Watu 60 hufariki dunia kila siku kwa TB

0
1133

Mwandishi wetu, Mwanza

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, amesema Tanzania imefanikiwa kupunguza vifo vitokanavyo na ugonjwa wa TB lakini bado kwa siku watu 60 hufariki dunia nchini kutokana na ugonjwa huo.

Alisema hayo wakati wa kusaini tamko la maazimio ya viongozi wa dini lililobeba ajenda ya mapambano dhidi ya ugonjwa wa Kifua kikuu (TB).

Alisema Baraza la umoja wa mataifa lililokutana Septemba mwaka 2018, liliweka maazimio na malengo ya  kuongeza kasi ya  kutokomeza TB  ifikapo mwaka 2030.

“Maambukizi mapya ya TB nchini yamepungua kwa asilimia 18 kulinganisha  na hali ya mwaka 2015 na hivyo kufanya Tanzania  kuwa miongoni  mwa nchi saba  duniani ambazo zipo katika mwelekeo sahihi wa kufikia malengo ya mpango mkakati wa Shirika la Afya Duniani (WHO) ya kutokomeza TB kwa hatua ya kwanza ya mwaka 2020.

Aidha, Ummy alisema  vifo vitokanavyo na TB peke yake vimepungua kutoka 30,000 mwaka 2015 hadi 22,000 mwaka 2018 na hiyo ni sawa na punguzo la asilimia 27.

“Licha ya mafanikio haya, nchi bado ina vifo vingi vinavyosababishwa na TB ambapo kwa sasa takribani watu 60  hufariki kila siku hapa nchini”, alisema .

Hata hivyo alisema hadi sasa Serikali ina vituo 103 vinavyotoa huduma za wagonjwa wa TB sugu ikilinganishwa na kituo kimoja kilichokuwepo mwaka 2015.

Naye Spika wa Bunge, Job Ndugai, alisema Serikali inatenga mabilioni ya fedha katika kushughulikia masuala ya afya hususani kwenye upande wa tiba ambapo gharama za matibabu zinakuwa kubwa.

 “Wananchi wanadhani wizara ya afya inasimamia tiba tu, tusisahau kinga ni muhimu sana  dhidi ya magonjwa, tutakaposimamia kinga  Serikali itakua inaokoa gharama kwenye matibabu na kupunguza mzigo wa matibabu kama Serikali,”alisema Ndugai

Aidha, aliwashauri viongozi wa dini kwamba licya ya kusaini azimio  hilo, kuzungumza na waumini  wao suala zima la TB.

Alisema anayo imani kuwa watalibeba na kulitekeleza na kuwafanya wananchi kupata uelewa wa ugonjwa huo na kujitokeza  kupima afya zao na kuanza dawa  ili wasiwaambukize wengine.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here