26.2 C
Dar es Salaam
Saturday, August 13, 2022

Wizara ya Ardhi, Viwanda matatani

Mwandishi Wetu-Dar es Salaam

  • Zaingia katika mtego wa JPM kwa kuzungusha wawekezaji

MABALOZI wameanza kuitikia wito wa Rais Dk. John Magufuli kumpelekea taarifa za watendaji wanaokwamisha wawekezaji wakiziweka kitanzini  Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Wizara ya Viwanda na Biashara.

Aprili 9 akiwa ziarani mkoani Njombe, Rais Magufuli aliwataka mabalozi kupeleka kwake watendaji wa Serikali wanaozungusha wawekezaji ili naye awazungushe kama tairi.

Jana Rais Magufuli alitoa wiki moja kwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Wizara ya Viwanda na Biashara kukamilisha taratibu za uwekezaji kwa Kampuni ya Sugar Investment Trust (SIT) ya Mauritius ambayo imecheleweshwa kuwekeza katika uzalishaji wa sukari tangu mwaka 2017.

Taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais – Ikulu, Gerson Msigwa, ilisema Rais Magufuli alitoa agizo hilo jana Dar es Salaam baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti wa kampuni hiyo, Gansam Boodram aliyeongozana na Balozi wa Mauritius nchini, Jean Pierre Jhumun.

Katika mazungumzo hayo, Boodram alimweleza Rais Magufuli kuwa yupo tayari kulima ekari 25,000 za mashamba ya miwa kwa ajili ya uzalishaji wa sukari na kwamba uwekezaji huo utawezesha kuzalisha tani 125,000 za sukari, ajira za kudumu 3,000 na ajira za muda 5,000.

Alisema licha ya mafanikio hayo tarajiwa, amekwama kuendelea kutokana na kusubiri majibu ya Serikali kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuhusu upatikanaji wa eneo la uzalishaji wa miwa na ujenzi wa kiwanda cha sukari.

Kutokana na maelezo hayo, Rais Magufuli aliagiza ufanyike uchambuzi wa haraka katika maeneo ya Bonde la Mto Rufiji mkoani Pwani, eneo la shamba la Mkulazi mkoani Morogoro na eneo la Kibondo mkoani Kigoma ili mwekezaji huyo apatiwe na kuanza mara moja uwekezaji kwa kuwa nchi inahitaji kuongeza uzalishaji wa sukari utakaomaliza upungufu wa tani zaidi ya 100,000 ambazo kwa sasa zinaagizwa kutoka nje ya nchi.

Taaarifa hiyo pia ilieleza kuwa Rais Magufuli alimwagiza Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dk. Edward Mhede, kufuatilia makubaliano ya ushirikiano katika uvuvi kati ya Tanzania na Mauritius ambayo hayajatiwa saini tangu 2017 licha ya wawekezaji wa nchi hiyo kuonesha nia ya kutaka kuwekeza katika uvuvi na viwanda vya samaki.

Balozi Jhumun alimweleza Rais Magufuli kuwa Mauritius inao uzoefu mkubwa katika uvuvi na viwanda vya samaki na kwa kuitikia wito wake wa kuhamasisha wawekezaji kuja hapa nchini, amefanikiwa kupata kampuni zilizo tayari kufanya uwekezaji huo baada ya makubaliano kati ya nchi hizo kutiwa saini.

 Rais amezionya taasisi za Serikali kikiwemo Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kwa kutoharakisha taratibu za kuwawezesha wawekezaji kuwekeza na amemhakikishia Balozi Jhumun kuwa atafuatilia kuhakikisha uwekezaji wa Kampuni ya SIT unafanyika.

“Ndugu zangu watendaji wa Serikali badilikeni, acheni kukwamisha wawekezaji, fanyeni maamuzi na kama yanawashinda toeni taarifa kwenye mamlaka za juu,” alisema Rais Magufuli.

AGIZO LA KWANZA

Aprili 9, Rais Magufuli aliwaweka kitanzini watendaji wa Serikali wanaokwamisha wawekezaji, huku akitaka mabalozi kuwapeleka kwake watendaji wanaowazungusha wawekezaji ili naye awazungushe kama tairi.

Alisema ili kuvutia wawekezaji, aliihamishia TIC katika Ofisi ya Waziri Mkuu, lakini akiona huko pia wanasuasua atairudisha Ofisi ya Rais ili mtu akifika leo akitaka kuwekeza, kesho apate anachotaka.

Akizungumza katika uzinduzi wa kiwanda cha kuchakata majani ya chai cha Ruangu mkoani Njombe, Rais Magufuli alisema watendaji katika maeneo hayo muhimu wamekuwa kikwazo na kusababisha wawekezaji kukimbilia nchi jirani.

Alisema kwa upande mmoja, masharti magumu ya uwekezaji nchini yamekuwa kikwazo kwa uwekezaji, hivyo ni vyema masharti hayo yapunguzwe.

“Kumekuwa na masharti magumu ya uwekezaji, wawekezaji wengi wanakimbilia nchi jirani kwa sababu ya urasimu na vi-masharti vya hovyo vimekuwa vingi. Tunajichelewesha wenyewe.

“Unakuta mwekezaji anakuja kuwekeza nchini, mara wanaanza kutokeza watu wa mazingira wanakuja na yao wakati mazingira ya Mungu yapo, mara wanakuja Osha sijui wanataka kuosha uso au nini. Mimi sasa ndiyo Rais na ninasema wawekezaji ukipata tu kiwanja anza kujenga, hayo mambo mengine yatakuja baadaye,” alisema.

Alisema tatizo lililopo ni kwa watendaji kuwa na ‘vichwa kama kamongo’, hawafai na wamekuwa tatizo katika uwekezaji, kwa kuwafanya wawekezaji kuwa maadui zaidi ya kuwafanya marafiki.

Rais Magufuli aliwataka mabalozi wa nchi za nje kuwasiliana naye moja kwa moja iwapo kuna wawekezaji kutoka katika nchi zao ambao wanazungushwa wanapofika nchini, ili aweze kuwashughulikia watendaji wanaowasababishia urasimu.

“Ninawaambia mabalozi kama kuna wawekezaji wanataka kuwekeza nchini na wakazungushwa zungushwa, waleteni kwangu ili na mimi niwazungushe hao watumishi, nitajua nitawazungusha kama tairi au nini,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,625FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles