22.2 C
Dar es Salaam
Friday, October 11, 2024

Contact us: [email protected]

Waziri awasilisha Azimio la Mkutano Mkuu wa ILO katika Kamati ya Bunge

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako, amewasilisha azimio la kujumuisha suala la Usalama na Afya Mahali pa Kazi katika misingi minne ya awali ya Shirika la Kazi Duniani (ILO) ya haki katika maeneo ya kazi katika vikao vya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria vinavyoendelea jijini Dodoma.

Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, akijibu baadhi ya hoja za wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria katika kikao cha Kamati hiyo ambacho Waziri Mwenye Dhamana ya Masuala ya Kazi, Prof. Ndalichako, aliwasilisha azimio la ILO ambalo suala la Usalama na Afya Mahali pa Kazi lilijumuishwa katika misingi minne ya awali ya Shirika hilo ya haki katika maeneo ya kazi.

Azimio hilo lilipitishwa na kwa kauli moja na Nchi Wanachama wa ILO (Tanzania ikiwemo) katika Mkutano Mkuu wa 110 wa Shirika la Kazi Duniani uliofanyika Geneva, Uswisi kuanzia Mei 27 hadi Jun 11, 2022 ambapo Waziri Mwenye dhamana ya Masuala ya Kazi, Prof. Ndalichako alihudhuria akiwa ameambatana na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Khadija Mwenda pamoja na watendaji wengine wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu).

Mkufunzi wa OSHA, Moteswa Meda, akiwasilisha mada kuhusu masuala ya huduma ya kwanza mahali pa kazi katika Kamati ya Bunge Katiba na Sheria ambapo wajumbe wa Kamati hiyo wamefundishwa kwa vitendo namna ya kuwahudumia wafanyakazi wanaopata changamoto mbali mbali za kiafya mahali pa kazi ikiwemo kupoteza fahamu, kuumia, kupata athari za sumu na kemikali.

Misingi ya awali ya ILO ya haki mahali pa kazi ni pamoja na; Uhuru wa kujumuika na utambuzi wa haki ya majadiliano ya pamoja (freedom of association and the effective
recognition of the right to collective bargaining), Kukomesha mifumo yote ya kazi za
kushurutishwa na kulazimishwa (the elimination of all forms of forced or compulsory
labour), Kukomesha ajira za watoto (the effective abolition of child labour), na Kukomesha kwa ubaguzi kwenye ajira na mahali pa kazi (the elimination of discrimination in respect of employment and occupation).

Kwa mujibu wa azimio hilo lililopitishwa mwaka jana, suala la usalama na afya mahali pa kazi (a safe and healthy working environment) unakuwa ni msingi wa tano wa haki katika maeneo ya kazi.

Akiwasilisha azimio hilo mbele ya Kamati ya Katiba na Sheria, Waziri Ndalichako, amesema, Ofisi ya Waziri Mkuu imeona ni muhimu kuishirikisha Kamati kuhusu azimio hilo ili kuiwezesha kuyafahamu mabadiliko hayo na hivyo kuendelea kutekeleza jukumu lake la kuishauri Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi ya OSHA ipasavyo hususan katika masuala Usalama na Afya nchini.

“Waheshimiwa wabunge tumeona ni vema tukawasilisha kwenu azimio hili ambalo limepitishwa na Nchi Wanachama wa Shirika la Kazi Duniani na nchi yetu ikiwemo
hivyo kutokana na azimio hili masuala ya Usalama na Afya mahala pa kazi yanakuwa si wajibu wa Kisheria pekee bali haki ya msingi mahali pa kazi,” Waziri Ndalichako ameieleza Kamati ya Katiba na Sheria.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria,
Joseph Mhagama, amemshukuru Waziri Ndalichako kwa jitihada anazofanya katika
kuhakikisha kwamba Kamati hiyo inawezeshwa kutekeleza jukumu lake la kuisimamia Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi chini yake kupitia semina na mafunzo mbali mbali ambayo amekuwa akiyaandaa kupitia Taasisi anazoziongoza.

Nae Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, ameishukuru Kamati kwa miongozo na ushauri ambao imekuwa ikiitoa katika kuendelea kuboresha masuala ya Usalama na Afya mahali pa kazi ambapo ameahidi Taasisi yake kuendelea kufanya kazi kwa bidii pamoja na kutekeleza maelekezo na kufanyia kazi ushauri ambao umekuwa ukitolewa na Kamati hiyo.

Wasilisho hilo la Waziri Ndalichako katika Kamati, limefanyika sambamba na mafunzo ya huduma ya kwanza mahali pa kazi ambapo wabunge hao wamefundishwa kwa vitendo namna ya kuwahudumia wafanyakazi wanaopata changamoto mbali mbali za kiafya mahali pa kazi ikiwemo kupoteza fahamu, kuumia, kupata athari za sumu na kemikali.

OSHA ni Taasisi ya Serikali chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) wenye jukumu la kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ya mwaka 2003.

Sheria hii pamoja na mambo mengine inawataka waajiri wote kuhakikisha kwamba maeneo yao ya kazi yanatambulika na OSHA ili kufikishiwa huduma muhimu ukiwemo ukaguzi wa usalama na afya, ushauri wa kitaalam pamoja mafunzo muhimu ya usalama na afya mahali pa kazi.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Joseph Mhagama (kushoto) akifuatilia wasilisho la Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako, katika kikao cha Kamati hiyo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Joseph Mhagama (kushoto) akifuatilia wasilisho la Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako, katika kikao cha Kamati hiyo.

Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria wakifuatilia wasilisho la Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako, kuhusu azimio lililopitishwa na Nchi Wanachama wa Shirika la Kazi Duniani katika Mkutano wa 110 uliofanyika Geneva Uswisi Juni mwaka jana.
- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

  1. Hapo kila mtu anafikiria posho atakayofutika mwisho wa kikao .
    Kuanzia mkutano wa Geneva hadi kamati ya wabunge. Nchi ya kulamba asali
    Hakuna zaidi

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles