro.

Akizungumzia mchezo huo, Kocha Mkuu wa Yanga, Luc Eymael alisema amerekebisha kasoro alizozibaini kwenye michezo yao iliyopita, hivyo anaamini leo wataonja radha ya pointi tatu.

“Nafahamu mchezo utakuwa mgumu lakini mipango yetu ni kushinda mchezo wa kesho na kuvuna pointi tatu na kusogea juu ya msimamo wa ligi,” alisema.

Naye Kocha Mkuu wa Alliance, Fredy Minziro alisema anaiheshimu Yanga kwakua ni timu kubwa lakini hiyo haimaanishi wamekuja Dar es Salaam kutalii zaidi ya kupiga ia pointi tatu.

“Tumekuja Dar es Salaam tukiwa tumefanya maandalizi ya kutosha, lakini tunaiheshimu Yanga na hili litatufanya kuingia uwanjani na tahadhari,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles