29.3 C
Dar es Salaam
Thursday, May 2, 2024

Contact us: [email protected]

WAZIRI UMMY AAGIZA DAKTARI ACHUKULIWE HATUA

 

Na Samwel Mwanga


WAZIRI wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto, Ummy Mwalimu ameagiza achukuliwe  hatua daktari wa Hospitali ya Wilaya ya Maswa,  Laurent Biyengo, aliyedaiwa kushindwa kuingia kazini badala  akaenda kunywa pombe.

Inadaiwa kuwa kitendo hicho kilisababisha wagonjwa kutopatiwa huduma za utabibu.

Waziri alitoa maelekezo hayo kwa  Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI, Dk. Zainab Chaula, hivi karibuni.

Inaelezwa kuwa  baadhi ya wagonjwa waliofika katika hospitali hiyo  Septemba 27 mwaka huu   saa 1:00 hadi saa 3:30 usiku walikosa kukosa huduma kwa vile  daktari huyo wa zamu  hakuwapo.

Hali hiyo ilisababisha ujauzito aliokuwa nao Salome John   kuharibika wakati wakimsubiri daktari huyo ambayo ilidaiwa alikuwa anakunywa pombe.

Waziri Ummy aliutoa maelekezo hayo kwa   simu   baada ya kupata taarifa hizo kupitia ujumbe mfupi wa maandishi (SMS) kutoka kwa mwandishi wa   MTANZANIA kuhusu kutokuwapo daktari wa zamu hospitalini hapo.

“Nimemwelekeza Naibu Katibu Mkuu Tamisemi ashughulikie suala hilo,” alisema Waziri.

Wagonjwa waliopatwa na madhira hayo   walisema  walifika   hospitalini hapo  kwa ajili ya kupata matibabu lakini cha kushangaza daktari wa zamu hakuwapo.

Kwa mujibu wa wagonjwa hao, wauguzi waliokuwapo  walishindwa kumhudumia hasa  Salome John aliyekuwa akilia kutokana na maumivu aliyokuwa akiyapata.

Wauguzi hao walisema  taratibu  zilikuwa haziruhusu hadi waelekezwe  na daktari hali iliyosababishaujauzito wa mgonjwa utoke.

“Tulimsubiri  daktari lakini hakuonekana na  ilipofika saa 3:20 usiku maumivu yalimzidi binti yangu na   hatimaye mimba yake ikatoka,” alisema Suzana Kalumbilo ambaye ni mama mzazi wa Salome John.

Walieleza  kuwa baada ya kuona hali inazidi kuwa mbaya walimpigia  simu  Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dk. Seif Shekalaghe ambaye naye alichukua jukumu la kumpigia simu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dk. Jonathan Budenu.

Dk. Budenu   alifika muda mfupi baada ya kupigiwa simu na DC Dk.  Shekalaghe na kufanya jitihada za kupata daktari mwingine ambaye alifika na kuanza kutoa huduma kwa wagonjwa waliokuwapo, walisema wagonjwa hao.

Walisema Ilipofika   saa 3:40 usiku ndipo  Bihengo alipofika akiwa amelewa   lakini Dk. Budemu alimtoa nje na kumtaka asitoe huduma yoyote kutokana na hali aliyokuwa nayo.

Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dk .Shekalaghe alisema amesikitishwa na kitendo hicho na kueleza kuwa hawezi kuwavumilia watumishi wa serikali wa namna hiyo.

Alisema watumishi wa aina hiyo  wamekuwa wakiichonganisha serikali na wananchi kutokana na kutotimiza majukumu yao.

Hata hivyo aliulaumu uongozi hospitali hiyo kwa kushindwa kuwasimamia watumishi wa aina hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles