31.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 11, 2024

Contact us: [email protected]

Watumiaji dawa za nywele hatarini kupata upara

Na VERONICA ROMWALD-DAR ES SALAAM



WATUMIAJI dawa za kisasa za kulainisha nywele wapo katika uwezekano mkubwa wa kupata matatizo ya ngozi na kunyonyoka nywele siku za usoni (kuwa vipara).

Hayo yalielezwa Dar es Salaam jana na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Ndani, Grace Shayo wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), alipozungumza na MTANZANIA katika mahojiano maalumu.

Alisema hali hiyo inaweza kuwapata watumiaji kwani baadhi ya kemikali zilizochanganywa kutengeneza dawa hizo zinapotumika huenda kuathiri afya ya ngozi.

“Ni kweli matumizi ya dawa za nywele yanaweza kusababisha mtumiaji kuishia kupata matatizo ya ngozi, kuna wakati mtu akipakwa dawa hizi ngozi yake huungua.

“Kutokana na kule kuungua, kama ngozi ya kichwa itapona na kuacha kovu, basi sehemu hiyo yenye kovu inaweza isiote nywele tena kama ilivyokuwa hapo awali katika maisha yake,” alisema.

Alisema kwa kawaida mtu anapopaka dawa yoyote kwenye ngozi kuna kiwango fulani ambacho hufyonzwa na ngozi yake kuingia ndani ya mwili.

“Kimsingi dawa yoyote ile ya kupaka au ya kuchua hufyonzwa kuingia ndani ya mwili kupitia ngozi.

“Ingawa tafiti zilizopo hazioneshi uhusiano wa moja kwa moja wa matumizi ya dawa za nywele na madhara, lakini jamii inapaswa kujua kwamba huathiri afya ya ngozi na viungo vingine.

“Kwa mfano kuna tafiti zilizoonesha kuwa dawa za kunyoosha nywele, rangi za nywele na ‘conditioner’ za nywele zaweza sababisha saratani ya matiti,” alisema.

Alisema yapo magonjwa ya ngozi ya aina nyingi na kwamba kuna mengine ambayo hurithiwa tangu wakati wa uumbaji wa mtoto.

Dk. Grace alisema si kila ugonjwa wa ngozi unatokana na maambukizi ya vimelea hai kama bakteria, fangasi na nyinginezo.

Alisema matibabu dhidi ya magonjwa ya ngozi ya kurithi hutegemeana na aina ya ugonjwa husika.

“Ndiyo maana tunashauri jamii kufika hospitalini kwa uchunguzi zaidi ili wapatiwe matibabu sahihi dhidi ya magonjwa ya ngozi yanayowakabili,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles