20.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, September 28, 2022

WIZARA TANO ZAONJA JOTO LA JIWE


MAREGESI PAUL NA GABRIEL MUSHI -DODOMA/DAR ES SALAAM       |

WAKATI Bunge la Bajeti likiendelea na vikao vyake vya kujadili makadirio ya mapato na matumizi ya wizara mbalimbali kwa mwaka wa fedha 2018/2019, hali imekuwa tofauti kwa wizara tano pindi zilipowasilisha bajeti zake katika siku za hivi karibuni.

Bajeti za Wizara ya Kilimo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, zilipita kwa ‘mbinde’ baada ya wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wale wa upinzani kuungana kuzipinga kwa hoja zenye mashiko.

Kimsingi ni nadra kwa wabunge wa CCM kupinga bajeti za wizara, lakini hali imekuwa tofauti baada ya baadhi yao wakiwamo Nape Nauye (Mtama) na Husein Bashe (Nzega Mjini) kuonekana vinara kuzikosoa.

Pamoja na hoja ya kuzipinga na kuwapo tishio la kuzikwamisha, lakini bajeti hizo zilipitishwa licha ya kwamba wabunge hao walisema hawatakuwa tayari kuziunga mkono kwa sababu Serikali haionyeshi nia ya dhati ya kuwasaidia wakulima, wafugaji na wavuvi ambao ni sehemu ya wachangiaji wakubwa wa pato la taifa.

Lakini wabunge hao waliotishia kuikwamisha, hawakuonyesha tena makali yao tofauti na ilivyotarajiwa kupitia michango yao na hatimaye Bunge lilipitisha bajeti hizo licha ya malalamiko mengi yaliyokuwapo awali.

Akizungumzia hilo, Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea (Chadema), aliliambia Bunge kwamba hakuna mbunge yeyote wa CCM mwenye uwezo wa kuzuia bajeti isipite kwa sababu kila wanapoonyesha nia ya kuikwamisha huitwa na kudhibitiwa katika vikao vyao vya wabunge wa chama hicho.

Pia Kubenea alienda mbali zaidi kwa kusema kama angetokea mbunge yeyote wa chama hicho ambaye angekwamisha bajeti hiyo, angekuwa tayari kuliomba Bunge lisimlipe mshahara wake wa mwezi huu ili fedha hizo zikasaidie jamii majimboni.

Alisema wabunge wa CCM hawana uwezo wa kusimamia misimamo yao hadi mwisho kwa kuwa kuna kawaida hoja zao kudhibitiwa. 

WIZARA YA KILIMO

Pamoja na mambo mengine, dalili za mambo kuwa magumu zilionekana mapema wiki hii wakati wabunge wakijadili bajeti iliyowasilishwa na Waziri wa Kilimo, Dk. Charles Tizeba.

Dk. Tizeba aliwasilisha bajeti hiyo akiomba kuidhinishiwa Sh bilioni 170.2 kwa mwaka wa fedha 2018/2019 ikiwa ni pungufu kwa asilimia 23, ikilinganishwa na mwaka 2017/2018 iliyokuwa Sh bilioni 221.

Licha ya bajeti hiyo kupita, Tizeba alipata wakati mgumu, huku akilazimika kunyofoa baadhi ya vifungu vilivyoibua utata wakati Bunge lilipoketi kama Kamati ya Matumizi.

Akichangia, Nape, alisema kuna kila sababu bajeti hiyo kuondolewa bungeni kwa kuwa idadi kubwa ya wabunge walioichangia hawaiungi mkono.

“Nikiikubali bajeti hii, wananchi wa korosho, mbaazi, ufuta, pamba na wengineo watanishangaa.

“Pamoja na hayo, naangalia ilani ya CCM ambayo baadhi yetu hawataki tuinukuu, naona inapingana na bajeti hii. Kwahiyo, tuishauri Serikali irudi mezani, iende ikaipitie upya na kuweka vipaumbele vya wananchi,” alisema Nape.

Kwa upande wake, Bashe, aliungana na Nape na kutaka bajeti hiyo iondolewe bungeni kupitia kanuni ya 69 ili Dk. Tizeba na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, wakakae na kuona jinsi ya kuiboresha.

“Sisi wabunge hasa wa CCM, tuna wajibu wa kuwalinda wakulima wakiwamo wa mahindi, pamba, wafugaji wa ng’ombe na wavuvi wa samaki, lakini sisi ndio tunaowanyanyasa,” alisema.

Mbunge wa Babati Mjini, Pauline Gekul (Chadema), alisema Serikali haiwezi kufanikiwa katika suala la viwanda kwa sababu imeshindwa kuimarisha sekta ya kilimo.

Kutokana na mvutano huo, Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Zungu, alilazimika kuiagiza Kamati ya Bunge ya Bajeti, ikutane na wabunge wawili wa CCM, waliotishia kukwamisha bajeti hiyo.

Zungu alifikia hatua hiyo baada ya Nape na Bashe, kutishia kuikwamisha kutokana na kutoridhishwa na majibu ya Dk. Tizeba kuhusu sekta ya kilimo. 

WIZARA YA MIFUGO NA UVUVI

Baada ya Dk. Tizeba kuwekwa kikaangoni, ilifuata zamu ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina, aliyewasilisha bajeti yake na kuliomba Bunge kuidhinisha Sh bilioni 56.45 kwa mwaka 2018/2019.

Mpina alisema fedha za maendeleo za wizara hiyo kwa mwaka 2017/18 hadi kufikia Aprili, mwaka huu zilikuwa hazijapokewa.

Bajeti hiyo ya mwaka 2017/2018 inatakayomalizika Juni, mwaka huu iliidhinishiwa Sh bilioni sita kwa miradi ya maendeleo.

Kama ilivyokuwa kwa Wizara ya Kilimo, wabunge wa CCM na upinzani walichachama na kuitaka Serikali iondoe bajeti hiyo kwa kuwa imejaa kasoro.

Pia baadhi waliikosoa operesheni za uvuvi haramu ikiwamo sangara na namna inavyotumika vibaya kuwatenda wavuvi mithili ya watumwa ndani ya nchi yao.

Tishio hilo lilianza kuwekwa na Mbunge wa kuteuliwa, Abdallah Bulembo.

Katika maelezo yake, Bulembo alimlalamikia Mpina kwamba kupitia operesheni za kukabiliana na wavuvi haramu zinazofanyika nchini ikiwamo Operesheni Sangara iliyoko katika Ziwa Victoria, CCM inaweza kuwa na wakati mgumu wakati wa kuomba kura kwa wananchi kuanzia mwakani wakati wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Kwa mujibu wa Bulembo, kinachofanywa na Mpina hakikubaliwi na Serikali ya CCM kwa kuwa hakiko katika ilani ya chama hicho, huku akisema inawezekana waziri huyo anataka wapinzani wakishinde chama chao wakati wa kampeni za kisiasa.

“Hivi kama tunawanyanyasa na kuwadhalilisha wavuvi, CCM tutaombaje kura kwao?” alihoji.

Huku akipigiwa makofi na baadhi ya wabunge wa chama hicho tawala na upinzani, Bulembo, aliitaka Serikali isitishe operesheni hizo kwa sababu washiriki wanawadhalilisha wavuvi kwa kuwapora samaki, kuwachukulia zana zao za uvuvi na kuwanyanyasa kwa njia mbalimbali.

Mbunge mwingine wa CCM aliyetishia kukwamisha bajeti hiyo na kutaka iondolewe bungeni kwa kile alichosema ina kasoro nyingi ni Bashe aliyelalamikia utaratibu wa baadhi ya hoja nzito za wabunge wa chama hicho zinazoonyesha kuikosoa Serikali zimekuwa zikiishia kwenye vikao vya chama chao na katika Kamati ya Uongozi ya Bunge.

Katika maelezo yake, Bashe alitoa mfano jinsi hoja ya Nape ilivyoishia katika kikao cha chama chao baada ya kuitwa na kuhojiwa katika Kamati ya Uongozi ya Bunge.

Mbunge mwingine wa CCM ambaye kabla ya bajeti hiyo kuhitimishwa alionekana kuwa mwiba kupitia uchangiaji wake lakini mwishoni akakaa kimya, ni Goodluck Mlinga wa Ulanga Mashariki.

Kama ilivyokuwa kwa wabunge wenzake, naye alipinga vitendo vya unyanyasaji wanavyofanyiwa wavuvi, lakini akaunga mkono operesheni kufanyika katika Mto Kilombero.

Pia mbunge pekee wa CCM aliyepinga bajeti hiyo na hatimaye kutishia kushika shilingi ya mshahara wa Mpina ni Constantine Kanyasu wa Geita Mjini.

Awali, Kanyasu alisema haungi mkono bajeti hiyo kutokana na udhalilishaji wanaofanyiwa wavuvi katika Ziwa Victoria na akaendelea na msimamo huo hadi bajeti ilipokuwa ikihitimishwa.

Hata hivyo, baada ya kushika shilingi ya mshahara wa Mpina na mjadala kufayika kuhusu hoja yake hiyo, mwishoni aliruhusu bajeti ipitishwe baada ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba, kueleza hatua zitakazochukuliwa na Serikali katika kukabiliana na madhara yanayolalamikiwa kupitia Operesheni Sangara na nyinginezo.

Wakati hayo yakiendelea, Spika wa Bunge, Job Ndugai, alimtaka Mpina ayafanyie kazi malalamiko ya wabunge kuhusu operesheni za kupambana na wavuvi haramu.

Ndugai alisema kama Bunge lingeamua kuunda tume maalumu kuchunguza utekelezaji wa operesheni hiyo, anaamini ingeibua mambo mazito kama ilivyokuwa wakati wa Tume ya Operesheni Tokomeza.

Mbunge wa Viti Maalumu, Dk. Wale Semesi (Chadema), alilalamikia operesheni hiyo na kutaka iundwe tume kuichunguza kwa sababu inaathiri wavuvi kama ilivyofanyika wakati wa Operesheni Tokomeza.

Kwa upande wake, Mpina, alielezea umuhimu wa Operesheni Sangara kutokana na mafanikio yaliyopatikana na kwamba hakuna sababu ya kuisimamisha kwa kuwa imekuwa na mafanikio ya kutosha.

Kwa mujibu wa Mpina, wakati wa operesheni hiyo nyavu haramu 555,431 zilikamatwa, kilo 181,217 za samaki zilikamatwa, kilo 5,147 za mabondo zilikamatwa, pikipiki 269 na magari 564 yalikamatwa.

Pia aliwashangaa wabunge wanaolalamikia operesheni hiyo kwa kuwa pamoja na kulalamika bungeni, hawajawahi kumfikishia malalamiko yao ili ayafanyie kazi.

Alisema wakati wa ziara ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, aliyoifanya wilayani Ukerewe hivi karibuni, hakukuwa na malalamiko kutoka kwa wananchi na wavuvi juu ya operesheni hiyo. 

WIZARA YA MAJI NA UMWAGILIAJI

Aprili 30, mwaka huu ilikuwa zamu ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Isack Kamwelwe kuwekwa kikaangoni baada ya kuwasilisha bajeti ya Sh Sh bilioni 727.3 kwa mwaka 2018/2019 ikiwa ni ongezeko la zaidi ya Sh bilioni 79. Bajeti ya mwaka 2017/2018 ilikuwa Sh bilioni 648.

Licha ya kupitishwa Mei 2, mwaka huu, Kamwelwe, alipata wakati mgumu baada ya wabunge kuendeleza mpango wa kuungana kutaka kukwamisha bajeti ya wizara hiyo iliyojadiliwa kwa siku tatu.

Mpango huo ulidhihirishwa kutokana na mahitaji ya maji kuwa makubwa kwa binadamu hali iliyowalazimu wabunge wote kuweka kando itikadi zao za kisiasa kwa kuungana na kulijadili kwa kina hitaji hilo huku lawama nyingi wakiishushia Serikali kwa kushindwa kuiendeleza miradi ya maendeleo ya maji nchini.

Wabunge hao walieleza kufedheheshwa na ufinyu wa bajeti ya wizara hiyo huku baadhi wakibainisha namna miradi ya maendeleo ya sekta ya maji inavyotafunwa na watoto wa vigogo waliopewa kuitekeleza.

Licha ya ufinyu wa bajeti ya mwaka huu, pia ilibainika katika bajeti inayoishia Julai, mwaka huu utekelezaji wake ulikuwa hafifu kutokana na kiwango kidogo cha fedha kilichotolewa na Serikali na wahisani.

Kwa mujibu wa randama ya bajeti hiyo, wahisani walichangia asilimia 12 pekee ilhali Serikali iliitoa asilimia 38 katika kutekeleza miradi ya maendeleo ya sekta ya maji.

Hali hiyo ililazimu baadhi ya wabunge kuishauri Serikali kuwa iuze ndege zake mbili aina ya Bombardier ili fedha zitakazopatikana ziweze kutumika kutekeleza miradi hiyo.

Wazo hilo lilitolewa na Mbunge wa Kilwa Kusini, Suleiman Bungara (CUF) maarufu kwa jina la Bwege, aliyeonyesha ‘madoido’ kwa kuigiza kulia wakati akichangia mjadala wa bajeti hiyo.

Mbunge wa Kibamba, John Mnyika (Chadema), alimtaka Kamwelwe kuirudisha bajeti hiyo ili ikaandaliwe upya kwa kuwa haitekelezeki.

Mjadala kuhusu sekta ya maji na umwagiliaji iliendelea kupamba moto baada ya Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ali Kessy (CCM), kusema anao ushahidi wa baadhi ya watoto wa viongozi wakubwa waliomilikishwa miradi ya maji katika Mkoa wa Rukwa namna wanavyomshawishi ili asizungumze kuhusu ubadhirifu uliopo katika miradi hiyo.

Alisema kutokana na wakandarasi kupewa miradi ‘kimjomba mjomba’, hali hiyo imesababisha wananchi wa Nkasi kukosa maji na kipindi cha masika huchimba maji kwenye madimbwi kama panya.

Hoja ya kesi iliungwa mkono na Mbunge wa Chemba, Juma Nkamia (CCM), aliyeliomba Bunge kuunda tume maalumu ya Bunge kuchunguza miradi ya maji nchi nzima kwa kuwa kuna ubadhirifu zaidi ya uliokuwa katika mchanga wa dhahabu (makinikia).

Pia alisema baadhi ya miradi ya maji katika jimbo la Chemba amepewa Ofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) hali inayothibitisha namna gani kulivyo na ubadhirifu.

Kutokana na utekelezaji hafifu wa bajeti ya wizara hiyo, wabunge wengi walitaka maelezo kuhusu mkopo wa Sh trilioni 1.1 kutoka Serikali ya India.

Mkopo huo ulitolewa ahadi tangu kipindi cha uongozi wa Serikali ya Awamu ya Nne kwa lengo la kutekeleza miradi ya maji katika miji 17.

Hata hivyo, wakati akijibu hoja hizo, Mpango, alisema tayari Serikali ya India imekubali kutoa mkopo wa Dola za Marekani milioni 500 (Sh trilioni 1.1) kutekeleza miradi ya maendeleo katika sekta ya maji nchini.

Pia bajeti hiyo zilisababisha Mnyika na Ester Bulaya (Bunda) kutimuliwa ndani ya ukumbi wa Bunge.

Hali hiyo ilijiri katika kipindi ambacho Bunge lilikaa kama kamati ambapo Mnyika aliendelea kushikilia msimamo wa kutaka bajeti hiyo iahirishwe.

Kabla ya kuondolewa bungeni kwa amri ya Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, Mnyika alionekana kutokubaliana na uamuzi wa Dk. Tulia kwa kutompa nafasi ya kufafanua hoja yake.

Bulaya naye alitimuliwa muda mfupi baadaye baada ya kuendekeza usumbufu ndani ya Bunge. 

WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI

Kwa mara ya kwanza katika Bunge la bajeti, baadhi ya wabunge wa upinzani wakiongozwa na Godbless Lema na Zitto Kabwe walisusia Bunge na kutoka nje ya ukumbi kwa madai kuwa Zungu anaendesha Bunge kibabe.

Hayo yaliibuka wakati Bunge lilipokaa kama kamati Aprili 27, mwaka huu kupitisha vifungu vya bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Wabunge hao walitoka baada ya Lema kutakiwa kumpatia Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Mwigulu Nchemba, jina la ofisa aliyedai anahusika katika mauaji ya watu.

Lema na wabunge wengine wa upinzani waliondoka bungeni wakidai Zungu anaendesha Bunge bila kufuata kanuni na taratibu kwa kuwanyima wapinzani kujadili masuala muhimu yanayohusu maisha ya wananchi.

Hata hivyo, baada ya wabunge kutoka, Lema alisema baadhi ya wabunge wanaotaka kuzungumza mambo ya msingi wanazuiwa wakiambiwa yamepitwa na wakati.

Pia baadhi ya mambo yaliyoitikisa wizara hiyo ni mauaji na utekaji wa watu, miili kuokotwa katika fukwe za bahari na uadilifu usiokuwa wa kuridishwa kwa Jeshi la Polisi.

Mbunge wa Viti Maalumu, Janeth Masaburi (CCM), alimtaka Mwigulu kuleta bungeni taarifa za kifo cha aliyekuwa kiongozi wa Chadema, Chacha Wangwe na Mchungaji Christopher Mtikila.

Akichangia mjadala kuhusu wizara hiyo, alimtaka alete taarifa za uchunguzi wa tukio la watalii waliomwagiwa tindikali na makanisa yaliyochomwa moto Zanzibar.

Kwa upande wake, Lema alimshauri Mwigulu na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro, kwenda kuuza maandazi kama wameshindwa kutambua watu wasiojulikana wanaodaiwa kusababisha maiti zaidi ya 1,000 kuokotwa kwenye fukwe.

Zitto alimtaka Mwigulu aeleze nini kinaendelea wilaya za kusini mwa Tanzania kwa sababu hadi sasa zaidi ya watu 348 wamepotea.

Alisema kati ya hao 348, watu 68 wamethibitika kuwa wamefariki dunia.

Akizungumzia baadhi ya hoja zilizoibuliwa na wabunge hao, Mwigulu, alisema si kweli kwamba Serikali inahusika na watu waliopotea kwa sababu wapo wahalifu wa dawa za kulevya na wa kutumia silaha waliokimbia familia zao na kuvuka mipaka kuelekea nje ya nchi.

WIZARA YA VIWANDA

Mjadala ulioshuhudiwa wakati wabunge wakipitisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa fedha wa 2018/19 nao uliiweka katika wakati mgumu si tu wizara hiyo bali watendaji akiwamo Waziri wake, Charles Mwijage.

Wizara hiyo ambayo kimsingi ndiyo iliyobeba ajenda ya ‘Tanzania ya Viwanda’ inayotekelezwa na Serikali ya awamu ya tano, ilielemewa na hoja ambazo si mpya sana, lakini zilizochagizwa na migogoro ya mafuta na sukari ulioibuka hapo kabla, lakini pia kuporomoka kwa masoko nje ya nchi.

Hoja zilizoibuliwa na Zitto ndani na nje ya Bunge na baadae Bashe kuhusu mizozo hiyo, lakini pia viwanda, uwekezaji, gharama za kodi na kuporomoka kwa masoko nje ya nchi, ndizo ambazo ziliiweka katika wakati mgumu wizara hiyo.

Kauli ya ukali ya Spika Ndugai kwa Waziri Mwijage, akimtaka kutoa majibu yanayoridhisha kuhusu mzozo wa mafuta ya kula ulioibuka kabla ya kumalizwa na Rais Dk. John Magufuli wiki hii, lakini pia akitaka utaratibu mpya wa safari za nje kwa mawaziri, yote hayo yalitoa taswira hiyo hiyo.

Wiki iliyopita gazeti hili liliripoti juu ya mjadala uliozuka baada ya wizara hiyo kuwasilisha bajeti yake ikiwanukuu wafuatiliaji wa mambo wakianisha baadhi ya hoja ambazo walidai hazipaswi kuendelea kuachwa ama kupuuzwa ili kufanikisha ajenda ya viwanda.

Miongoni mwa hoja hizo ni ile ya kufungamanisha sekta ya kilimo na viwanda ambayo Zitto anaona ndiyo njia sahihi ya kutatua migogoro mingi ya kale, ambayo imekuwa ikiibuka mara kwa mara, ikiwamo sukari na mafuta ya kula.

Akichangia bungeni wiki hii na katika andiko lake, Zitto ambaye amekuwa akieleza hoja hiyo tangu mwaka 2016, alisema huo ndio mkakati pekee wa kupambana na tatizo hilo kwani itaongeza thamani ya mazao ya wakulima na kuhakikisha viwanda vinavyoanzishwa vitategemea kwa kiasi kikubwa malighafi kutoka ndani ya nchi, hasa bidhaa za kilimo.

Katika hesabu zake anasema iwapo jambo hilo lingetekelezwa, ziada ya sukari ambayo ingeuzwa nje, ingeweza kuliingizia taifa fedha za kigeni, dola za Marekani milioni 500, sawa na 30% ya malengo ya Mpango wa Maendeleo kwa sekta ya viwanda, wa kupata mapato ya fedha za kigeni, kiasi cha dola za Marekani bilioni tatu.

Zitto alishangaa hoja hiyo kupuuzwa na kusema huo ndio msingi wa migogoro inayoshuhudiwa sasa kwani bado hakuna mpango wa taifa wa namna ya kufidia nakisi ya sukari itokanayo na uzalishaji mdogo wa bidhaa hiyo nchini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
202,097FollowersFollow
554,000SubscribersSubscribe

Latest Articles