28.7 C
Dar es Salaam
Monday, October 25, 2021

WENYE UZITO MKUBWA HATARINI KUSAGIKA MIFUPA

Na LEONARD MANG’OHA

-DAR ES SALAAM

WATU wenye uzito mkubwa, watumiaji wa dawa kwa muda mrefu, wazee wenye umri wa miaka 50 na wagonjwa wa selimundu, wanakabiliwa na hatari ya kupatwa na tatizo la kusagika mifupa ya nyonga na magoti.

Kauli hiyo ilitolewa na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Mifupa katika Hospitali ya Aga Khan, Dk. Harry Matoyo, katika mkutano na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, uliohusisha uongozi wa hospitali hiyo na washirika wao kutoka nchini India.

Akizungumza katika mkutano huo, unaolenga kuwajengea uwezo madaktari wa hospitali mbalimbali nchini, Matoyo alisema kawaida tatizo hilo huwakabili zaidi wazee wenye umri wa zaidi ya miaka 50, lakini pia huweza kuwakabili vijana, hususan wenye uzito mkubwa.

“Uzito unapokuwa mkubwa sasa huathiri zaidi magoti kuliko hata nyonga, kwa sababu uzito unapokuwa mkubwa magoti hubeba mzigo mkubwa na kufanya mifupo kusogeleana kutokana na kupungua kwa ute uliopo kwenye ‘joint’ (maungo) ya goti na kusababisha mfupa laini kusagika na hatimaye mifupa kugusana na kuanza kusagika na kusababisha maumivu.

“Hii husababisha wagonjwa wengi huja wakiwa na maumivu katika maeneo mbalimbali na hata kushindwa kutembea vizuri,” alisema Matoyo.

Mtendaji Mkuu wa Hospitali hiyo, Siwaso Konteh, alisema wameamua kushirikiana na wadau wao hao kutoka India kutokana na kuwa na uwezo mkubwa katika kutibu kwa kutumia teknolojia.

“Wamekuja kuona nini tunafanya ambapo watasaidia kuwapa ujuzi, hasa wa kiteknolojia madaktari wetu kwa sababu watakuwa wakifanya nao kazi ya kutoa huduma ya upasuaji pamoja. Haitakuwa faida kwa Aga Khan peke yetu, bali kwa Tanzania nzima, ikiwamo Muhimbili, ambao tumekuwa tukishirikiana nao kwa muda mrefu,” alisema Koteh.

Muuguzi Mkuu wa hospitali hiyo, Lucy Hwai, alisema ushirikiano huo umelenga kuboresha uhusiano baina yao, utakaosaidia kuongeza ufanisi katika maeneo mbalimbali.

“Wametoa kiasi cha dola za Marekani milioni 80 kufadhili ujenzi wa jengo jipya hospitalini linaloendelea kujengwa, litakalokuwa na uwezo kuchukua vitanda 170 na kuongezeka kwa jengo hilo ni wazi kuwa wagonjwa wataongezeka na tutahitaji madaktari wengi kutoa huduma kwa wagonjwa hao.

“…katika siku hizio chache watakazokuwa hapa, hawa madaktari watatoa huduma ya upasuaji kwa wagonjwa ambao wamepatikana baada ya kuwafanyia vipimo, naamini hadi mwaka ujao wagonjwa wengi watanufaika kwa kutibiwa hapa baada ya jengo hili kukamilika,” alisema Hwai.

Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa Hospitali ya Prince Ally Khan, Sanjay Aok, alisema ushirikiano huo utapunguza adha kwa wananchi kupata matibabu kutokana na wengi wao kuwa masikini, hivyo kushindwa kumudu gharama za kwenda kutibiwa nje ya nchi.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
163,099FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles